6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Istiqaamah – Njia ya Waumini!

Nguvu ya kweli haiko kwenye umbo au misuli ya mtu. Wengi wanaonekana kuwa na msimamo na utofauti mpaka pale litakapoibuka jambo litakalofichua ukweli wao halisi na udhaifu wao. Kisha, kuna wale wachache ambao wanaweza kuwa hawaonekani kwa jamii lakini wana daraja kubwa kwa Mola wao. Wanaweza kuonekana dhaifu na wasio na umuhimu, lakini kumbe ni aina ya watu ambao kamwe hawapotezi njia yao. Pale ambapo watu wanapogubikwa na hofu na taabu, wao hawakunji uso hata kidogo.Hiyo ndiyo nguvu ya kuwa na Istiqaamah!

Istiqaamah ni nini?

Istiqaamah ni unyoofu, usahihi, uadilifu, utimamu na kadhalika. Inatokana na neno la Kiarabu ‘qama’ yaani ‘kuinuka’ au ‘kusimama kwa kunyooka.’

Kutokana na neno hilo, ‘qama’, tunapata maneno kama (mustaqeem) kama ilivyo katika ‘Sirat alMustaqeem’ (Njia Iliyonyooka).

Kwa Muumini, Istiqaamah ni fadhila na hadhi ambayo hawezi kuishi bila ya kuwa nayo. Ni Sifa ambayo tunajitahidi wakati wote kuifikia, ingawa wakati mwingine tunaweza kufeli.

Katika zama hizi ambapo fitna imetamalaki na kufanya dhambi hadharani limekuwa jambo la kawaida, watu wengi wamepoteza Istiqaamah waliyokuwa nayo awali. Nguvu ya kubaki kwenye njia iliyonyooka imewaponyoka!

Allah ‘Azza wa Jalla’ anataja katika Surah Fussilat: “Hakika waliosema, ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike, nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa’” [Qur’an, 41:30].

Mwenyezi Mungu anasema tena: “Basi, simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na wale wanaoelekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe. Wala msichupe mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo.” [Qur’an, 11:112].

Malipo ya Istiqaam a h katika huu ulimwengu si chochote isipokuwa Pepo, kama inavyotajwa katika aya ya kwanza kati ya mbili za hapo juu.Istiqaamah inafuatia baada ya tamko letu la Imani kwa Mwenyezi Mungu (Shahada) na ndiyo inayosaidia na kuimarisha’Tawhid’ yetu.

Kwa kuongezea katika unyoofu na umadhubuti, Istiqaamah pia inahusu kuacha dhambi na kuepuka kuchupa mipaka, kama Allah ‘Azza wa Jalla’ aliyosema katika aya iliyotangulia ‘wala msichupe mipaka” akiifanya kuwa sehemu ya amri iliyotolewa katika aya iliyopo juu.

Istiqaamah yetu haiwezi kukamilika mpaka tuwe ndani ya mipaka iliyowekwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu kupitia sharia.

Tukumbuke hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) inayomuhusisha Sufyan bin Abdullah (Allah amridhie) ambaye alikwenda kwa Mtume na kusema:

“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie kitu kuhusu Uislamu ambacho siwezi kumuuliza yeyote isipokuwa wewe.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimwambia, sema:

“Namuamini Allah na baada ya hapo kuwa mnyoofu” [Sahih Muslim].

Kama watetezi wa Uislamu, inatupasa kutambua kwamba kuendeleza Istiqaamah ni mchakato wa muda mrefu. Haitokei siku moja tu au baada ya kusikiliza hotuba moja, bali ni harakati zinazoendelea ambazo ndani yake tunaweza kujikuta tukishindwa mara nyingi.

Istiqaamah ipo katika maneno, viten- do, nia, dhamira n a hali zetu. Ni kile ambacho tabia yetu inajengeka juu yake na ndiyo kinachoamua mafikio yetu Siku ya Malipo. Katika historia yote ya Kiislamu, akisi ya Istiqaamah imeng’ara kutoka kwa watu wazito.

Kwa kweli Mitume ambao walikuwa mstari wa mbele kuongoza ulimwengu huu chini ya muongozo wa Mwenyezi Mungu walikuwa na Istiqaamah hasa!

Kulingania taifa ambalo limezama kwenye ukafiri na ‘shirk’ siyo kazi rahisi unapokuwa peke yako. Ni rahisi sana mtu kukimbia baada ya kuona dalili ya kwanza tu ya kukataliwa, lakini haikuwa hivyo kwa Mitume amani ya (Allah iwashukie).

Mwenyezi Mungu amewafanya Mitume kuwa madhubuti katika njia yake na amejenga ndani yao ‘Istiqamah’ wanayoihitaji ili kukabiliana na kazi yenye mitihani mizito kama hiyo.

Maswahaba wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) walilelewa na Qur’an ambayo si tu iliwabadili haraka, bali pia iliwajenga kuwa madhubuti na waadilifu. Istiqaamah na subira yao ilikuwa kubwa kiasi kwamba madhila ya kutisha waliyokabiliana nayo hayakutosha kuwatikisa, wala kuwafanya watoe kauli potofu. Maswahaba walikuwa kama mwamba uliosimama imara dhidi ya mawimbi makali yanayouzunguka.

Istiqaamah inahitajika wakati wa faraja, kama vile inavyohitajika wakati wa dhiki. Hii ni kwa sababu, wakati moyo unapoanza kuhisi usalama na kujiamini kwa majivuno kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, basi jua kuwa moyo huo ushaingia fitna na umeshindwa.

Ni wakati wa vipindi hivi ndiyo watu wengi wanaanza kuteseka kutokana na usahaulifu. Maono yao yanahama kutoka Akhera na kwenda duniani, na hivyo vitendo vyao vinaanza kulenga kupata na kuvuna manufaa ya ulimwengu kwa gharama ya dini yao.

Ni katika vipindi hivi ndiyo mtu anakuwa kipofu kwa dhambi zake, na hivyo haoni haja ya kutubu. Hiyo ndiyo sababu wema waliotangulia waliogopa sana vipindi virefu vya raha na faraja katika maisha yao.

Istiqaamah hata hivyo, hairuhusu kabisa mtu kupotoshwa kwa urahisi.Inamzuia mtu kuwa na udhaifu kama huo katika Uislamu wake na kuudumisha moyo wake na miguu katika Njia Iliyonyooka.Istiqaama inawafanya watu kuwa madhubuti iwe wakati wa ugumu au faraja.

Istiqaamah ya moyo

Ibn Rajab (Allah amrehemu) amesema: “Mzizi wa Istiqaamah upo kwenye moyo unapokuwa madhubuti katika Tawhid.”

Kuwa na Tawhid sahihi ni muhimu katika kila dakika ya Uislamu wa mtu. Tawhid sahih ni kumtambua Allah ‘Azza wa Jalla’ kama Mola na Muumba wetu na kufanya ibada zetu zote kwa ajili yake na kutakasa imani yetu kwake.

Tunapaswa kujifunza kumpenda Yeye, kuogopa adhabu yake na kuwa na matumaini ya malipo yake. Tujifunze kuwa na ‘Tawakkul’ (kumtegemea Allah) na tuhakikishe tunaikana miungu yote potofu, kama vile alivyowahi kuulizwa Abubakr (Allah amridhie): “Istiqaamah ni nini?” naye akajibu: “Kutomshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote.”

Kwa kauli hiyo, Abubakr alimaanisha kwamba Istiqaamah ya mtu inajengwa na uadilifu wa dhati n a Tawhid sahihi.

Moyo ukiwa kwenye kitovu cha maisha, ndiyo nguvu ambayo mara nyingi husukuma vitendo vyetu vingi. Hiyo ndiyo sababu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Kwa hakika, ndani ya mwili kuna kipande cha nyama ambacho kinapokuwa sawa, basi mwili wote unakuwa sawa; na kinapofisidika, basi mwili wote unafisidika. Kwa hakika kipande hicho ni moyo.”

Kwa hiyo, moyo ambao umejengwa juu ya Tawhid utaamrisha na kulingania kufanya matendo mema. Ibn Rajab (Allah amrehemu) ameuita moyo kama ‘Mfalme wa mwili’ kwa kuwa unatiiwa na kufuatwa.

Baadhi ya kauli za Salaf kuhusu Istiqaamah

Wanazuoni mbalimbali na watu wema kutoka katika Historia ya Kiislamu wametoa kauli kadhaa na kushauri kuhusu ‘Istiqaamah.’

Ali bin Abi Talib na Ibn Abbas (Allah awaridhie): “Istiqaamah ina maana ya kufanya mambo ya faradhi (mambo ya wajibu katika Uislamu).” Kwa upande wao, Mujahid amesema: “Kuwa mnyoofu na madhubuti katika ‘La ilaha illa-Allah’ mpaka utakapokutana na Mwenyezi Mungu.” Naye Khalifa wa tatu muongofu, Uthman bin Affan (Allah amridhie) amesema: “Istiqaamah ni kutakasa matendo yako kwa ajili ya Allah (yaani kuwa muadilifu katika matendo).” Hasan al-Basri naye kaizungumzia Istiqaamah kasema: “Kuwa madhubuti na mnyoofu katika amri za Mwenyezi Mungu. Fanya kazi katika utiifu wake na jiepushe na kutokuwa mtiifu kwake.”

Ibn al-Qayyim ananukuu baadhi ya watu wenye elimu waliosema:

“Kuwa rafiki wa Istiqaamah na siyo mtafuta heshima na utukufu (miongoni mwa watu) kwa sababu nafsi yako inatafuta hii heshima na utukufu, wakati Allah ameitaka (nafsi yako) kutafuta Istiqaamah.

Ibn al-Qayyim pia amesema: “Nilimsikia Ibn Taymiya akisema: ‘Utukufu mkubwa zaidi upo katika uwepo na mahitaji ya Istiqaamah.”

Hitimisho

Hii ndiyo Istiqaamah ambayo tunaihitaji sana ili kulinda dini yetu, kujijenga katika hii Dunia, na kuwasili salama Akhera. Istiqaamah ndiyo itakayotusaidia dhidi ya maadui wetu na dhidi ya shetani na jeshi lake. Pia, Instiqaamah ndiyo itakayotusaidia kufanya maamuzi yenye nguvu na sahihi katika maisha yetu yote na kuyasimamia maamuzi hayo kimadhubuti.

“Hakika waliosema, ‘Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakabaki wanyoofu (istiqamu) hawatakuwa na hofu, wala hawatahuzunika. Hao ndiyo watu wa Peponi, watadumu humo, kuwa ni malipo kwa waliyokuwa wakiyatenda.” [Qur’an, 46:13-14].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close