6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Ibada ya Dhikri Katika Hijja

Dhikri katika ibada ya hijja ni jambo lililopewa uzito na umuhimu mkubwa. Hii ni ibada yenye kujitegemea na yenye mafungamano ya karibu baina ya mja na Mola wake. Hakuna ibada inayokosa katika malengo yake uwepo wa kusudio la kumtaja na kumkumbuka Allah. Hii ina maana kuwa, ibada zote katika Uislamu zimewekwa kwa lengo la kumtaja Allah.

Dhikri ni ibada inayojitegemea

Mwenyezi Mungu anasema: “Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru,” [Qur’ an, 2:152]. Hii inaonesha kuwa, katika maisha ya muislamu hakuna jambo muhimu kuliko kukithirisha ibada ya dhikri. Allah Mtukufu anatuambia: “Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni asubuhi na jioni,” [41:42].

Abuu Hurayra (Allah amridhie) amesema: “Siku moja Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa anatembea katika njia ya kuelekea Makka, akapita katika jabali moja linaitwa Jumdaan akasema: Tembeeni, hili ni jabali la jumdaan, wametangulia Almufarriduun: Wakasema Almufarriduuna ni akina nani? Akasema: Wanaume na wanawake wenye kumtaja sana Allah,” [Muslim].

Dhikri ilivyofungamana na ibada nyingine

Dhikri pia inafungamana kwa ukaribu na ibada ya swala, kama anavyobainisha Allah Aliyetukuka: “Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana Mungu ila Mimi tu. Basi Niabudu Mimi, na ushike swala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi,” [Qur’ an, 20:14]. Aya hii inaonesha kuwa, ibada ya swala ni sababu na ni sehemu ya kumtaja Allah Mtukufu.

Hijja na ibada ya dhikri

Dhikri ni ibada inayochukua nafasi kubwa katika ibada ya hijja. Matendo yote ya hijja, yani kutufu, kutembea baina ya Swafa na Marwa (Kusa’ayi), kurusha mawe, kuchinja na mengineyo, makusudio yake ni kumtaja Allah. Allah Aliyetukuka anasema:

Si vibaya kwenu kuitafuta fadhila ya Mola wenu Mlezi. Na mtakapomiminika kutoka Arafa mtajeni Mwenyezi Mungu penye Masha’ril Haram. Na mkumbukeni kama alivyokuongoeni, ijapokuwa zamani mlikuwa miongoni mwa waliopotea. Kisha miminikeni kutoka pale wanapomiminika watu, na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha: hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu. Na mkishatimiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya watu wanaosema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani! Naye katika akhera hana sehemu yoyote,”[Qur’ an, 2:198-200].

Ukizitazama aya hizi kwa umakini na mazingatio, utaona namna dhikri ilivyochukua nafasi kubwa katika maeneo mbalimbali. Inajulikana wazi kuwa Allah amekataza watu kuzungumza maneno machafu wanapokuwa katika ibada hii adhimu. Hapa ndipo ambapo, dhikri huchukua nafasi kubwa katika ibada ya hijja.

Allah anaendelea kusema: “Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazohesabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka katika siku mbili (akarejea), si dhambi juu yake; na mwenye kukawia pia si dhambi juu yake, kwa mwenye kumcha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake,” [Qur’ an, 2:203].

Siku zilizokusudiwa hapa ni zile za ‘Tashriiq’ au kuchinja, ambazo Mwenyezi Mungu anawaamuru mahujaji wakithirishe kufanya dhikri baada ya kufanya matendo mengi ya hijja.

“Na watangazie watu Hijja; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.

Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia ucha mungu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyokuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema,” [Qur’ an, 22:27-28].

Katika aya hizi Allah anaonesha kuwa malengo ya kuwepo kwa ibada ya hijja ni kuwafanya watu wapate manufaa makubwa na waweze kumtaja Allah ndani ya siku hizi maalumu kutokana na kuwaruzuku na kuwapa manufaa ya aina mbalimbali.

Hivi ndivyo linavyodhihiri wazi jambo la dhikri katika ibada ya hijja kupitia aya za Qur’ an zinazozungumzia ibada ya hijja na matendo yake. Dhikri imechukua nafasi kubwa katika kila eneo panapotekelezwa ibada ya hijja, hivyo kutomtaja Allah katika maeneo haya matakatifu ni kupoteza fursa kubwa ya ibada ya ibada ya hijja ambayo msingi wake ni kumtaja Allah.

Ni vema hujaji aimarishe muda wake kwa kumtaja Allah Mtukufu, akiwa njiani, katika mapumziko na katika hali yoyote.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close