6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Hakika hiyo ni kazi ya shetani

Imepokewa kutoka kwa Qays bin As–sakan Al–Asad (Allah amridhie) kwamba, Abdullah Ibn Mas’uud (Allah amridhie) aliingia kwenye nyumba ya mwanamke aliyekuwa amevaa shanga nyekundu, akazikata (shanga hizo) na kusema:

“Hakika familia ya Abdullah haihitaji shirk.” Kisha Ibn Mas’uud akataja mambo aliyoyahifadhi kutoka kwa Mjumbe wa Allah (rehema na amani imshukie). Ibn Mas’uud alimsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Visomo (ruqya) visivyothibiti, hirizi (At–Tamaaim), limbwata (At–Tiwaalah) – vyote hivyo ni shirk.” [Haakim/ Silsilatu As–swahiha, uk. 331].

Mafunzo ya tukio

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwajenga Maswahaba zake katika misingi ya kumtegemea Allah ‘Azza Wajallah’. Hii inatokana na ukweli kuwa, kila kitu katika ulimwengu huu kinafanyika chini ya makadirio yake Allah ‘Azza Wajallah’na matakwa yake.

Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibnu Mas’uud (Allah amridhie) kwamba siku moja aliona uzi katika shingo ya mkewe akamuuliza, ni kitu gani hiki? Mkewe akajibu: “Ni zindiko (kinga).”

Ibnu Mas’uud aliushika uzi huo kwa mkono wake na kuukata kisha akamwambia mkewe: “Nyinyi familia ya Abdullah hamuhitaji shirk.” [Ibnu Majah]. Ibnu Mas’uud (Allah amridhie) alimkataza mkewe kuvaa uzi akitambua kuwa hilo ni kosa litakalomgharimu Siku ya Kiyama.

Ruqya (Kisomo cha kinga)

Tunashuhudia mara kwa mara watu wakisomewa ruqya kutoka na na matatizo mbalimbali. Hata hivyo, yafaa tutambue kwamba wapo watu wanaosoma kisomo (ruqya) kilichothibiti kwa dalili sahihi za kisharia, na wengine – ima kwa kujua au kwa kutokujua hufanya ruqya inayokwenda kinyume na sharia ya Uislamu.

Kufanikiwa kwa mtu au kutatuliwa shida yake hakumaanishi moja kwa moja kuwa kisomo alichofanyiwa ni cha kisharia, kwani wakati mwingine Iblis (shetani aliyelaaniwa) humpambia mtu jambo kwa lengo la kuwapoteza watu huku wengi wao wakidhani wamefanikiwa.

Abdullah alipomkataza mkewe kuvaa uzi shingoni, mkewe alijitetea kwa kusema:

“Naapa kwa Allah kuwa jicho langu lilikuwa linauma, na nilikuwa nakwenda kwa myahudi anayetibu kwa kisomo (ruqya). Anaponisomea jicho langu hutulia.” Abdullah (Allah amridhie) akasema: “Hakika hiyo ni kazi ya shetani. Shetani alikuwa anashika jicho kwa mkono wake, akilisomea linaacha. Hakika ilikuwa inatosha wewe kusema kama alivyokuwa akisema mjumbe wa Allah ‘Liondoshe tatizo ewe Bwana wa watu. Ponya, hakika wewe ndiye mponyaji. Hakuna ponyo jingine lisilokuwa la kwako, ponyo lisilobakisha ugonjwa.’” [Abu Daudi].

Kuna aina nyingi za visomo visivyokubalika kisharia. Miongoni mwa visomo hivyo ni kisomo (ruqya) ambacho maana ya matamshi yake haifahamiki, na kisomo kinachotokana na majina ya majini na mashetani au kinachofanywa kwa namna ambayo haikubaliki katika sharia ya Kiislamu.

Hirizi ya kishirikina (Tamimah)

Asili ya neno ‘Tamimah’ni shanga walizokuwa wanavishwa watoto wachanga kwa ajili ya kuwakinga na kijicho, zongo na mfano wake. Waarabu waliziita ‘Tamimah’kwa sababu waliamini kuwa ni kinga na ponya madhubuti kwa watoto wao.

Lakini kwa upande wa sharia ya Kiislamu, neno hili ‘Tamimah’linagusa kila kitu kinachotundikwa au kuvalishwa watoto, wanyama au wagonjwa kwa lengo la kuwakinga na maradhi mbalimbali na matatizo mengine.

Miongoni mwa hirizi za kishirikina ni matalisimu yanayoandikwa na waganga wa kienyeji kwa lengo la kuwakinga watu na maradhi, vijicho na husda. Mengi ya matalisimu haya yanalenga kutaka msaada kwa mashetani na mara nyingi hutundikwa kwenye nyumba, magari na sehemu za biashara.

Uislamu umekataza watu kuvaa pete zenye vito vya aina fulani kwa ajili ya kutii matakwa ya majini, kuvaa ringi ya shaba au fedha kwa dhumuni la kupata baraka au kujikinga na maradhi au kuvaa uzi wenye jina maalumu kwa lengo la kujikinga na matatizo.

Kuvaa ngozi, kuwavalisha watoto uzi/ kamba nyeusi na kutundika hirizi kwenye nyumba kwa makusudio mbalimbali hayo yote ni katika matendo ya shirk. Hirizi zote tulizozitaja hapo juu hakuna hata moja yenye manufaa kwa mwanadamu.

Katika jumla ya hirizi ni kuandika aya za Qur’an na adhkaar na kuzifunga katika ngozi au kitambaa kisha kuzifunga kwa watoto au wagonjwa. Hata hivyo, wanazuoni wa Kiislamu wametofautiana kuhusu jambo hili.

Pamoja na kwamba jambo hili lina ikhlafu, ni vema Muislamu akajitenga nalo kwa sababu hadith zilizothibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) zimezungumza jambo hili kwa ujumla pasina kuhusisha aina fulani ya hirizi.

Baadhi yetu tumekuwa tukitundika hirizi zenye aya za Qur’an au adhkaar mbalimbali za kisharia tukiamini kuwa hiyo ni njia sahihi ya kujikinga na husda, kijicho na matatizo mengineyo. Kujikinga kwa sura hii hakujathibiti katika Qur’an wala Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Tiwala (Limbwata)

Hii ni aina nyingine ya ushirikina unaotumika sana katika maisha ya wanandoa. Uchawi huu unaohusiana na mapenzi hutumiwa sana na wanawake ili wapendwe na kufurahiwa na waume zao. Katika kuzungumzia uchawi huu, Imamu Al–Khattwabi (Allah amrehemu) amesema: “Hii ni aina mojawapo ya uchawi.” [Aunul–Ma’abud].

Ni wajibu kwa Waislamu kusahihisha itikadi zao hasa katika mambo ambayo yanafungamana na manufaa au madhara. Waislamu waelewe kuwa, hakuna chenye kunufaisha au kudhuru pasina makadirio na matakwa ya Allah. Kujiwekea kinga za kishirikina kwenye nyumba, kwa watoto na sehemu nyingine yote haya ni mambo ya haramu ambayo Muislamu anapaswa kujiepusha nayo.

Ni vizuri Muislamu akajisomea mwenyewe Aya za Qur’an na akishindwa si vibaya akasomewa na mtu mwingine kwa kuzingatia mipaka ya kisharia. Napenda kuchukua fursa hii kuwasihi wale wanaowasomea watu ruqya, wasilifanye jambo hilo kuwa ni biashara au kulifanya kwa ahadi na uhakika kuwa watu waliowasomea wataondokewa na matatizo. Kupona ama kutokupona hakutokani na uwezo au umahiri wa msomaji, bali jambo hilo lipo chini ya milki ya Allah ‘Azza Wajallah’.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close