6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Fanya haya upate radhi za Allah

Kuridhiwa na Allah ni miongoni mwa neema kubwa ambayo wataipata watu wa peponi. Lakini hili si jambo jepesi kwani radhi za Allah hazipatikani isipokuwa kwa kufanya yale yatakayokuwa ni sababu ya kuridhiwa huko.

Sote tuna matumaini ya kupata radhi za Allah, lakini yapasa tuelewe kuwa hazipatikani isipokuwa kwa njia zake. Tunasoma ndani ya Qur’ an kuwa wapo watu ambao Allah ameshawaridhia kama ilivyothibiti katika aya na hadith mbalimbali.

Mathalan katika Surat Tawba (Qur’an, 9:100), Mwenyezi Mungu anasema:

“Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Muhajirina na Answar, na waliowafuata kwa wema, Allah ameridhika nao, na wao wameridhika naye; amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

Hawa ni wale waliotangulia mwanzo (Muhaajiruna) katika umma wa Kiislamu na wakawa wa mwanzo kuamini, kupigana Jihad na kuisimamisha dini ya Allah. Watu hawa walihamishwa katika mji wao wa Makka, na kwa ajili ya dini, wakaacha mali zao wakitafuta radhi za Allah.

Kundi la pili ni la wale waliowapokea wageni (Ansar), wakawapa makazi, wakawapenda pasi na kinyongo, wakawafadhilisha kuliko nafsi zao licha ya umasikini uliokuwa ukiwakabili.

Hao wote Allah amewatangazia radhi zake juu yao na malipo ya pepo yenye kila aina ya neema na ubora kutokana na yale waliyoyafanya. Haya ni makundi ya watu ambao wametangaziwa kufuzu kama anavyotufahamisha Mwenyezi Mungu.

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipofungamana nawe (Muhammad) chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa ushindi wa karibu.” [Qur’an, 48:18].

Allah anaelezea fadhila zake na rehema katika kuwaridhia Waumini kutokana na kumpa ahadi ya utii Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), ahadi ambayo ilipelekea kuchuma furaha ya duniani na Akhera, na ikawa sababu ya wao kuridhiwa na Allah.

Ahadi hii au kiapo hiki kinachojulikana kwa jina la ‘Ba’ atur Ridhwaan’ (kutokana na kuridhiwa na Allah Aliyetukuka) huitwa pia kiapo cha watu wa mti. Nacho ni kiapo kinachorejea pale Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipokuwa anafanya mazungumzo na washirikina katika tukio la Hudaibiya.

Katika tukio hilo, Mtume aliwakusanya Maswahaba wapatao 1,500 alioambatana nao kwenye msafara wake na akachukua ahadi ya utii kutoka kwao, kuwa wapo tayari kwa mapambano na hakuna yeyote atakayekimbia.

Kwa utayari wao, Allah aliwatangazia kuwa amewaridhia kwa kitendo chao hicho. Maswahaba walioshiriki katika ukombozi huu ni wale waliokula kiapo chini ya mti (Bay’atur Ridhwaan), ambao pia walihusika na faida ya ngawira kama sehemu ya malipo waliyoahidiwa na Allah Aliyetukuka.

Kutokana na mafanikio hayo ya Maswahaba, tunayo haja ya kufuata sababu zitakazopelekea kupata radhi za Allah. Kuna mambo mengi yametajwa katika Qur’an na Sunna za Mtume, ambayo ni sababu au njia ya kupata radhi za Allah. Hapa tutataja baadhi ya m a m b o hayo.

Mosi: Imani na matendo mema

Kumuamini Allah Ta’ala na kutenda matendo mema, ni mambo mawili yanayolazimiana. Imani isiyoambatana na matendo mema haina thamani, na pia matendo bila imani hayana thamani mbele ya Allah. Haya ni mambo mawili yanayosababisha mja kupata radhi za Allah na malipo ya kudumu katika pepo.

Allah Aliyetukuka anasema: “Hakika walioamini na wakatenda mema, hao ndiyo bora wa viumbe. Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni bustani za daima, zipitazo mito kati yake. Wakae humo milele. Allah Yu radhi nao, na wao waradhi naye. Hayo ni kwa anaye mwogopa Mola wake Mlezi.” [Qur’an, 98:7–8].

Watu bora mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaomuamini yeye na kutenda mambo mema. Allah Ta’ala atawaingiza peponi Siku ya Kiyama na wataishi humo milele. Hii ni kwa sababu, Allah amekubali matendo yao na amewaridhia. Uimara wa imani zao na juhudi ya kutenda yaliyo mema umewapelekea kupata radhi za Allah Aliyetukuka.

Pili: Uchamungu

Ucha Mungu ni moja ya sababu zitakazopelekea mtu kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Allah anasema:

“…Nikuambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamungu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake waliotakaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.” [Qur’an, 3:15].

Allah anaeleza kuwa wale wenye kumcha na kusimamia vema utumishi wao kwake watapata kila aina ya kheri ambazo jicho halijapata kuona, sikio halijapata kusikia na wala moyo haujapata kuhisi, lakini kubwa kuliko yote ni kupata radhi za Allah.

Tatu: Ukweli

Miongoni mwa sifa zinazopelekea kupata radhi za Allah ni ukweli. Tunapozungumzia ukweli tuna maana ya kuwa mkweli katika vitendo na nia kwa ajili ya Allah, waja wa Allah na kwa nafsi yako mwenyewe. Sifa hii itamfanya mja siyo tu kupata radhi za Allah bali pia kusalimika na adhabu ya Siku ya Kiyama.

Allah anasema: “Mwenyezi Mungu atasema, ‘Hii ndiyo siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao. Wao watapata bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.’” [Qur’an, 5:119].

Wakweli ni wale ambao matendo yao yamenyooka na kuwa sawa na kauli zao na nia zao. Hawa ni wale wanaofuata njia iliyonyooka na wakafuata muongozo ulio sawa.

Nne: Kuamrisha mema, kusimamisha sala na kutoa zaka

Haya ni matendo yanayopelekea mja kupata radhi za Allah Aliyetukuka. Allah anasema:

“Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu, Mwenye Nguvu, Mwenye Hekima.” [Qur’an, 9:71].

Katika aya hii, Allah Ta’ala anabainisha kuwa, Waumini wanaume na wanawake, wenyewe kwa wenyewe ni wenye kupendana na kusaidiana, wanaamrishana mambo mema yanayotambulika kisharia ikiwemo tabia njema na itikadi sahihi.

Tano, kuharakia katika kumtii Allah

Allah Aliyetukuka ananukuu kauli ya Nabii Musa akisema:

“‘Na nini kilichokutia haraka ukawaacha watu wako ewe Musa?’ Musa akasema, ‘Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia Mola wangu Mlezi ili uridhike.’” [Qur’an, 20:83–84].

Allah alikuwa ameahidi kumteremshia Nabii Musa Taurati kwa muda wa siku 30, lakini akatimiza ahadi hiyo kwa siku kumi. Licha ya ahadi kutimia, bado Musa alikuwa na shauku na pupa ya kuendelea kumuelekea Mola wake kwa ajili ya kupata ufunuo (Wahyi). Ndipo Allah akamuuliza Musa, ni jambo gani limemfanya ashindwe kuwasubiri jamaa zake? Musa alijibu kuwa amefanya haraka kwa sababu ya kutaka radhi za Mola wake. Mja yeyote mwenye haraka ya kutii maagizo ya Allah hufanya mambo yenye kumridhisha ili apate ridhaa ya Mola wake Mlezi.

Sita: Kumshukuru Allah

Allah anasema: “Na mkishukuru yeye huridhia hilo kwenu nyinyi.” [Qur’an, 39:7].

Katika aya hii, Allah anatutaka tumshukuru kwa kumpwekesha, kumtakasia dini na kumwabudu kwani hayo ni mambo yanayomridhisha. Tukifanya hivyo tutapata rehema zake na baraka katika maisha haya ya dunia na kesho Akhera.

Saba: Kujitakasa na shirk

Allah Aliyetukuka anasema: “Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allah) ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika bustani zipitazo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndiyo Hizbullahi (Kundi la Mwenyezi Mungu). Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.” [Qur’an, 58:22].

Katika aya hii, Allah Aliyetukuka anawaagiza Waumini kujenga urafiki na watu wenye imani ya Mungu mmoja na kuwachukia wale wenye kumfanyia uadui, hata kama watakuwa ni jamaa zao wa karibu.

Watu wenye wasifu kama huu ndiyo ambao Allah amethibitisha nyoyo zao kwa kuwa imani zao hazitetemeshwi wala kuathiriwa na matatizo ya kilimwengu na tamaa zake. Hawa ndiyo ambao Allah Ta’ala ameridhia matendo yao na kamwe hatowakasirikia Siku ya Kiyama, nao watakuwa wameridhia takrima walizozipata kutoka kwa Mola wao.

Nane: Kuridhika na makadirio (mpango) wa Allah

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika malipo makubwa yanakwenda sambamba na mitihani, na kwa hakika Allah anapowapenda waja huwatahini. Atakayeridhia basi naye atapata radhi za Allah na atakayekasirika atakasirikiwa.” [Tirmidhiy].

Mitihani ni dalili ya kheri wala si shari, hivyo ni wajibu kwa aliyekumbwa na matatizo kusubiri na kuvumilia ili apate radhi za Allah.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close