6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Faida za kuchanganyika na watu

Wakati mmoja Nabii Daudi (amani ya Allah imshukie) alikaa faragha (peke yake) mithili ya mtu mwenye huzuni. Allah Aliyetukuka akamuuliza: “Mbona uko kimya.” Nabii Daudi akajibu: “Ewe Mola wangu, nimewahama watu wangu kwa ajili yako.” Allah akamwambia: “Nikujulishe jambo ambalo ukilifanya utawatangulia watu (utaziteka nyoyo zao) na kuzifikia radhi zangu?” Akasema: “Ndio (nijulishe).” Allah akamwambia: “Changanyika na watu kwa tabia zao na imarisha imani yako kwangu.” [Ibn Rajab/ Jaamiul – Ulumi Walhikam].

Mafunzo ya tukio

Nabii Daudi (amani ya Allah imshukie) alijitenga na watu ili apate wasaa mzuri wa kumuabudu Allah ‘Azza Wajallah’. Lakini Allah, kwa hekima na ujuzi wake uliotukuka alimfunza Nabii Daudi njia bora zaidi ya kupata radhi zake ambayo ni kuchanganyika na watu na kuvumilia kasoro (mapungufu) zao.

Inajulikana kuwa mwanadamu ni kiumbe wa kijamii (hawezi kuishi peke yake), hivyo ni lazima achanganyike na makundi mbalimbali ya watu ili aweze kupata mahitaji yake.

Ni hakika kwamba wanadamu wanategemeana. Hakuna awezaye kujigamba eti, anajitosheleza kwa kila kitu. Kila mmoja kati yetu anamuhitajia mwingine kwa namna moja au nyingine.

Ni muhimu sana kuchanganyika (kushirikiana) na watu kwa sababu, katika jamii yoyote watu hutofautiana viwango vya elimu, ujuzi na uwezo wa kutatua matatizo yanayoikabili jamii, taasisi au nchi.

Hata hivyo changamoto kubwa inasalia katika kutofautiana tabia na dhamira za watu. Lililo muhimu ni watu kuvumiliana na kuheshimiana ili kuenzi umoja na undugu wa kibinadamu.

Mchango wa tabia njema katika kuboresha maisha ya watu

Tabia njema ina nafasi kubwa katika kuboresha maisha ya watu na kuepuka matendo mabaya kama vile ufisadi, ulaji rushwa na mengineyo.

Ni ukweli usiopingika kuwa tabia njema inachangia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi katika kazi, pia ni kipimo cha uaminifu kwa watu. Zaidi ni kwamba tabia njema huleta maelewano, ushirikiano na uhusiano chanya miongoni mwa wanajamii.

Hisia za upendo, kuhurumiana, kuheshimiana na kuaminiana zinapokita katika nyoyo za watu, jamii huishi kwa amani na utulivu na hivyo kuondosha uwezekano wa watu wanyonge kunyanyaswa, kunyonywa na kudhulumiwa. Mtu aliyejipamba kwa vazi la tabia njema za Kiislamu hawezi kuwadhulumu wengine kwa sababu ana hofu na Mungu.

Athari ya tabia njema katika jamii

Athari ya tabia njema katika jamii yoyote hudhihirishwa na uchache wa matatizo yaliyopo katika jamii hiyo. Hii inatufunza kuwa tabia njema ndio msingi madhubuti na imara unaojenga jamii yenye kuwajibika katika nyanja zote.

Tabia njema ni kinga dhidi ya matatizo yanayoikabili jamii na yanayoweza kuharibia utulivu, amani na mafungamano baina ya watu. Kuna tofauti kubwa kati ya jamii iliyojipamba na tabia njema na jamii isiyotaka kujua jambo lipi ni baya na lipi zuri.

Kwa kawaida watu hutofautiana tabia, fikra, haiba na matarajio yao kwa kiwango kikubwa. Kundi moja linavyofikiri na kufasiri changamoto wanazokumbana nazo ni tofauti na linavyofikiri kundi lingine. Tofauti hizi ndizo hasa zinazotufanya tulazimike kuchanganyika na watu. Ukweli ni kwamba usipochanganyika na watu huwezi kufika mbali.

Faida za kuchanganyika na watu

Kuchanganyika na watu ni chachu ya kupata maendeleo endelevu ya kiuchumi kijamii na kidini. Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Muumini anayechanganyika na watu na kuvumilia maudhi yao ni bora kuliko yule ambaye hachanganyiki na watu na kuvumilia maudhi yao.” [Tirmidhi na Ibn Majah].

Kulingana na hadith hii, Muislamu anatakiwa achanganyike (ajumuike) na watu na avumilie maudhi yao kwa kuwa kufanya hivyo kuna faida na tija kubwa kwake, ikiwamo kuvuna thawabu nyingi katika sala za jamaa msikitini na katika ibada ya hijja.

Mbali na faida za kidini, pia mijumuiko hutoa fursa kwa watu kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu mpya za kimkakati zitakazowezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Mtu anayependa kujitenga hawezi kujifunza mambo mazuri kutoka kwa wengine.

Namna ya kuienzi tabia njema

Tabia ni muonekano wa nje wa fikra za mwanadamu. Tabia ya mtu hudhihirishwa na matendo au maneno yake ambayo hutafsiri yale yaliyopo moyoni mwake. Watalaamu wanasema tabia hurithiwa kutoka kwa wazazi (baba na mama) na pia hujengwa na jamii inayomzunguka mwanadamu.

Vigawanyo vya tabia

Tabia zimegawika katika makundi mawili. Kuna tabia njema na tabia mbaya. Shabaha ya Uislamu ni kuhakikisha waja wanajipamba kwa tabia njema ili kupata radhi za Allah na si kutafuta sifa au umaarufu.

Mafundisho ya Uislamu yanalenga kujenga mafungamano endelevu kati ya wazazi, watoto na jamaa wa karibu sambamba na kuchunga haki za majirani Waislamu na wasiokuwa waislamu kulingana na mipaka aliyoiweka Allah ‘Azza Wajallah’. Hivyo yatupasa tujipambe kwa tabia njema ili tupate radhi za Allah na hatimaye tuingie kwenye pepo yake.

Umuhimu wa tabia njema unakuja pale unapochukuliwa kama kipimo cha utu na ustaarabu. Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi wanadamu tumeteremsha kwenu mavazi na mapambo na vazi la uchaMungu hilo ndiyo bora zaidi.” [Qur’an, 7:26].

Kwa kulitambua hilo, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewatuma Mitume na Manabii ulimwenguni ili waje kufundisha jamii zao adabu na tabia njema.

Na miongoni mwa tabia njema zenye uzio mkubwa kwa Muislamu ni kuwaheshimu na kuwathamini watu wote (wakubwa na wadogo), kuchukia maovu na kuyapiga vita, kusaidia masikini, yatima na wajane, kuwahurumia wanyama, kuwazuru wagonjwa na kulea watoto katika misingi na maadili ya dini.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close