6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Dini ipi ni stahiki mwanadamu kuifuata?

Maudhui ya makala hii tunadhani ina umuhimu wa aina yake, hususan katika zama zetu hizi zilizojaa fitna. Tunasema haya kwa sababu katika wakati huu ambapo duniani kuna mamia ya dini, baadhi ya wafuasi na hata viongozi wa dini wamekuwa wakipigia chapuo dhana ya dini mseto kwa lengo la kuleta na kudumisha amani.

Msingi wa dhana ya dini mseto ni kuwafanya wa wafuasi wa dini tofauti wakiri kuwa dini za wenzao pia ni sahihi na zote ni njia za kuwafikisha salama kwa Muumba wao (kwa wanaoamini kuwepo kwake). Wanaoipigia chapuo dini mseto wanahisi ndio njia bora ya kudumisha utangamano.

Hata hivyo wafuasi wa dhana ya dini mseto wanasahau kuwa ingawa Uislamu ni dini inayolingania amani, lakini pia ni dini yenye misingi yake ambayo lazima izingatiwe. Moja ya misingi yake muhimu ni kukanusha dini zote zilizoundwa na mwandamu.

Kwa mujibu wa mafunzo ya itikadi ya Kiislamu, mtu haiwezi kukubaliwa imani yake na kuwa Muislamu wa kweli mpaka aikufuru, aikane mifumo yote iliyotengenezwa na wanadamu. Pia, Muislamu analazimika kuamini kwamba Uislamu ndiyo dini sahihi zilizobakia zote ni upotofu na mwisho wa wafuasi wake ni motoni.

Allah Aliyetukuka anasema: “Hakuna kulazimishwa (katika kuingia) katika dini, uongofu umeshapambanuka na upotofu. Basi anayemkataa shetani na akamuamini, Allah bila shaka ameshika kishiko chenye nguvu kisichovunjika, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.” [Qur’an 2: 256].

Katika aya nyengine, Mwenyezi Mungu anasema: “ Na atakayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake, naye akhera atakuwa katika wenye hasara (kubwa) [Qur’an 3: 85].

Hapa ndipo kwenye mtihani kwani Muislamu hatakiwi moyoni mwake kuwa na hata chembe ya dhana kwamba Uislamu na sheria zake haufai kushika hatamu katika maisha ya watu na ya kwamba eti sheria zake ni ngumu na zinamkandamiza au kumnyima haki mwanadamu. Muislamu anapaswa kujua kwa hoja makini kwa nini amechagua na kubaki katika Uislamu.

Ni katika muktadha huo ndiyo nimeandika makala hii ili kuzichambua sifa za dini inayomfaa mwanadamu na anayostahiki kuifuata na kisha kubaini mapungufu ya mifumo waliyoitengeneza wanadamu, inshaAllah.

Maumbile ya mwandamu

Kutokana na maumbile yake, mwanadamu hupenda kuishi maisha yenye maana na lengo (purpose) na yenye kumpatia furaha, usalama na amani.

Kwa hiyo, kinadharia mwanadamu angelipenda kufuata njia (dini) itakayomuhakikishia kufikia aina hiyo ya maisha. Hapa tutataja baadhi ya sifa za dini itakayompatia mwandamu mahitaji hayo tuliyoyataja.

Dini ijengwe juu ya misingi ya ukweli

Dini ya haki anayohitaji mwanadamu ni lazima ijengwe juu ya msingi ya ukweli unaokubaliana na maumbile. Dini hiyo pia imueleweshe mwanadamu nafasi yake halisi hapa ulimwenguni.

Kwa maana nyengine, dini hiyo imuoneshe, kwa hoja, nini chanzo cha ulimwengu na vilivyomo, imfahamishe mwanadamu asili yake, lengo la kuwepo kwake na jinsi ya kulifikia.

Dini ya kweli haitamdanganya mwanadamu kuwa eti ulimwengu huu hauna muumbaji bali uliibuka tu, na wala hauna anayeuendesha. Dini hiyo haitamdanganya mwanadamu kuwa maumbile yaliyomzunguka hayana malengo na yatatoweka hivyo hivyo. Dini ya namna hiyo itamfanya mwandamu aishi maisha yasiyo na maana.

Dini iendane na maumbile

Ili mwanadamu aishi maisha ya furaha, amani na kuepukana na migongano ni lazima afuate mfumo wa maisha unaoenda sambamba na utaratibu kanuni za maumbile. Kwa maana nyengine, dini ya kweli lazima imuundie binadamu utaratibu ama sheria zinazofuatwa na maumbile.

Iwapo patakuwa na dini inayomfanya mwanadamu aendeshe maisha yake ya kimwili na kiroho kinyume na utaratibu wa nguvu za asili zinazomzunguka itampelekea aishi maisha ya matatizo yenye migogoro na upinzani mkali baina yake na maumbile hayo.

Kwa hiyo dini ya kweli lazima iweke sheria zinazolingana na sheria zinazoyatawala maumbile makubwa au nguvu za asili.

Dini imtosheleze mwanadamu mahitaji yake

Hii nayo ni sifa muhimu ya dini ya kweli. Tumeshagusia hapo juu kwamba, dini ya kweli lazima itoe majibu sahihi juu ya ukweli wa maumbile yanamzunguka mwanadamu, nafasi yake hapa duniani, lengo la kuja kwake, namna ya kulifikia na pia imuelekeze hatima ya maisha yake ni nini.

Dini ya kweli pia itosheleze hisia za mwanadamu kwani kawaida mwanadamu huwa na hali tofauti. Kama mwanadamu yupo katika hali ya furaha kwa kupata mafanikio fulani, dini ya kweli imuelekeze namna bora na salama ya kusherehekea.

Kamwe haitakuwa dini ya kweli ambayo itamuachia mwadamu afanye furaha yake, madaraka yake, utajiri wake, ushindi wake na umaarufu wake viwe chanzo cha misiba yake, kudhalilika kwake, kudharaulika kwake au kuwadhulumau na kuwanyanyasa wengine.

Kwa upande wa pili, mwanadamu hufikwa na hali ya huzuni na machungu yaliyotokana na kuharibikiwa katika maisha. Dini ya kweli, kadhalika, lazima imuelekeze namna ya kukabiliana na hali kama hizo.

Dini ya kweli imliwaze mwanadamu, impe matumaini na kumsubirisha kwa ahadi ya kweli ya malipo makubwa ya baadae – yaani imjengee msingi wa baada ya dhiki faraja.

Dini ambayo itamuacha mwanadamu afe kwa huzuni, akate tamaa, awaangukie wengine miguuni kwa kuwaabudu, ama ayachoke maisha, itakuwa si dini inayostahiki mwanadamu kuichagua.

Dini ifuatwe na ulimwengu mzima

Dini ya kweli ni hitajio la watu wote. Hivyo, lazima iwe ndiyo dini iliyofuatwa na mwanadamu katika vipindi vyote tangu kuanza historia yake hapa ulimwenguni. Dini hiyo pia lazima ibaki mpaka mwisho wa historia yake ili kila mwanadamu aipate na aweze kuishi maisha ya furaha, yenye maana na kufikia lengo.

Kwa hivyo, dini ya kweli ni dini ya watu wote, wa zama zote na wa sehemu zote za ulimwengu. Dini hiyo haina budi kutokuwa na mipaka ya kijografia wala ya wakati. Kwa ajili hiyo, dini ya kweli haitapewa jina linaloambatana na mtu, mahali au wakati.

Dini ya kweli iwe ni njia ya maisha iliyokamilika

Ni lazima dini ya kweli imuwekee mwandamu utaratibu wa maisha utakaomuwezesha kukiendea kila kipengele muhimu cha maisha binafsi, familia, taifa na kimataifa. Dini ya kweli, vilevile, imuongoze mwanadamu katika maisha yake kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kiroho na utu wake.

Kadhalika, dini hiyo imuelekeze mwandamu namna ya kuabudu na namna ya kuoanisha ibada na maisha ya kila siku. Haitakuwa ni dini ya kweli ambayo mwanadamu anayostahiki kuichagua iwapo itatenganisha ibada na utendaji wa kila siku au kumuwekea mwanadamu mipaka ya utumwa wake kwa yule anayemuabudu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close