6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Allah amejiharamishia dhuluma, basi nawe usidhulumu

Dhuluma inatajwa kuwa miongoni mwa makosa makubwa yaliyokatazwa katika Kitabu kitukufu cha Qur’an pamoja na Hadith za Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah zimshukie). Katika dini ya Uislamu dhuluma imetajwa kama jambo lenye kuangamiza na kuleta athari kubwa katika maisha yetu ya kila siku na akhera tuendako.

Ndugu yangu Muislamu, kabla ya kusonga mbele zaidi tujiulize ni kwa nini vitendo vya dhuluma vimekuwa vikizidi kila uchao? Kwa nini dhuluma imekuwa ni sehemu ya maisha yetu? Je, hatuoni kwamba tukidumu katika dhuluma tutaangamia? Jawabu la maswali haya ni rahisi.

Kwa kiasi kikubwa, dhuluma imeongezeka kwa sababu Waislamu tumeacha maelekezo na maamrisho ya dini na kujifanyia tutakayo sisi wanadamu. Tulipoacha maelekezo ya Allah, tumejikuta tumetekwa na ushawishi wa shetani.

Wakati tumetopea katika dhuluma, tumesahau kuwa dhambi hiyo huangamiza na ndio maana Mwenyezi Mungu na Mtume wake, katika Qur’an na Sunna wametuonya tuache dhuluma. Kwa namna yoyote ile, Muislamu hapaswi kukubali kudhulumiwa na wala yeye asimdhulumu mtu yeyote, hata wa imani tofauti na yake. Qur’an Tukufu inasema:

“Msidhulumu wala msidhulumiwe.” [Qur’an, 2:279].

Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu, Waislamu wanakatazwa kufanya vitendo vya dhuluma hivyo ni busara kwa kila Muislamu kuacha kufanya dhuluma na pia ni busara kuacha kuhimiza au kuiunga mkono dhuluma.

Dhuluma ni dhambi kubwa na yenye kumchukiza Allah Aliyetukuka ambaye kupitia Qur’an amesema hawapendi madhalimu. Sasa basi kwanini wanadamu tudhulumu!? Jambo la kujiuliza ni je, Waislamu tupo tayari kuchukiwa na aliyetuumba kwa sababu ya dhuluma? Hakika hakuna Muislamu thabiti atakayekuwa tayari kuchukiwa na Allah Aliyetukuka kwa kuendekeza dhuluma. Wakati mwingine wanadamu tunafanya mambo kwa makusudi; lakini mara nyingi tumekuwa tukifanya mambo hayo hayo kwa mazoea, pengine tukiona tupo sahihi bila ya kujua kwamba tunakosea. Huu ni ujinga wa hali ya juu.

Kwa kuzingatia ukubwa wa dhambi ya dhuluma, ni vema tukajifunza mazingira yote ya dhuluma pamoja na kuzifahamu athari zake. Kujifunza mazingira ya dhuluma inaweza kuwa sababu ya kuachana na vitendo hivyo viovu.

Aina za dhuluma

Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu na ufafanuzi wa Hadith za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), zipo aina mbalimbali za dhuluma.

Dhuluma ya mja kwa Mola wake

Dhuluma ya kwanza ni ile ya mja kwa Mola wake. Hii hutokea pale mja anapokwenda kinyume na maelekezo ya Mola wake kwa kumkanusha Allah, yaani hufanya kufuru kwa Muumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Qur’an inasema:

“Na waliokufuru ndiyo waliojidhulumu,” [Qur’an, 2:254].

Aina hii ya dhuluma haishii hapo tu bali pia kitendo cha mja kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu kingine katika ibada huingia katika aina hii ya dhuluma. Na dhuluma hii, kwa mujibu wa Qur’an, ndiyo kubwa na isiyo na msamaha. Qur’an imekataza dhuluma hii kwa kusema:

“Usimshirikishe Allah, hakika shirk ni dhuluma kubwa mno.” [Qur’an, 31:13].

Dhuluma ya mja kwa mja mwenzake

Kadhalika, ipo dhuluma ya mja kwa mja mwenzake. Dhuluma hii hutokea pale mja anapomtendea ubaya mwenzake au viumbe vingine vya Mwenyezi Mungu kwa kuvunja au kuchukua sehemu ya haki isiyokua yake. Allah Aliyetukuka anatuambia katika Qur’an Tukufu:

“Enyi mlioamini! Msiliane mali zenu kwa batili…” [Qur’an, 4:29–30].

Pia, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Yeyote atakayemega haki ya Muislamu kwa kiapo chake alichoapa ili imuhalalikie, basi kwa kufanya hivyo Allah amekwishamuwajibishia moto na kumharamishia pepo.” [Muslim].

Dhuluma ya mja dhidi ya nafsi yake

Ipo pia dhuluma ya mja kwa nafsi yake. Hiki ni kitendo cha kuacha maamrisho ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ambayo mja anatakiwa kuyatekeleza na kuacha yale yote yaliyokatazwa, ambayo mja hujifanyia na kujidhulumu mwenyewe. Allah anasema:

“Nao hawakutudhulumu sisi walipohalifu amri yetu lakini walikua wanajidhulumu nafsi zao kwa kuacha kututii.” [Qur’an, 2:57].

Athari ya dhuluma

Kwa ujumla, dhuluma huleta athari kadhaa. Dhuluma mara nyingi hupelekea ugomvi na kufarakana baina ya watu, huzorotesha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kupelekea taifa kuingia katika umasikini; na pia husababisha uadui na kuzorotesha usalama wa watu na mali zao. Mbaya zaidi ni kuwa wanaodhuluma, mwisho wa maisha yao, moto mkali wa Allah unawasubiri.

Allah Aliyetukuka anatuambia: “Enyi mlioamini! Msiliane mali yenu kwa dhuluma, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemu. Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhalimu, basi huyo tutamuingiza motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 4:29–30].

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Madhalimu na wasaidizi wao wote kwa pamoja wataingizwa motoni.” [Dailamiy].

Ili kuleta amani miongoni mwa wanadamu, ni vema Waislamu wakawa mfano katika kuikataa dhuluma kwani ni adui mkubwa wa ustawi wa wanadamu sio tu hapa duniani bali hata kesho Akhera. Hivyo, Muislamu anasisitizwa kujiiepusha na dhuluma, kuikataa dhuluma, kupambana na dhuluma na kuwa na imani kuwa Allah ndiye mtoaji wa riziki na Yeye ndie mpokonyaji.

Kwa hakika, Allah ‘Azza Wajallah’ anampa riziki amtakaye. Na Yeye (Allah) ndiye anayepanua riziki hiyo kwa yule amtakaye, na anayepunguza riziki hiyo kwa amtakaye. Hakuna ‘Razzaaq’ zaidi Yake. Allah anasema kuhusu riziki:

“Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njia asiyoitarajia.” [Qur’an, 65:2–3].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close