9. Khutbah

Hatua 10 za Kuandaa Khutba ya Ijumaa

Ni ukweli ulio wazi kwamba wengi miongoni mwa makhatib wa sala ya Ijumaa hawaandiki khutba zao. Baadhi ya makhatib huandika nukta muhimu katika karatasi ndogo na wakati mwingine hunukuu maneno yaliyowahi kusemwa na wengine. Miongoni mwa athari hasi za kutoandika khutba ni kusahaulika haraka ujumbe wake. Hivyo, ni muhimu makhatib wakaandika khutba zao na kuzihifadhi kwa maandishi au kuzirekodi kwenye ‘CD’ na ‘DVD’ kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. Sote tunafahamu namna umma wa Kiislamu unavyoendelea kunufaika na vitabu vya Maimamu wakubwa wanne: Imam Abu Hanifa, Imam Malik, Imam Shafi na Ahmad bin Hambal. Hapana shaka yoyote kwamba kuwapo kwa vitabu hivyo kunatokana na juhudi zilizofanywa na wanazuoni waliopita (Allah awarehemu) ambao walishirikiana kuviandika na pia kuvihifadhi ili visipotee. Umma wa Kiislamu utaendelea kufaidika na elimu za maimamu hao mpaka pale Allah Mtukufu atakapoirithi ardhi hii na vilivyomo juu yake.

Maandalizi ya khutba na mambo ya kuzingatia

Khatib anaweza kuandaa vizuri khutba yake kisha kuichapisha na kuiweka katika mfumo wa vipeperushi (posters) au kitabu kidogo na kuwagawia watu. Pia, anaweza kuiweka khutba yake katika mitandao ya kijamii ili itumiwe katika mimbari mbalimbali za misikiti ya ndani na nje ya nchi.

Khatib wa Ijumaa anatakiwa aangazie matukio muhimu yaliyojitokeza au yatakayojitokeza katika jamii ili khutba yake iwe na taathira kwa waumini. Hebu sasa tutaje mambo muhimu ambayo khatib anapaswa kuyazingatia wakati anapotoa khutba.

Mambo 10 muhimu

  • Kwanza, Khatib awasilishe khutba kwa lengo la kutafuta radhi za Allah na si kutafuta sifa, umashuhuri au kukubalika na watu.
  • Pili, Khatib atoe khutba kwa kuegemea dalili kutoka katika Qur’an Tukufu na Sunna (Hadith) sahihi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).
  • Tatu, khatib akusudie kuwafundisha watu mambo ya dini yao upande wa kiitikadi, kisharia na kitabia.
  • Nne, Khutba itawale hisia, akili na mioyo ya watu.
  • Tano, khatib awatahadharishe watu dhidi ya kufanya mambo yanayochukiza na kuangamiza umma.
  • Sita: Khutba ilenge kujibu changamoto zinazowakabili Waislamu na jamii kwa ujumla na kuzitafutia ufumbuzi wenye tija.
  • Saba: Khatib asifumbie macho vitendo viovu vinavyofanywa na watu wasiotambua thamani ya utu na heshima ya binadamu.
  • Nane, khatib aheshimu na kujali hisia za Waislamu kwa kutamka maneno mazuri yenye staha pindi anapohutubia.
  • Tisa, khatib asimshambulie mtu au kumvunjia heshima yake kwa kumtaja jina au wasifu wake isipokuwa kwa dharura inayoruhusiwa kisharia au kulinda maslahi ya dini. Khatib anatakiwa awasilishe khutba yake kwa lugha ya jumla.
  • Na nukta ya kumi na ya mwisho, khatib asichukue muda mrefu kuhutubia na wala asitamke maneno ya karaha, kashfa, kejeli, dharau au kutoa maneno yatakayopelekea Waislamu kugawanyika.

Kuzingatia tofauti ya uelewa

Kama ambavyo watu hutofautiana viwango vya uelewa, makhatib nao wanatofautiana viwango vya elimu na ufahamu. Tatizo lililopo ni kwamba baadhi ya makhatib wametosheka na elimu ndogo waliyonayo na hawana hamu/ kiu ya kurejea kwenye vitabu vilivyofafanua maudhui anayoiwasilisha.

Pia, kuna wanaonukuu riwaya au maandiko katika kitabu kimoja. Changamoto huja pale khatib anapodhani kuwa kitabu alichokirejea ni bora kuliko vitabu vingine. Wapo makhatib ambao katika khutba zao hunukuu maelezo kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya dini. Lakini makhatib wa sampuli hii ni wachache sana.

Kiini cha tatizo

Makhatib wengi huandaa khutba zao usiku wa kuamkia Ijumaa, asubuhi yake au muda mchache kabla ya kupanda kwenye mimbari; pia kuna wanaopanda kwenye mimbari huku wakiwa hawajui wazungumzie nini. Badala yake hutumia muda wa kati ya salamu na adhana kufikiria cha kuzungumza.

Huku ni kudharau akili za Waislamu na kupuuza khutba ya Ijumaa ambayo Allah ‘Azza Wajallah’ ameipa umuhimu mkubwa. Ukweli ni kwamba kuna tofauti kubwa kati ya khutba zilizoandaliwa na zile zisizoandaliwa. Makhatib wafahamu kuwa khutba ni sawa na kitabu na mtoaji khutba ni sawa na mtunzi wa kitabu, mtafiti ama mwandishi.

Umuhimu wa kuandika khutba

Kuandaa khutba ni jambo zuri kwani khatib hupata muda wa kufanya uchunguzi wa kile atakachokiongea. Khatib anapochukuwa uzoefu kwa wenzake ni rahisi sana kuziba upungufu alionao au kurekebisha makosa yake.

Hivyo ni vizuri kila khatib amfundishe mwenzake njia na mbinu bora za kuandika khutba ili kuweka uwiano wa kifikra na hatimaye kila mmoja afaidike na mwenzake.

Kwa kuzingatia kuwa watu hutofautiana kimawazo, kielimu na kifikra ni vizuri kila baada ya Ijumaa moja khutba itolewe na mtu mwingine tofauti na yule aliyezoeleka msikitini ili watu wajifunze Uislamu wao kutoka kwa wengine.

Hatua za kuandaa khutba ya Ijumaa

Zipo hatua kadhaa unazoweza kuzitumia kuandaa khutba ya Ijumaa, ikiwamo kuchagua maudhui ya khutba, kukusanya maandiko, nukuu, nukta muhimu za maudhui pendekezwa na kutafuta rejea (References).

Endapo khatib atachagua maudhui (mada) ya kushukuru anatakiwa anukuu aya za Qur’an na hadith za Mtume zinazozungumzia suala la kushukuru, pia adurusu vitabu vinavyozungumzia adabu na tabia nzuri kikiwemo cha Ibn Abu Dunia.

Khatib anatakiwa atoe ushahidi wa kimaandiko katika yale anayozungumza ili khutba yake iwe na mashiko na iweze kukubalika kwa wale anaowahutubia. Baada ya kunukuu ushahidi na nukta anazotaka kuzielezea, ataweka kichwa cha habari kinachoendana na mada atakayoitoa.

Kwa mfano, kupitia aya isemayo: “Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali,” [Qur’ an, 14:7], khatib anaweza kuandika anuani isemayo ‘Kushukuru ni sababu ya kuongezewa neema’.

Pia khatib anaweza kuweka vichwa vidogo vya habari (Sub–heading) kama vile ‘Faida za kushukuru na mifano ya wenye kushukuru’ au ‘Matokeo ya kukufuru neema na mifano yake’ Kisha khatib ataanza kutoa khutba kulingana na utaratibu aliouweka.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close