2. Deen

Faida za vikao vya kumtaja Allah- 1

Mwanadamu ni mwanajamii na kwa tabia yake ya kimaumbile kamwe hawezi kuishi maisha ya kujitenga; na akifanya hivyo atapata matatizo. Uthibitisho wa hili ni hali ya mabedui (Waarabu wa mashambani) katika zama za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambao walikuwa wakiishi maisha ya kujitenga na watu, jambo ambalo lilimkera Mtume na Maswahaba zake (Allah awaridhie). Pamoja na kupenda kwake kuishi kijamii, mwanadamu anapokuwa katika maeneo ya mikusanyiko amewekewa vidhibiti na mipaka ambayo anapaswa kuichunga wakati wa kuzungumza au kutenda jambo.

Uislamu unatupa miongozo na taratibu za kuzingatia ili tusivuke mipaka ya Allah, pia unatufundisha na kutuelekeza juu ya vikao na mikusanyiko yenye ubora, mavuno na faida. Vikao vipo vya aina nyingi na ndio maana ni muhimu kwa Muislamu kutafakari juu ya aina ya vikao anavyopendelea na faida au hasara anayoweza kuipata. Vipo vikao vinavyoleta hasara, na vipo nyenye faida.

Miongoni mwa vikao vyenye mavuno mazuri na faida kubwa ni vile vinavyohusiana na utajo wa Allah, vikao ambavyo watu hawaachi kunasihiana na kuusiana. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

Faida ya vikazi vyenye kutajwa Allah ndani yake ni pepo.” [Swahih Attarghiib]. 

Hadithi hii na nyinginezo imebeba bishara kubwa kwa watu wenye kupendelea kukaa vikao vya kiimani, vyenye kukusanya wasomaji wa kitabu cha Allah (Qur’ an), kumdhukuru Allah, kunasihiana na kukumbushana mambo yenye manufaa.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Pindi mtakapopita katika viwanja vya pepo burudikeni, wakasema ni vipi hivyo viwanja vya pepo? Akasema ni mikusanyiko (halqa] ya kumtaja Allah.” [Tirmidhi].

Kuna faida nyingi watu kukaa vikao vya kumtaja Allah

Kwanza ni kusamehewa madhambi pamoja na kukubaliwa dua. Wale wenye kukaa katika vikao vya kumtaja Allah hao ni katika watu wenye kustahiki msamaha wa Allah.Wao hupata yale wanayoyaomba kwake na hubadilishiwa makosa yao na kuwa mema.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakuna watu waliokusanyika kwa ajili ya kumtaja Allah, wakawa hawataki chochote isipokuwa ni radhi zake, huitwa na mwitaji kutoka mbinguni na kuwaambia kwamba simameni mkiwa mmeshasamehewa, kwa hakika makosa yenu yamebadilishwa na kuwa mema.” [Swahih Attarghiib].

Hili ni jambo jepesi ambalo ujira wake ni mkubwa. Kuhudhuria vikao vya kumtaja Allah kwa namna na sifa aliyotufundisha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kunamfanya mtu ajiweke katika mazingira ya kustahiki msamaha wa Allah.

Kuhudhuriwa na Malaika

Miongoni mwa faida anazozipata mwenye kuhudhuria vikao vya kumtaja Allah ni kule kuhudhuria malaika na kuwa pamoja nao. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika Allah anao Malaika wanaotembea na kuzunguka katika ardhi wakitafuta vikazi vya dhikri. Wanapofika katika kikao anachotajwa Allah hukaa pamoja nao na huzungukana kwa mbawa zao, wanapomaliza huachana na hupanda kwenda mbinguni (Huko mbinguni), Allah huwauliza huku akiwa anajua,‘Mmetoka wapi?’ Husema,‘Tumetoka kwa waja wako wanaokutakasa na kukutukuza na kukusifu, wanakuomba na wanakutaka ulinzi.’ Anawaambia, ‘Wanaomba nini?’ (hali ya kuwa anajua). Wanasema, ‘Wanakuomba pepo.’ (Allah) anasema, ‘Je, wamewahi kuiona?’ Wanasema, ‘Hapana ewe Mola Mlezi.’ (Allah) anasema: ‘Ingekuwaje kama wangekuwa wameiona.’ Kisha anasema, ‘Wananitaka niwalinde na nini?’Wanasema,‘Kutokana na moto.’ Anasema,‘Je, wameuona?’ Wanasema, ‘Hapana.’ (Allah) anasema, ‘Ingekuwaje kama wangekuwa wameuona.’ Kisha (Allah) anasema, ‘Shuhudieni hakika nimewasemehe na nimewapa walichoniomba na nimewakinga na kile walichoniomba niwakinge kwacho.’

Malaika wanasema, ‘Ewe Mola wetu hakika kati yao kuna mja mkosefu ambaye amekaa nao tu lakini si miongoni mwao.’ (Allah) anasema, ‘Na yeye vile vile nimeshamsamehe. Hao ni watu ambao hawi muovu yule anayekaa nao.” [Muslim].

Tazama faida ya kikao cha namna hii. Allah anazungumza na Malaika kuhusu watu hawa waliotenga muda wao, wakawa wanamtaja Allah badala ya kwenda katika vijiwe vya mazungumzo ya kupumbaza na kupoteza muda. Jambo la kuzingatia katika vikao vya kumtaja Allah ni kutumia nyiradi (Adhkaar) alizozifundisha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa namna ile ile aliyokuwa akimtaja Allah yeye pamoja na maswahaba wake.

Vikao vilivyokusudiwa hapa si mikusanyiko kama ile wanayoifanya baadhi ya watu kwa namna wanavyojua wenyewe huku wakiimba badala ya kumtaja Allah. Wakafanya hivyo wakidhani kimakosa kuwa ndiyo vikao vya kumtaja Allah!

Kwa hakika, ibada ni jambo lenye utukufu sana na anayehusishwa na ibada ni Allah pekee, mwenye nguvu na utukufu. Haifai kumtaja Allah isipokuwa kwa namna ambayo imethibiti kisharia kwani huo ndio mfumo anaoupenda na kuuridhia Mwenyezi Mungu na ndio maana ukafundishwa katika sharia.

Bila shaka Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), Maswahaba zake.(Allah awaridhie) pamoja na wanazuoni wema waliotangulia walikuwa wakimtaja Allah, nao wakatufundisha huo utajo wenyewe [adhkaar za kisharia].

Hivyo ni wajibu wetu kutii na kufuata utaratibu huo na si kuzua na kuanzisha njia ambazo hazina nafasi katika dini.

Itaendelea…

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close