4. Darasa La Wiki

Wanahubiri maadili lakini ni mafisadi

Ufisadi ni msamiati maarufu katika medani ya siasa na uchumi hususan barani Afrika. Katika Uislamu, msamiati huu umepata umaarufu kwa sababu zipo aya za Qur’ an zinazokemea ufisadi.

Mathalan, katika Surat Rum, Allah ‘Azza Wajallah’ anasema: “Ufisadi umeenea nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale yaliyofanywa na mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.” (30:41).

Kwa kutambua uzito na ukubwa wa dhambi ya ufisadi, katika nchi mbalimbali duniani utasikia watu wanasema, ‘Hawa bwana ndio mafisadi wa nchi hii, lazima wachukuliwe hatua.’ Hii ni kwa sababu, aghlabu mtu fisadi mwenye kufanya mambo kwa malengo binafsi, huwa na tamaa na ubinafsi na pia hujawa na hofu ya kugundulika juu ya ufisadi wake, kwa hiyo hutumia propaganda chafu kutaka kuhalalisha analolisimamia.

Lakini Mwenyezi Mungu anasema: “Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanaomuomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi zake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la maisha ya dunia. Wala usimtii tuliyemghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka,” (Qur’ an, 18:28).

Pamoja na usia huo wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu, inastaajabisha kuona ufisadi unafanywa kwa kiwango kikubwa katika zama hizi licha ya kuwa na madhara makubwa kiuchumi, kijamii na kidini. Haya ni matokeo ya baadhi ya tabia za kimakosa zinazoota mizizi katika jamii ambazo baadae hugeuka na kuwa ada madhubuti ambayo mtu hawezi kuikiuka na kuiacha.

Japo si haramu kuzungumzia ufisadi msikitini, lakini kwa mazoea ambayo haijulikani asili yake, baadhi ya watu wanaona kuwa haifai kutamka neno hili ndani ya nyumba za ibada kwa sababu kufanya hivyo ni kuchanganya dini na siasa.

Hali hii ndio iliyowafanya Maimamu na Masheikh wengi kushindwa kuuzungumzia ufisadi ipasavyo katika misikiti yao kwa kuona kuwa huko yapo mambo maalum yanayopasa kusemwa, na kamwe sio ufisadi. Kutokemea ufisadi kama ilivyoamriwa na dini ndiko kunakowafanya watu wengi wakiwamo wafanyakazi wa serikali na wale wa sekta binafsi waone kuwa ufisadi si jambo baya, na hivyo wanatumia vyeo (nyadhifa) walivyopewa kuhujumu uchumi.

Miongoni mwa hao wapo wanaohubiri maadili katika familia zao, lakini wao wenyewe wamezama katika lindi la ufisadi, tena wameung’ata kwa magego yao. Mwenyezi Mungu anawaonya watu wa aina hii kwa kuwaambia: “Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda? Ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda.” (61:2-3).

Na katika usimulizi wake, Usama bin Zayd bin Harith (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Ataletwa mtu Siku ya Kiyama, naye ataingizwa motoni. Utumbo wake utatoka nje, naye atayashikilia akiwa anazunguka kama anazunguka punda kwa mtambo. Watu wa motoni watakusanyika na kusema, ‘Ewe fulani una nini? Si ulikuwa ukiamrisha mema na kukataza mabaya?’ Atasema, ‘Ndio, nilikuwa nikiamrisha mema lakini siyafanyi na nikikataza mabaya, nami nikiyaendea.’” (Bukhari na Muslim).

Aya na hadithi vinadhihirisha wazi kuwa, wapo watu wanaokwenda kinyume na yale wanayowausia wengine na wao watapata adhabu kali mno. Ndugu Muislamu, elewa kuwa uchamungu si kusema ‘Laa Ilaaha Illa Llah’ pekee, bali tamko hilo ni lazima liambatane na vitendo (amali njema).

Na kwa kuwa nafsi inaamrisha mabaya, yapasa ujitoe katika nafsi mbaya yenye kuamrisha maovu na kupupia kuifika nafsi tulivu (Nafsul Mutwmainna).

Baadhi ya madhara ya ufisadi

Tubanwe na hofu ya Mungu katika yote hayo na tuache kuchukua haki zisizotuhusu kwani mara zote ufisadi huacha madhara katika jamii, ikiwamo mifarakano na visasi baina ya watu. Mbaya zaidi ni kwamba, ufisadi hufunga fursa za maendeleo jambo linalosababisha watu kupata hasira na uchungu, na hivyo kuichukia nchi yao.

Athari mbaya zaidi ni ile ambayo mja ataipata Siku ya Kiyama pale atakapoadhibiwa na Mola wake ndani ya moto wa Jahannam. Kwa kuzingatia yote hayo, Waislamu wanawajibika kuutazama ufisadi kwa jicho la tatu na kuuangalia kwa werevu kwani moja ya sifa ya watu werevu ni kuzichunguza nafsi zao kwa kila jambo na kufanya yale yatakayowafaa baada ya kufa.

Jambo la muhimu ni kutazama athari ya kila tunalolifanya kwa kuwa athari ndio kipimo cha uzuri au ubaya wa matendo ya mja. Mwenyezi Mungu anasema: “Kwani hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyokuwa mwisho wa waliokuwa kabla yao? Hao walikuwa wamewazidi hawa kwa nguvu na athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi yao. Na wala hapakuwa wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.”

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close