4. Darasa La Wiki

Wafunze Watoto Kutunza Mazingira

Agosti 1, mwaka 2017, inabaki kuwa ni siku muhimu na ya kihistoria kwa wadau wa mazingira nchini Kenya, wakikumbuka kupitishwa sheria mpya inayopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Hii ilikuwa hatua muhimu katika vita dhidi ya uchafuzi wa mazingira. Wakenya wote hongereni sana.
 
Ni muhimu kujua kuwa wanaoharibu mazingira yetu sio viumbe kutoka sayari nyingine.

Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya imekuwa nchi ya pili kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki. Huko nyuma Rwanda ilikuwa nchi ya kwanza kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo.

Kwa mtu aliyewahi kuitembelea Rwanda na hasa mji wa Kigali atakubaliana nami kuwa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki ni jambo muhimu. Kwa sasa Rwanda ni safi na inapendeza.

 

Kwa Tanzania, ijapokuwa hatujapiga rasmi marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, zipo juhudi nyingi zinazofanywa za kuhifadhi mazingira yetu. Tumesikia na kuona juhudi kubwa zinazofanywa na serikali, viongozi wa dini na asasi binafsi katika kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji. Tumesikia na kuona juhudi za kuhifadhi maziwa, mito, mabwawa na bahari.

Kwa kipekee tuwape kongole ndugu zetu wa Zanzibar kwa kupiga marufuku mifuko ya plastiki. Ukitembea katika maeneo mbalimbali ya Unguja hasa katika fukwe utaona raha. Kwa sasa suala la uhifadhi mazingira linatoa sura mpya kwa upande wa visiwani. Hongereni sana ndugu zetu.

 

Pia, ni muhimu kutambua na kupongeza juhudi za viongozi wetu wa kitaifa katika kuifanikisha vita hii ya uhifadhi wa mazingira. Juhudi hizi zimepewa nguvu kubwa na msimamo wa rais na viongozi wengine waandamizi wa kitaifa kushiriki kwa vitendo katika harakati za utunzaji mazingira. Ni imani yangu kuwa suala la matumizi ya mifuko ya plastiki punde si punde litakuwa historia.

 

Kijamii, tuunge mkono juhudi hizi za serikali kwa kuwafunza watoto wetu suala la uhifadhi wa mazingira kivitendo. Ni muhimu kujua kuwa wanaoharibu mazingira yetu sio viumbe kutoka sayari nyingine. Naam! muharibifu wa kwanza wa mazingira ni mimi, wewe na yule.

 

Naam! Sisi ndiyo ambao hukata miti kwa ajili ya kupata mkaa. Sisi ndiyo tunaotupa taka hovyo. Sisi ndiyo tunalima karibu na vyanzo vya mito. Sisi ndiyo tunaochoma misitu hovyo. Sisi ndiyo wavuvi haramu.

 
Kama wanajamii, ni muhimu tuwajengee misingi imara watoto wetu ili watakapokuwa watu wazima wafahamu umuhimu wa kutunza mazingira. Kwa masheikh na viongozi wengine wa dini, suala la mazingira ni mada muhimu ambayo waumini wanapaswa kukumbushwa mara kwa mara.
 

Waumini wetu wanapaswa kukumbushwa kuwa dunia si yao peke yao. Wanapochafua mazingira ya bahari kwa mabomu au sumu wanaleta madhara kwa viumbe wa majini, jambo ambalo ni dhuluma kwa viumbe wengine. Kwa wazazi au walezi, tutumie nyumba zetu kama darasa maalum la kuhifadhi mazingira.

 

Ni muhimu sana kuonesha kwa mfano suala la uhifadhi mazingira katika kiwango cha familia. Hii itawajenga watoto kupenda kuhifadhi mazingira na kuchukia tabia za uharibifu wa mazingira. Miongoni mwa mambo muhimu ya kufanya kwa mzazi kama sehemu ya kumuandaa mtoto wako kivitendo ni haya yafuatayo:

 

Jenga utamaduni wa kuwa na sehemu maalum ya kutupa taka

Hapo nyumbani kwako ni darasa zuri la kuwafunza watoto kuhusu uhifadhi wa mazingira. Inashangaza katika nyumba zetu nyingi hatuna utaratibu wa kuwa na chombo maalum cha kuhifadhi taka. Tenga ndoo moja, boksi, kapu au chombo chochote ambacho mtatumia kuhifadhi taka. Taka zinapojaa kuwe na sehemu maalum ya kwenda kuziweka. Inaweza kuwa ni shimo au sehemu nyingine maalum ya kuhifadhia taka.

 

Mnaomiliki usafiri/vipando, jiepusheni kutupa taka barabarani

Kama tulivyoongea kuhusu taka za nyumbani, ni muhumu pia kujiepusha na kutupa taka hovyo kwa wale mnaomiliki vyombo vya usafiri. Mwenendo wenu huu unawafundisha watoto tabia isiyofaa. Jenga utamaduni wa kuwa na chombo maalum ambacho wewe na abiria wako mtatunza taka.

 

Jadiliana na watoto kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira

Ni muhimu kujadiliana na watoto kuhusu uhifadhi wa mazingira. Waeleze kuhusu umuhimu wa mazingira na hatari inayotukabili kama tutayaharibu. Waeleze namna wao kama watoto wanaweza kushiriki katika kuyahifadhi. Unaweza pia kuwasimulia hadithi na au kuwatungia nyimbo mbalimbali kuhusu umuhimu wa mazingira kwa ustawi wa mwanadamu.

 

Wahimize watoto kuotesha miti na kutunza bustani

Ni muhimu kujua kuwa watoto wanapenda sana maua kwa kuwa yana rangi nzuri za kuvutia. Tumia mwanya huo kuwafunza watoto kutunza mazingira kwa kuotesha miti hasa ile ya matunda. Kitendo cha kushiriki moja kwa moja katika kuotesha miti kitawajenga kuamini kuwa wao ni sehemu ya watunzaji wa mazingira. Miti waliyootesha wataitunza na hawatakubali iharibiwe. Ni wazi kuwa, watakapokuwa watu wazima tabia ya kupenda kutunza mazingira itakuwa imekomaa.

Jadiliana na watoto kuhusu nishati mbadala

Kama mzazi ni muhimu kujadiliana na watoto wako umuhimu wa nishati mbadala katika uhifadhi wa mazingira. Waulize kuhusu nishati ya jua, gesi, makaa ya mawe n.k. Mijadala hii ilenge kuongeza ufahamu wa watoto kuhusu njia mbadala zinazoweza kutumika kutupatia nishati bila kuharibu mazingira
Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close