2. Deen4. Darasa La Wiki

Utukufu wa mwezi Muharram, siku ya Ashura na bid’a zifanyikazo

Sifa zote njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu ambaye amewaneemesha waja wake kwa kuwaletea misimu ya kheri ili iwe sababu ya kufutiwa dhambi zao na kuwazidishia fadhila na thawabu kutokana na mema yao. Mwezi Muharram (Mfunguo nne) ni mwezi wa kwanza wa kalenda ya Kiislamu na ni miongoni mwa miezi minne mitakatifu ambayo ni Dhul-Qaada (Mfunguo pili), Dhul-Hijja (Mfunguo tatu), Muharram (Mfungo nne) na Rajab.

Mwezi Muharram unafuatia baada ya kumalizika kwa msimu wa ibada tukufu ya Hijja. Ni kutokana na faida lukuki zilizomo ndani ya mwezi wa Muharram, leo nitazungumzia ubora, fadhila na pia kukosoa matendo ya kibid’a yanayofanywa katika mwezi huu mtakatifu. Sasa endelea…

Utukufu wa mwezi Muharram

Allah Aliyetukuka anasema: “Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni miezi 12 tangu siku aliyoumba mbingu na ardhi; katika hiyo minne ni mitakatifu, hiyo ndiyo dini ya sawa kwa hiyo msizidhulumu nafsi zenu ndani yake (miezi hiyo)”. [Qur’an, 9:36].

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema katika Hadithi iliyopokewa na Abii Bakrah (Allah amridhie): “Hakika zama zinazunguka katika mhimili wake tokea siku Allah aliyoumba mbingu na ardhi. Mwaka ni mjumuiko wa miezi 12. Katika hiyo, kuna miezi minne mitukufu: mitatu imeongozana, nayo ni Dhul–Qaada, Dhul– Hijja na Muharram; na Rajab ambao upo baina ya Jumada (Mfungo tisa) na Shaaban.” [Bukhari na Muslim].

Imam Qurtuby, Mwanazuoni mweledi katika fani ya Tafsiri ya Qur’an amesema: “Hakika Allah Aliyetukuka ameipa hadhi miezi hii mitakatifu kwa kuitaja na akakataza katika miezi hiyo watu kudhulumiana, japokuwa dhuluma imekatazwa siku zote.”

Ubora wa Mwezi Muharram

Wanazuoni wametofautina mitazamo kuhusu mwezi ulio bora zaidi kati ya miezi minne mitakatifu katika mwaka. Wanazuoni waliopita akiwamo Imam Al–Hasan na wengineo wamesema mwezi wa Allah wa Muharram ndiyo mwezi bora. Wahbi bin Jariri amesema: “Hakika Allah ameuanza mwaka kwa mwezi Mtakatifu ambao ni Muharram (Mfunguo nne). Hakuna mwezi wowote katika miezi 12 (ukitoa mwezi wa Ramadhan) ulio mtukufu zaidi mbele ya Allah kushinda mwezi wa Muharram.”

Ushahidi unaofahamisha ubora wa mwezi wa Muharram ni Hadithi iliyopokewa na Abi Hureira (Allah amridhie) kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema: “Funga bora baada ya Mwezi wa Ramadhan ni ya mwezi wa Allah Muharram. Na Sala bora baada ya sala tano za faradhi ni sala ya usiku (Qiyaamu Llayl).” [Muslim].

Ibn Qassim (Allah amrehemu) amesema: “Mwezi bora (kufanya) amali ya  sunna baada ya Ramadhan ni mwezi wa Allah Muharram, kwani (ndani yake) kuna baadhi ya sunna ambazo ni bora zaidi kuliko sunna katika baadhi ya siku kama sunna ya funga ya Arafa na siku kumi za Dhul–Hijja (Mfunguo tatu).” Naye, Ibn Rajab (Allah amrehemu) amesema: “Mtume ameuita mwezi huu kuwa ni wa Allah. Kunasibishwa huku kwa mwezi huu kwa Allah ni utambulisho wa utukufu na ubora uliomo ndani ya mwezi huu.”

Hekima ya funga ya Ashura

Sababu sahihi ya utukufu wa siku hii ni tukio kongwe na la siku nyingi lililoelezwa katika Hadithi kadhaa za Mtume, kama ilivyoelezwa katika Hadithi iliyopokewa na Ibn Abbas (Allah amridhie) kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alifika Madina, akawakuta Mayahudi wanafunga siku ya Ashura. Mtume akawauliza: “Ni siku gani hii mnayoifunga?” Wakamjibu: “Hii ni siku tukufu Allah aliyomuokoa Mtume wake Musa na jamaa zake na kumuangamiza Firauni na jeshi lake. Mtume Musa alifunga kwa kumshukuru Mola wake, hivyo na sisi tunafunga.” Mtume akasema: “Sisi tuna haki zaidi na ubora kwa Musa kuliko nyinyi.” Hivyo Mtume wa Allah akaifunga na kuwaamuru watu waifunge. [Bukhari na Muslim].

Funga hii zamani ilikuwa ni wajibu, lakini ilipofaradhishwa funga ya Ramadhan, ikatoka katika hukumu ya ulazima na kuwa sunna. Katika Hadithi nyingine iliyopokewa pia na Mama Aisha amesema kwamba, Makuraishi walikuwa wakifunga Ashura katika kipindi cha ujahili; na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) naye alikuwa akifunga na kuwaamuru watu kufunga. Lakini pindi ilipofaradhishwa funga ya mwezi wa Ramadhan Mtume alisema: “Mtu anayetaka afunge na asiyetaka aiwache.” [Bukhari na Muslim].

Fadhila na utukufu wa siku ya Ashura

Kufunga siku hii kuna fadhila kubwa. Imepokewa Hadithi kutoka kwa Abuu Qatada Al-Ash’ari (Allah amridhie) kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliulizwa kuhusu funga ya Ashura, akasema: “Hufuta madhambi ya mwaka uliopita.” [Muslim].

Wanazuoni wamesema katika ubainifu wa ufutaji wa madhambi haya: “Hakika Allah aliyetukuka husamehe madhambi madogo kwa mtu aliyefunga siku ya Ashura, ama madhambi makubwa ni lazima mtu alete toba ili Allah amsemehe madhambi yake. Mtu anayefunga sunna ya Ashura hufutiwa madhambi yake madogo na kama hana huenda akafutiwa makubwa, na kama hana ‘Insha Allah’ Allah atampatia thawabu.”

Imepokewa Hadithi kutoka kwa Ibn Abbas (Allah amridhie) amesema: “Sijapata kumuona Mtume akitilia maanani zaidi funga ya siku iliyo bora kama funga ya Ashura, na mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhan.” [Bukhari].

Namna ya kufunga sunna ya Ashura

Ufungaji wa sunna hii ya siku ya Ashura, kama alivyobainisha Mwanazuoni Ibn Qayyim (Allah amrehemu) upo wa aina tatu. Mosi, ni utimilifu, yaani kufunga siku moja kabla ya Ashura na siku moja baada ya Ashura, kwa maana kufunga siku tatu ambazo ni siku ya 9, siku ya 10 na siku ya 11.

Pili, namna ya pili ni kufunga siku ya 9 na ya 10. Aina hii ndiyo iliyoelezwa na Hadithi nyingi za Mtume. Namna ya tatu, ni kufunga siku ya 10 pekee. [Rejea: ‘Zaadul–Maad,’ juzuu 2 uk 75–76].

Ibn Abbas (Allah amridhie) amesema: “Wakati Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipofunga siku ya Ashura na kuwaamuru watu waifunge, Maswahaba walimuuliza, ‘Ewe Mjumbe wa Allah, hakika siku hiyo wanaiadhimisha Mayahadi na Manasara!’ Mtume akasema, ‘Itakapofika mwakani Insha Allah, tutafunga pamoja na siku ya tisa.’ Ibn Abbas akasema, ‘Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akafa kabla ya mwaka uilofuata kufika.’ [Muslim].

Aidha, Ibn Abbas amepokea Hadithi kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye amesema: “Fungeni siku ya Ashura na mjitofautishe na Mayahudi, fungeni siku moja kabla yake, na siku moja baada yake.” [Ahmad].

Katika kuisherehesha Hadithi hii, Imam Nnawawi (Allah amrehem) amesema: “Na huenda sababu ni kukwepa kushabihiana na Mayahudi katika kufunga kwao siku ya kumi tu.”

Uzushi wa huzuni na kuombeleza

Miongoni mwa mambo yanayokera, kuchukiza na kutia kichefuchefu ni uzushi wa Madhehebu ya Shia kuinasibisha siku ya Ashura na majonzi kutokana na kifo cha mjukuu wa Mtume, Husein bin Ali bin Abii Twalib (Allah amridhie) ambaye aliuawa shahidi katika mwaka wa mia sita Hijriya.” (Sheikh al–islami ibn taymiyya (allah amrehemu).

Katika siku ya Ashura hairuhusiwi kisharia kufanya ibada yoyote inayofungamana na siku hii isipokuwa kufunga tu. Juu ya hilo, Sheikh Al–Islami Ibn Taymiyya (Allah amrehemu) amesema: “Miongoni mwa mambo yanayokera, kuchukiza na kutia kichefuchefu ni uzushi wa Madhehebu ya Shia kuinasibisha siku ya Ashura na majonzi kutokana na kifo cha mjukuu wa Mtume, Husein bin Ali bin Abii Twalib (Allah amridhie) ambaye aliuawa shahidi katika mwaka wa mia sita Hijriya.”

Jambo lililo dhahiri ni kwamba, baadhi ya vikundi na madhehebu yamebuni na kuzusha mambo ndani ya siku hii ambayo hayana msingi wala mashiko yoyote katika Uislamu na huyanasibisha mambo hayo na Hadithi za uongo au dhaifu.

Katika siku ya kumi katika mwezi wa Muharram (Mfunguo nne), siku ya Ashura, madhehebu ya Shia huadhimisha siku hii na kuomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume Husein bin Ali ambaye aliuliwa huko Karbala katika nchi ya Iraq mwaka wa 61 Hijriya.

Uombolezaji huu haujaelelezwa na sharia yoyote ya Allah Aliyetukuka wala Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) wala watu wema waliotangulia, wala yeyote katika watu wa familia ya Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie).

Msiba wa kifo cha Husein (Allah amridhie) unapasa uchukuliwe na kuzingatiwa kama misiba mingine ya watu watukufu kwa njia zilizofafanuliwa na sharia ya Uislamu. Mfano wake ni msiba wa baba yake Hussein, Ali bin Abii Twalib ambaye naye aliuliwa kama Hussein (Allah amridhie).

Misingi itikadi ya Kishia (Raafidha)

Madhehebu ya Ahlus Sunnat wal–Jamaa, wanayahesabu na kuyazingatia madhehebu ya Shia kuwa ni miongoni mwa vikundi potofu kutokana na baadhi ya vitendo na kauli zao. Mfano, madhehebu ya Shia huamini na kuitakidi kuwa, kuna andiko la Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) lillothibitisha stahili ya uimamu wa Ali bin Abii Twalib (Allah amridhie) baada ya kufa Mtume na kwamba Ali bin Abii Twalib amehifadhiwa kutenda madhambi na hivyo yeyote aliyempinga ni kafiri.

Aidha, madhehebu ya Shia wanaamini kwamba Muhajirun (wahamiaji kutoka Makka) na Answari (wenyeji wa Madina) walilificha andiko linalompa uimamu Ali. Ni kutokana na misimamo hii ndiyo maana madhehebu ya Ahlul Sunna wal–Jamaa wanawahesabu wafuasi wa madhehebu ya Shia kuwa ni miongoni mwa vikundi potofu.

Hussein bin Ali ni nani?

Husein bin Ali bin Abii Twalib AlHashimiy anatoka kabila la Kikuraishi. Yeye ni katika wajukuu wa Mtume aliyezaliwa na binti wa Mtume, Fatima (Allah amridhie). Husein alikuwa akifanana sana na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Mtume aliwataja yeye na ndugu yake Hasan, kwa kusema: “Hasan na Hussein ni katika vijana watukufu wa peponi” [Tirmidhiy].

Naye alishiriki pamoja na baba yake katika vita vya Al–Jamal na Siffin na alipambana na Makhariji – watu waliokuwa wakimpinga baba yake (Ali) mwaka wa 60 Hijriyya.

Kuuawa kwa Husein bin Ali (Allah amridhie) kuliibua na kuchochea fitina baina ya watu, kama ilivyokuwa kwa mauaji ya Uthman bin Affan (Allah amridhie). Nayo ni miongoni mwa sababu kubwa ambazo zilisababisha fitina na umma kumeguka vipande vipande hadi leo.

Katika shari na fitna zilizozalikana kutokana na kuuawa Husein ni kuibuka kikundi ambacho kwa sababu aidha ya ujahili, dhuluma, upingaji, unafiki au upotevu, kilijikita katika kudhihirisha huruma na mapenzi kwa watu wa familia ya Husein bin Ali (Allah awaridhie wote) na kuifanya siku ya Ashura kuwa ni siku ya huzuni, majonzi na uombolizaji.

Jambo la kusikitisha ni kuwa waliyafanya haya wakiiga mila na desturi za wakati wa kijahili, kama vile kuvipiga vifua vyao na kuziparura nyuso zao na kufanya tanzia kwa kufuata mila na desturi za kijahili na zilizokatazwa.

Mtazamo wa Uislamu kuhusu msiba

Katika kuuawa kwa Hussein bin Ali (Allah amridhie), shetani alipata sababu ya kuwashawishi watu kubuni na kuzusha mambo mawili katika dini. Uzushi wa kwanza ni huzuni na uombolezaji ikiwemo kujipiga mwilini na pia kuratibu na kupanga sherehe za uombolezaji.

Uzushi wa pili ni kuwatukana na kuwatusi watu wema, kuwalaani na kusimulia visa vya uongo dhidi ya baadhi ya Maswahaba. Jambo hili, lilifungua mlango wa fitina na kuugawa umma kwani halimo katika wajibu, sunna, wala mtazamo wa makubaliano ya pamoja ya wanazuoni wa Kiislamu (Ijmai).

Kubuni uzushi wa kufanya huzuni na kuomboleza katika misiba ya zamani ni katika mambo makubwa ya haramu ambayo Allah na Mtume wake  (rehema za Allah na amani zimshukie) wameyakataza [Rejea:Minhaju Sunnatu nnabiyya juzuu: 2 Uk: 322–323].  Jambo hili linapingana na sharia ya Allah, ambayo inaamuru katika msiba watu wawe na subira na kusema: “Innaa lillahi wainnaa ilaihi rrajiuun” na kutaraji thawabu kutoka kwa Allah.

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anaelekeza katika Quran Tukufu namna ya kupokea misiba: “…..Na wabashirie wanaosubiri. Wale ambao ukiwasibu msiba husema, ‘Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, kwake yeye hakika tutarejea.’” [Qur’an, 2:155–156].

Na katika Hadithi, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Si katika sisi (Waislamu) mtu anayejipiga usoni kwa kuomboleza wakati wa msiba, au anayechana nguo zake au kupaza kelele mfano wa kipindi cha ujahili.” [Bukhari].

Aidha, Mtume wa Allah amesema: “Mimi ninajitenga mbali na mtu anayepaza sauti kwa kuomboleza wakati wa msiba na yule anayechana nguo zake wakati wa msiba.” [Muslim]. Vile vile, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie] amesema: “Mtu anayeomboleza kwa kupiga kelele iwapo hakutubia kabla ya kufa kwake atasimamishwa Siku ya Kiyama akiwa na kanzu ya shaba yenye moto mkali.”

Kadhalika, Mtume amesema tena: “Muislamu yeyote anayepatwa na msiba kisha akasema, ‘Innaa lillahi wa innaa ilaihi Rajiun’ (Sisi wote ni wa Allah na kwake yeye tutarejea). Ewe Mola wangu Mlezi nilipe katika msiba wangu huu, na unipe mbadala wake jambo la kheri.’ Allah atamjaza kheri katika msiba wake huo.” [Muslim]. Vilevile, Mtume amesema mambo manne ni katika mila na desturi za kijahili, miongoni mwa mambo hayo aliyoyataja ni kumlilia maiti kwa kupiga mayowe na kelele [Imam Ahmad].

Ikiwa mafundisho ya Allah Aliyetukuka na Mtume wake yamesema hivyo, hali inakuwaje pale uombolezaji huo unapojumuisha dhuluma kwa Waumini ikiwemo kuwalaani na kuwatukana na mengineyo ambayo hakuna anayeweza kuyahesabu isipokuwa Allah mwenyewe.

Hivyo ndivyo ambavyo Shetani amewapambia watu waovu walioifanya kuifanya siku ya Ashura kuwa siku ya huzuni, majonzi, kuomboleza, kupiga mayowe na kujipiga vifua sambamba na kutunga qasida za huzuni, na kusimulia riwaya zilizosheheni uongo kwa kiwango kikubwa na kuchochea chuki, ugomvi na kuanzisha fitina baina ya Waislamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close