4. Darasa La Wiki

Usirudie tena jambo hili ulilolifanya

Umar bin Atwaa bin Abiljauzaa (Allah amrehemu) amesimulia kwamba, Naafiu bin Jubayr alimtuma kwa Saaib (Allah awarehemu) kwa ajili ya kumuuliza jambo ambalo Muawiya (Allah amridhie) ameliona kwake (Saaib) na Muawiya akamkosoa.

Saaib akamuambia: “Ndiyo, niliswali pamoja naye sala ya Ijumaa. Baada ya Imam kutoa salamu, nilisimama palepale nilipokuwa nikiswali. Alipoingia, akanitumia ujumbe, akasema, ‘Usirudie tena jambo hilo ulilolifanya. Pindi utakaposwali Ijumaa, usiunganishe na sala nyingine mpaka utakapozungumza au utoke (sehemu uliyokuwepo) kwani hakika Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alitukataza kuunganisha sala na sala nyingine mpaka tuzungumze au tutoke tulipokuwa.” [Muslim].

Mafundisho ya tukio hili
Mara kwa mara tuwapo misikitini tunashuhudia baadhi ya watu wakitoka sehemu walizokuwa wanaswali sala za faradhi na kuhamia sehemu nyingine kwa ajili ya kuswali sunna. Huenda wengi tunafanya hivyo bila ya kujua maana na malengo ya kufanya hivyo.

Katika tukio hili, tumeona kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), aliwakataza Maswahaba kutenganisha ibada ya faradhi na sunna kwa kuhama eneo moja au kufanya Adhkaar. Katika kulifafanua hilo, Sheikh Ibnu Taymiyya (Allah amrehemu) amesema: “Sunna ni kutenganisha kati ya sala ya faradhi na sunna katika Ijumaa na katika sala nyingine, kama ilivyothibiti katika Hadithi kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amekataza kuunganisha sala na sala nyingine mpaka patenganishwe kwa kusimama sehemu nyingine au maneno (Dhikr).

Wala pasifanywe kama wafanyavyo watu wengi wanaounganisha salamu na rakaa mbili za sunna, kwani kufanya hivyo ni kuyaendea makatazo ya Mtume. Katika hili, kuna hekima ya kuipambanua faradhi na sala nyingine kama ambavyo hutofautishwa kati ya ibada na kisichokuwa ibada.” [Rejea: ‘Majmuul -fataawa,’ 24/202].

Pia, imepokewa Hadithi kutoka kwa Azraq bin Qays (Allah amridhie) akisema: “Mtu mmoja aliswali pamoja na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasimama kwa ajili ya kuswali rakaa mbili za sunna. Umar bin Khattwab (Allah amridhie) alisimama haraka, akamshika mabega na kumtikisa, kisha akamuamuru kukaa chini.”

Kisha (Umar) akasema: “Hawakuangamia Ahl-ulkitaab (Mayahudi na Manaswara] isipokuwa ni kwa sababu hapakuwa na kitenganishi baina ya sala zao.” Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema : “Amefanya vizuri mtoto wa Khatwaab.” [Ahmad, na Sheikh Albaani amesema ni Hadithi sahihi].

Kupitia tukio hili, tunajifunza umuhimu wa kutofautisha baina ya ibada moja na nyingine au ibada ya faradhi na sunna. Yapo maandiko (dalili) mbalimbali yanayohimiza kutenganisha baina ya ibada moja na nyingine. Mathalan, katika moja ya kauli zake, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amekataza kuitangulia funga ya Ramadhan kwa kufunga siku moja au mbili. Hii inaonesha uzito uliopo baina ya ibada za faradhi na sunna na kuiweka kila ibada katika daraja yake.

Namna bora ya kutenganisha ibada za faradhi na sunna
Kama tulivyobainisha katika Hadithi kuwa kinachotenganisha kati ya sala ya faradhi na sunna ni mtu kuhama mahali aliposwali sala ya faradhi au kuleta adhkaar za baada ya sala, yaani kuleta Istighfaar, Tasbih, Takbiir na nyinginezo ambazo zimethibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Jambo la kuzingatia wakati wa kuleta adhkaar ni kumtaja Allah katika utaratibu na mfumo alioufundisha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na Maswahaba zake (Allah awaridhie) na si kwa utaratibu walioubuni watu. Kumtaja Allah ni jambo lenye utukufu mno hivyo ni lazima lifanywe kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Mtume. Inafahamika kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), Maswahaba zake (Allah awaridhie) pamoja na wanazuoni miongoni mwa wema waliotangulia (Salafiy) walikuwa wakimdhukuru Allah na wakatuelekeza namna ya kumdhukuru. Hivyo, ni wajibu wetu kutii na kufuata utaratibu huo na hatupaswi kubuni njia nyingine.

Namna nyingine ya kutenganisha kati ya sala ya faradhi na sunna ni kusali sunna nyumbani. Tumeona katika mafundisho mbalimbali ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kupitia sunna zake akituhimiza kusali sala za sunna nyumbani. Mtume ametuambia: “Sala iliyo bora ni ile ambayo mtu anaisali nyumbani kwake isipokuwa sala ya faradhi.”

Pia, Imamu Nawawi (Allah amrehemu) amesema: “Sunna zinazoandamana na sala (Qabliya na Baadiya) pamoja na sunna nyingine, ni vizuri ziswaliwe mahali pengine tofauti na mahali paliposwaliwa sala ya faradhi. Sehemu bora kabisa ni nyumbani na kama si hivyo basi iwe msikitini ili mtu awe amesujudu katika maeneo mengi na aweze kuitofautisha sala ya faradhi na sunna.” [Rejea: ‘Sharhu Sahihi Muslim,’].

Jambo hili la kuitofautisha sala ya faradhi na sunna kwa Adhkaar au kwa kubadilisha eneo la kuswalia si jambo gumu, linawezekana kwa kila mmoja na ndiyo maana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anahoji akisema: “Hivi mmoja wenu anapomaliza kuswali faradhi anashindwa kusogea mbele au kurudi nyuma au kulia au kushoto? (Akikusudia kuswali Sunna).” [Rejea: Ibnu Majah na Sheikh Al–bani amesema ni Hadithi sahihi].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close