4. Darasa La Wiki

Usichokijua kuhusu Qiyamu Llayl

Katika bahati na nafasi muhimu alizonazo Muislamu zinazompatia hadhi, daraja na mapenzi makubwa mbele ya Muumba ni kuhuisha kisimamo cha usiku (Qiyamu Llayl).

Kusimama usiku kwa ajili ya kujikurubisha /kujipendekeza kwa Allah Ta’ala ni sunna iliyotiliwa mkazo mkubwa katika maisha ya kila siku ya Muislamu.

Umuhimu wa Sunna hii unaonekana katika maeneo yafuatayo: Mtume alidumu katika ibada hii, nayo ni dalili ya utukufu wake. Mama Aisha (radhi za Mungu ziwe juu yake) anasimulia:

“Mtume alikuwa akisimama usiku mpaka miguu yake inavimba. Nikasema, ‘Kwa nini unafanya haya yote ewe Mjumbe wa Allah, ilihali umeshasamehewa madhambi yako yaliyopita na yajayo?’ Akasema: ‘Basi je, nisiwe mja wa shukrani?!’” [Bukhari na Muslim].

Pia katika aya mbalimbali, Allah amewasifu waja wake wanaosimama usiku kwa ibada. Mfano wa aya hizo ni ile inayosema:

“Na wale wapitishao baadhi ya saa za usiku kwa ajili ya Mola wao kwa kusujudu na kusimama.” [Qur’an, 25:64].

Na katika kuthibitisha imani za waja hao wema, Mwenyezi Mungu anasema:

“Hakika wanaoziamini Aya zetu haswa ni wale tu ambao wakikumbushwa kwazo huanguka wakisujudu na humtukuza mola wao kwa (kutaja) sifa zake, nao hawatakabari. Huinuka mbavu zao kutoka vitandani wakati wa usiku ili kumuabudu Mola wao kwa kuogopa (moto) na kutarajia (pepo), na hutoa katika yale tuliyowapa.” [Qur’an, 32:15–16].

Mtume naye katika Hadith nyingi amebainisha umuhimu wa Qiyamu Llayl. Mwenyewe alikuwa akijitahidi sana kwa hilo kama alivyoHadithia Mama Aisha. Pia Mtume amebainisha kuwa, kisimamo cha usiku ni sababu ya mja kufutiwa dhambi zake.

“Jilazimisheni kusimama usiku kwani hiyo ni desturi ya watu wema kabla yenu, nacho ni kikurubisho kwa Mola wenu, na kifuta makosa, na kikatazaji cha dhambi.” [Tirmidhi].

Siri ya mafanikio kupitia ibada hii imebainishwa na Hadith ifuatayo:

“Sahl bin Saad amesema, Jibril (Amani imshukie) alikuja kwa Mtume na kumwambia, ‘Ewe Muhammad, ishi upendavyo lakini tambua wewe ni maiti, na mpende umpendaye lakini ujue utatengana naye, na tenda unavyopenda lakini utalipwa kwa vitendo hivyo.’ Kisha Jibril akamwambia, ‘Ewe Muhammad, utukufu wa Muumini ni Qiyamu Llayl na heshima yake ni kutosheka na kuacha kuwaomba watu.’” [Hakim na Bayhaqiy].

Usiku ni wakati wa utulivu zaidi na nafasi nzuri ya mja kunong’ona na Mola wake na kukubaliwa dua kwani moyo hupunguza mashaka ya dunia na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzingatia mtu anachokisema na anachokitenda. Mwenyezi Mungu anathibitisha hili kwa kusema:

“Hakika nyakati za usiku ndizo zenye utulivu zaidi na maneno hutua.” [Qur’an, 73:6].

Naye Mtume amesema: “Allah anakuwa karibu zaidi na mja katika usiku wa mwisho, basi mmoja wenu kama ataweza kuwa miongoni mwa wamtajao Allah katika saa hiyo basi afanye hivyo.” [Tirmidhiy na Abu Daud].

Pia Jaabir bin Abdillah (Allah amridhie) amesema: “Nimemsikia Mtume wa Allah akisema, ‘Katika usiku kuna saa ambayo mja yeyote akimuomba Allah kheri katika mambo ya dunia au Akhera, Allah atampa, na hayo ni kila usiku.” [Muslim].

Kutokana na Nusus (nukuu) hizi tunajifunza kuwa, pamoja na ibada tunazozifanya wakati wa mchana, bado tumepewa ofa (fursa) nzuri ya kujiweka karibu na Mola wetu nyakati za usiku.

Mtume amesema: “Qiyamu Llayl ndiyo desturi ya waja wema, kwa hiyo wachamungu hawatosheki na wingi wa ibada wanazozifanya mchana kwa sababu ni rahisi zaidi kushambuliwa na ria. Waja wema husimama usiku wakiitikia agizo la Allah: “Simamisha sala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na (msiache) Qur’an ya (sala) Alfajiri. Hakika kusoma Qur’an (katika sala) ya Alfajiri kunahudhuriwa (na Malaika), na katika usiku jiondoshee usingizi. Hiyo ni (ibada ya ziada) kwako, huenda Mola akakuinua cheo kinachosifika.” [Qur’an, 17: 78–79].

Na imepokewa kutoka kwa Imamu Shafi (Allah amrehemu) kwamba, aliugawa usiku vifungu vitatu. Theluthi ya kwanza aliandika, ya pili alisali na ya tatu alilala.

Kwa umuhimu huu, Muislamu anatakiwa aufanye usiku kuwa farasi wake, ampande ili amfikishe kwenye mji mtakatifu. Mashujaa wa ibada husimama usiku wakiswali na kumdhukuru Mola wao. Muislamu mkweli haendekezi porojo nyingi na majisifu au kujiliwaza kwa wingi wa twaa anapokuwa na watu mchana, halafu ukiingia usiku analala fofofo.

Muislamu mkweli halali kama mzoga kwani anaelewa kwamba Mwenyezi Mungu huiangalia ikhlas na ukweli wa ibada zake wakati wa usiku. Waislamu hatuna budi kuelewa kwamba, licha ya ibada tunazomuonesha Allah Ta’ala wakati wa mchana, pia tunapaswa kufanya ibada usiku ili kuthibitisha mapenzi yetu kwake.

Hii ni kwa sababu kila apendaye hutamani kukaa na mpenzi wake faragha na kufanya mazungumzo naye.

Kwa kuzinga- tia ukweli h u u , Mtume licha ya kuwahimiza Maswahaba zake kwa pamoja, alikuwa akiwahimiza pia mmoja mmoja kusali usiku. Kwa mfano, Mtume alimuusia Swahaba wake, Abdallah bin Amri:

“Ewe Abdallah, usiwe kama fulani, alikuwa akisimama usiku, kisha akaacha.” [Taz: ‘Bukhari Kitaabut Tahajud,’ uk. 1152].

Shetani na Qiyamu Llayl

Iblis (shetani aliyelaaniwa) anaijua vema siri ya Qiyamu Llayl; na hivyo, hufanya kila analoliweza kumtia uvivu na uzito Muislamu asiweze kusali usiku.

Katika Hadith iliyosimuliwa na Abu Huraira (Allah amridhie), Mtume amesema:

“Anapolala mmoja wenu shetani humfunga vifundo vitatu, anapotaka kuamka humwambia lala kwani bado una usiku mrefu. Muislamu akiamka na kumtaja Allah fundo moja hufunguka, akitawadha la pili linafunguka, na kama ataswali mafundo yote hufunguka na ataamka akiwa mchangamfu mwenye moyo safi. Vinginevyo, ataamka akiwa mchafu wa nafsi na mvivu.”

Tuutumie usiku kwa faida

Usiku una thamani kubwa kwa muumini wa kweli kuliko hata dhahabu au madini yoyote unayoyajua. Kwa sababu hiyo, Muislamu anashauriwa kutia nia ya kusimama usiku wakati anapoweka ubavu wake kitandani, pamoja na kufanya taratibu zote za wakati wa kulala kisharia.

Kuweka nia ya kuamka ni muhimu kwa sababu Muislamu anapolala huwa anamkabidhi usingizi wake Allah Ta’ala. Akiweka nia, halafu usingizi ukamzidi na kushindwa kuamka mpaka Alfajiri, basi Allah humlipa thawabu kamili. Mtume amesema:

“Mtu yeyote atakayetia nia ya kuswali usiku, kisha akazidiwa na usingizi, Allah humuandikia ujira wa sala yake, na usingizi wake unakuwa sadaka kwake.” [An–Nasai].

Ibada zote za usiku ni Qiyamu Llayl

Kitendo chochote anachokifanya Muislamu baada ya kuamka usiku kwa ajili ya ibada kwa lengo la kujikaribisha kwa Mola wake, huzingatiwa kuwa ni Qiyamu Llayl. Hata hivyo, sala imepewa umuhimu zaidi.

Kwa maana nyengine, mtu akitumia usiku kwa ajili ya mambo yoyote ya kheri, kisimamo kitakuwa kimepatikana. Ukiamka usiku kusoma Qur’an na kuihifadhi, kudurusu vitabu, kutunga vitabu vya dini, kuandika au kusoma makala elekezi, kuandaa darsa, kujibu maswali yaliyoulizwa, kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu, kumswalia Mtume  yote hayo na mengine katika matendo mema huzingatiwa kuwa ni matendo ya kheri. Matendo yote haya ni vema yafanywe baada ya sala

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close