4. Darasa La Wiki

Umuhimu wa kuandaa vijana wachamungu, wachapa kazi

Takwimu za kituo kinachojishughulisha na utafiti wa masuala mbalimbali, yakiwamo ya dini cha Pew Research Centre zinaeleza kuwa kuna Waislamu wapatao bilioni 1.8 duniani hivi sasa, ambao ni sawa na asilimia 24.1 ya watu wote duniani.

Hata hivyo, inakadiriwa kuwa itakapofika mwaka 2030, idadi ya Waislamu duniani itafikia bilioni 2.2. Kwa takwimu hizi, tunaona haja ya kuandaa vijana waadilifu, wachapa kazi na wachamungu ndani ya jamii.

Kwa kuwa vijana ndio msingi wa umma wa Kiislamu duniani na ndio tumaini la maendeleo, hatuna budi kuandaa mazingira yatakayowawezesha vijana kufikia maendeleo ya kielimu na
kiuchumi.

Tukizungumzia maadili, tunakusudia ni kanuni, miongozo au taratibu zinazotambulika kuwa nzuri na muhimu kwa jamii fulani, na ndani yake hubeba nidhamu, uchamungu, heshima, upendo, utu n.k.

Kimsingi maadili huathiri mwenendo mzima wa tabia ya mtu. Hivyo, ni vema tukajenga maadili ya vijana kwanza, ili kuwafanya watambue misingi ya Uislamu wao.

Ikiwa umma hautajengwa kwa maadili imara, tutakuwa tunaandaa kizazi cha watu mafisadi, majambazi, makahaba, vibaka, wezi na matapeli. Inawezekana matatizo mengi ya kijamii, kiuchumi na migogoro katika ndoa na familia, yanatokana na misingi mibovu tuliyojiwekea kama jamii.

Mwenyezi Mungu anatuambia ndani ya Qur’ an: “Na misiba inayokupateni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu, na juu ya hivi Allah anasemehe mengi.” [Qur’an, 42:30].

Endapo vijana watalelewa katika misingi ya kumjua Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie), itakuwa rahisi kwao kuepuka vitendo vinavyomong’onyoa maadili.

Na kwa kuwa maadili yanagusa kona zote za maisha ya binadamu, kuwasaidia vijana kumjua Allah na Mtume wake ni njia bora ya kuwaandaa viongozi makini, waadilifu wakweli, watakaoongoza kwa misingi ya haki, usawa, uwajibikaji na kuwashirikisha watu.

Nasema hivyo kwa sababu, kiongozi mwenye hofu ya Mungu, hawezi kuwa fisadi wala kula rushwa, hatadhulumu wala kuonea raia anaowaongoza, wala hatavumilia uonevu.

Ukisoma historia ya Swahaba Umar bin Khatwab (Allah amuwie radhi), utabaini kuwa Khalifa huyu wa pili katika Uislamu alikuwa mstari wa mbele katika kusimamia misingi ya haki na usawa kwa raia wake. Umar alifanya hivyo kwa kuzingatia yale aliyojifunza ndani ya Qur’ an na Hadithi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Katika hili, Umar alifanikiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi wake umeacha athari chanya si tu kwa Waislamu bali watu wa ‘imani zote za dini’. Kuhusu suala la uadilifu, Qur’an inatuambia: “Hakika Allah anaamrisha kufanya uadilifu na hisani na kuwapa (mahitajio na msaada) jamaa wa karibu; na anakataza machafu na maovu, na dhulma. Anakuaidhini ili mpate kukumbuka.” [Qur’an, 16:90].

Lakini haya yote hayatawezekana kama ndani ya jamii yetu hakutakuwa na utaratibu wa kuwalea watoto katika mazingira na misingi ya Tauhidi. Tutafanikiwa sana ikiwa kila jambo tunalotaka kulitekeleza katika dini na dunia yetu tutaliegemeza katika misingi ya tauhidi.

Kama Waislamu, tunapaswa kuwaandaa vijana wetu kuwa mawakala wa mabadiliko katika jamii. Kwa bahati mbaya wengi miongoni mwetu hatudhani kwamba maadili ni somo linalotakiwa kuwa na mtaala (Syllabus) maalum, yenye wasimamizi mahiri.

Katika kuandaa viongozi wachamungu na wachapakazi, jambo la awali ni kujua tunamtaka kiongozi wa aina gani? Katili, mpole, mwizi ama fisadi. Ukiona leo tuna viongozi mafisadi, walevi, waongo, wasio na huruma makatili, basi jua hivyo ndivyo walivyoandaliwa, kwa bahati mbaya ama makusudi. Kimsingi, mchakato wa kuandaa kiongozi bora hayakomi bali ni endelevu.

Ukweli usiopingika ni kwamba, tumeshindwa kuwaandaa vijana wetu kimaadili na ndio maana mara kwa mara tunashuhudia vitendo vya ulaji rushwa na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa umma.

Ili tuweze kujenga jamii imara, haja ya kuwaandaa vijana wetu kimaadili na kiitikadi ni muhimu sana. Katu hatuwezi kuwa na vijana wachamungu na wachapakazi ikiwa hatujawalea katika misingi ya kumjua na kumpenda Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani iwe juu yake).

Kama jamii tunawajibika kuwaandaa vijana wetu katika maadili ya dini na kuwafundisha kuwaheshimuwatu wote masikini, matajiri, wadogo, wakubwa, na kadhalika.

Allah ametuleta ulimwenguni ili tuwe wasimamizi wa mambo (Makhalifa) na ametupa uwezo na vipawa vya kutumia kila kilichopo ulimwenguni kwa manufaa yetu.

Na katika hili upo mtihani, ambao matokeo yake yatahudhurishwa mbele ya Mola Muumba siku ya kiyama. Hapo ndipo Allah atakapopima matendo yetu katika mizani yenye pande mbili, mazuri yetu (tuliyoyafanya) na mabaya yetu (tuliyoyafanya).

Binadamu hatuna uhuru wa kuamua tupendavyo upi uwe mwenendo wetu wa tabia, bali kipimo cha lipi jema na lipi ovu lazima kichukuliwe kutoka kwa Mola Aliyetuumba. Wajibu wetu ni kutekeleza kwa ukamilifu na uaminifu wajibu na ujumbe tuliokabidhiwa. Ikiwa hii ndio hadhi na nafasi yetu katika ulimwengu huu, ni dhahiri kuwa sisi si mabwana bali ni watumishi, hivyo inatupasa kutekeleza majukumu tuliyopewa na Muumba wetu.

Kwa maana nyingine, inatupasa kuishi na kutenda kulingana na maamrisho ya Allah Mtukufu. Pindi msimamo huu ukikubalika, na uhusiano uliopo kati yetu na Allah kueleweka, hoja zinazokuwakaganya wanafalsafa wa masuala ya maadili juu ya ustaarabu wa Kiislamu zitapata majibuyaliyo wazi na yanayotua akilini.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close