4. Darasa La Wiki

Uislamu umedhamini uhuru wa kujielezea na kuweka vidhibiti vya haki hiyo

Uhuru wa kujielezea katika Uislamu ni haki inayothibitishwa kwa kila mmoja. Haki hii inamuwezesha mtu yoyote kuchagua maoni anayoyapendelea katika masuala yake binafsi au ya umma. Pia, kupitia haki hii, kila mtu anaweza kutoa maoni yake mbele ya wengine.

Hata hivyo, wakati uhuru wa kujielezea unahusika na mtu kueleza mawazo na hisia zake kama anavyotaka, katika kufurahia uhuru huo haifai kusumbua wengine au kuwazuia wengine kutumia haki yao hiyo ya kujielezea.

Sheria ya Kiislamu siyo tu imepitisha haki ya kujielezea kwa kila Muislamu, bali pia imefanya huo kuwa ni wajibu kwa Muislamu kwani Mwenyezi Mungu amewawajibishia Waislamu kutoa nasiha, kuamrisha mema na kukataza maovu.

Ikiwa hivyo ndivyo, ni wazi kuwa wajibu huo hautekelezeki bila kutumia haki hii ya ya kutoa maoni na ushauri kuhusu jambo fulani au suala maalum. Kwa hiyo, sheria ya Kiislamu imempa Muumini haki hiyo ili kumuwezesha kutekeleza wajibu hizo, yaani kutoa nasaha na kuamrisha mema na kukataza maovu.

Uislamu umesisitiza sana uhuru wa kujielezea kupitia matini wazi katika Qur’an Tukufu na hadith za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Katika ambapo Qur’an imeeleza kuwa Uislamu inakubali maoni mbalimbli na kwamba kutofautiana kimaoni ni jambo la kawaida, Mwenyezi Mungu Amesema:

“Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watuwote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana” [Qur’an, 11:118].

Inafahamika kuwa kukhitalifiana baina ya watu ni jambo zuri linalochangia kuibua fikra tofauti zinazostawisha ulimwengu na kuiendeleza jamii. Lakini wakati mwingine kukhitalifiana katika maoni kunapelekea kupingana na migongano. Ili kuondoa kuvutana huko, Qur’an Tukufu imewataka Waislamu warejee hukumu ya Qur’an na Sunna kuhusu suala husika.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlio amini! Mt’iini Mwenyezi Mungu, na mt’iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema” [Qur’an, 4: 59].

Kuwepo maoni mbalimbali yanayoeleza mielekeo ya kifikra iliyopo katika jamii ya Kiislamu ni jambo lililothibiti. Qur’an Tukufu imebainisha kuwa katika jamii ya Kiislamu, wanamme na wanawake, wote wana haki ya kujielezea maoni na misimamo yao.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu.” [Qur’an, 9:71].

Inajulikana kwamba kuamrisha mema na kukataza maovu katika jamii hakukuhusishwa na masuala ya kidini, itikadi na ibada pekee bali imefungamanishwa pia na fikra zote zinazomhusu maisha ya mwanadamu kwa ujumla. Hakika, kuamrisha mema na kukataza maovu ndiyo nguzo muhimu na msingi mkubwa wa uhuru wa kujielezea katika Uislamu.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na Maswahaba wake katika enzi za ukalifa walikuwa wanasikiliza maoni ya wengine.

Kwa mfano, Swahaba Habab bin Mundhir (Allah amridhie) alitoa maoni yake kuhusu mahali pafaapo kwa majeshi ya Waislamu katika vita vya Badr kinyume na alivyoona Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na hatimaye Mtume alikubali rai yake alipoiona kuwa ni bora.

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliomba ushauri kutoka kwa Maswahaba kuhusu tukio la Al-Ifk lililohusisha Bi. Aisha alizushiwa shutuma za uongo za kufanya zinaa.

Miongoni mwa Maswahaba walimnasihi Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ampe Bi. Aisha talaka, lakini hatimaye Mwenyezi Mungu alitangaza usafi Bi. Aisha na heshima yake kupitia Qur’an Takatifu.

Na ipo mifano mingi mingine ambapo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliomba ushauri kutoka kwa Maswahaba wake. Baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kufariki Maswahaba waliendelea kufanya hivyo hivyo.

Vidhibiti vya haki za ya kujieeleza

Muislamu anapaswa kuzingatia vidhibiti na adabu maalumu wakati wa kutumia haki yake ya kujielezea.

Adabu na masharti haya ni pamoja na ukweli na uaminifu. Hii ina maana mtu atoe maoni yanayoambatana na aliyoyaona na kuyajua kiukweli hata ikiwa dhidi ya matamanio yake. Ikumbukwe kuwa, lengo kuu la uhuru wa kujielezea ni kubainisha ukweli na yaliyo sahihi, siyo kuficha ukweli na kusema uongo.

Pia, katika kujielezea, Muislamu anatakiwa akusudie kheri na siyo kutafuta majivuno, kujionesha, kiburi au tu kumpinga yule mwenye haki na mkweli. Wala asilenge mtu kuchanganya ukweli na batili, kupoteza haki za watu au kuonesha tu mabaya ya watu na kudharau mema yao. Katika kujieleza huko, pia mtu asilenge kuchafua sira ya mtu, hususan watawala; na wala asilenge kuwachocheza watu wapindue serikali ili kujipatia faida fulani.

Ni kwa kuzingatia masharti hayo ndiyo uhuru wa kujielezea katika Uislamu huleta faida na kuwa njia muhimu ya kuleta maendeleo ya jamii. Yakikiukwa masharti haya mtu anaweza kujikuta akitenda madhambi anayoyachukia Mwenyezi Mungu au kumuudhi mtu au jamii. Kuvunjwa kwa masharti haya pia kunaweza kupelekea kutokea ghasia katika jamii.

Uislamu umejengwa juu ya misingi ya Qur’an, Sunna na Ijmaa (makubaliano ya wanazuoni). Hivi ni vyanzo muhimu ambavyo haifai kuvivunja wala kuvipuuza kwani matendo yote ya Waislamu hupimwa kwavyo. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema:

“Enyi mlio amini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake” [Qur’an, 49:1].

Jambo muhimu la kuzingatia hapa ni kuwa kila jambo, liwe ibada au muamala, lina dalili yake kisheria na hakika Muislamu hana budi ila kuwajibika kwa mujibu wa hukumu inayotokana na dalili hiyo. Mwenyezi Mungu anasema:

“Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na hiyari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri katika jambo lao.” [Qur’an, 33: 36].

Ama kuhusu yale ambayo sheria haijataja dalili za wazi kuhusu hukumu yake, Muislamu huweza kufuata jitihada yake na kutoa hukumu aonavyo, lakini kwa kuzingatia vidhibiti na masharti maalum yatakayomuongoza kutopingana na misingi na kanuni kuu za jitihada katika kutoa rai.

Jambo la kusikitisha ni kwamba wapo baadhi ya walioelewa vibaya suala la uhuru wa kujielezea wakadhani wanaruhusiwa kutoa maoni yao bila ya kujali kaida, taratibu na masharti. Wapo pia waliokosea kudhani kuwa uhuru wa kujieleza unawapa wao fursa ya kutoa fatwa ya jambo ilhali hawana elimu.

Kutokana na kutoa fatwa bila elimu, watu hao wasiojali miiko ya kutumia uhuru wa kujieleza, wakahalalisha umwagaji damu, uharibifu wa mali na kushushia watu heshima bila haki – mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaharamisha na kuwaamrisha wanadamu wazihifadhi haki hizo.

Pia, kwa kutumia na kutegemea maoni yao mabaya, watu wanawatishia wasio na hatia na kuwasababishia kukosa makazi na kutoa uhai wao, jambo linalochafua hisia za kibinadamu kwa vurugu, ufisadi na ukatili wao.

Watu hao wakaendelea kufanya ufisadi kwa kueneza uharibifu katika sehemu mbalimbali duniani huku wakidai kwamba wao wapo sawa ila wengine ndiyo waharibifu wanaostahili kuadhibiwa!

Mwenyezi Mungu Akliyetukuka anaeleza hali ya watu wa aina hiyo kwa kusema: “Sema, ‘Je, tukutajieni wenye hasara mno katika vitendo vyao? Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri” [Qur’an, 18: 103-104].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close