4. Darasa La Wiki

Uislamu Kukomesha Kero za Vikao vya Njiani

Kila uchao duniainasonga mbele kwa kasi kubwa. Kila siku kuna maendeleo mapya ya uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia, na uvumbuzi zaidi utaendelea kutokea.

Hata hivyo, si kila mapya anayoyavumbua mwanadamu humnufaisha. Katika hayo yaitwayo ‘maendeleo’, baadhi, yanayomdhuru mwanadamu kiimani, kiuchumi, kijamii au kiutu.

Katika hili, Waislamu tuna bahati. Kwa kutumia sheria ya dini yetu kamilifu, tunaweza kupembua kati ya maendeleo na ufisadi. Pia, kwa kuitumia sheria hiyo, tunaweza kuufundisha ulimwengu maana halisi ya ustaarabu katika nyanja zote za maisha.

Na hapa ndio inatubainikia siri ya kufanywa Qur’an kuwa ndicho kitabu cha mwisho na Muhammad (rehema za Allah na amani zimfikie) kuwa Mtume wa mwisho.

“Muhammad si baba wa yoyote katika wanaume wenu, lakini yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.” [Qur’an, 33:40].

Ayah ii inamaanisha kuwa mafunzo ya Mtume huyu yalikidhi, yanakidhi na yataendelea kukidhi haja ya wanadamu wa zama zote zinazofuata popote walipo, kiitikadi, kiibada, kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, kielimu na kiuvumbuzi wa kisayansi pia.

Makala yetu wiki hii inachambua juu ya mafunzo ya Uislamu kuhusu suala la maudhi (kero) za barabarani na sheria ya vijiwe/vikao vya njiani

Abu Said al- Khudri (Allah amridhie) amenukuu kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Tahadharini na kukaa kwenye njia.” Wakasema: “Ewe Mtume wa Allah, sisi hatuna budi (kwani) njiani ni katika vijiwe vyetu ambako wenyewe tunazungumza humo.” Mtume akasema: “Kama lazima mkae, basi ipeni njia haki zake.”

Maelezo

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), kwanza, aliwakanya Maswahaba zake dhidi ya kukaa kwenye njia wapitazo watu mara kwa mara kwa sababu ya maovu yanayojiri ambayo ni vigumu kujiepusha nayo. Maovu hayo ni pamoja na kuwaudhi watu kwa kuwakodolea macho kusiko na haja.

Kawaida, watu huwa hawapendi kuwaona wengine wamekaa mahali wakifanya kazi ya kumtizama kila aendae na arudiye huku wakiwasema chini chini. Tumeona Mtume alipowakataza Maswahaba, wao walilalamika kwa kusema hizo ndio sehemu zao za kukaa na kuzungumza na hivyo itawawia vigumu wakikatazwa kukaa maeneo hayo.

Madai yao yalikuwa ya msingi. Kimaumbile, mwanadamu ni mtu wa jamii na hivyo hupenda na hufarijika anapojumuika na wenzake. Kwa kulitambua hilo, Mtume akawaambia:

“Kama lazima mukae katika njia, muipe haki zake.”

Inaonesha Maswahaba walimuelewa Mtume kuwa hana maana haswa ya kuwakataza kukaa vikao vyao njiani ila wanapaswa tu kuchunga nidhamu ya kukaa maeneo hayo. Katika maelezo ya wanazuoni, wengi wamelitafsiri katazo hili la Mtume kuwa ‘karaha’. Maana yake ni kuwa iwapo wanaokaa katika barabara watatimiza masharti, inafaa na si haramu.

Mwendelezo wa hadith

Hadith haikuishia hapo. Maswahaba walimuuliza:

“Ni zipi hizo haki za njia?” Akasema: “Kuinamisha macho, kuzuia maudhi, kurudisha salamu na kuamrisha mema na kukataza mabaya.” [Bukhari na Muslim].

Sasa hebu tuangalia maelezo ya haki hizi za njia moja baada ya nyingine – tukianza na suala la kuinamisha macho.

Kuinamisha macho

Kuinamisha macho maana yake ni kuacha kutazama vya haramu kama vile kuwakodolea macho wanawake, kuwatazama wapitao kwa jicho la husda au kuzipekuwa aibu za wapitao na vitu walivyochukua. Ijulikane kuwa kutazama ni mshale miongoni mwa mishale ya Iblis.

Allah Aliyetukuka anasema: “Waambie Waislamu wanaume wainamishe macho yao (wasitazame vilivyokatazwa) na wahifadhi tupu zao. Hili ni takaso kwao. Bila shaka, Mwenyezi Mungu anazo habari za (yote) wanayoyatenda. Na waambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao…” [Qur’an, 24:30-31].

Kuzuia maudhi

Hii inamaanisha maudhi yote yanayojiri barabarani ikiwemo kero ya kuwatazama, kuwasengenya, kuwatukana, kuwakebehi, kuwazomea, kuwapiga watu. Pia, inahusisha kuzuia maudhi ya kuwatisha watoto na kuwadhalilisha walemavu.

Kwa kweli, kwa sasa, kero za barabarani zimeongezeka na sasa zipo aina nyingi kuliko wakati ule wa Mtume. Hii ni kwa sababu hivi leo watu wanazidi kuvumbua namna nyingi za kuwaudhi wapita njia na kuzifanya barabara zisipitike.

Miongoni mwa shida wanazokumbana nazo wapita njia ni kuona aibu na kushikwa na hofu. Hali hii inafanya wapita njia hata kuchukia kuwaona tu watu wenye tabia hizo mbaya.

Miongoni mwa aina za maudhi ya njiani ni ule mtindo unaofanywa na baadhi ya vijana kiufunga noti uzi mwembamba kisha anajificha pembeni. Mtu akipita na kutaka kuiokota, anavuta uzi huku wakimcheka na kumzomea!

Kero nyingine za barabarani zama hizi ni madereva kuwakwaza wasafiri au wapita njia kwa kushindwa kufuata sheria za barabarani, kupaki magari sehemu isiyokubalika na kusabababisha msongamano bali hata ajali. Kero nyingine ni kusimamisha gari ghafla bila ya kutoa ishara. Kero/ adha hizi za njiani zimekomeshwa na Uislamu takriban karne 14 zilizopita.

Kupiga honi, kupiga vuvuzela, kuanzisha zogo, dereva kufungua muziki kwa sauti kubwa katika gari lake ni miongoni mwa maudhi mengine ambayo Mtume (rehema za Allah na amani zmshukie) tokea zamani.

Kuna wachezao barabarani kwa kuonesha kiwango cha uwezo wao umahiri wa hili au lile, kuna waendao mwendo kasi kiasi hadi wanasabisha ajali – hawa wote pia wanaingia katika katazo la katazo la Mtume.

Ikumbukwe kwamba, barabara kwa wakati mmoja – hutumiwa na watu mbalimbali wenye shida na hali zinazotofautiana. Kuzidi kwa kero barabarani ni matokeo ya kupuuzwa kwa ukweli huu.

Maana nyingine ya kuzuia kero

Sharti jingine la kuruhusiwa kukaa vikao vya barabarani ni kuondoa kila kitu kinachowakera wapita njia. Miongoni mwa kero zinazotakiwa kuondolewa njiani ni pamoja na maganda ya ndizi, utelezi na hata kamba inayoweza kumzonga mpita njia miguu na kumuangusha.

Kero nyingine za kuondoa njiani ni pamoja na tawi au gogo la mti, jiwe au kitu kitowacho harufu mbaya kama vile kinyesi au mzoga. Ni jukumu la wakaao vibarazani kuondoa kero hizi zote.

Kabla ya kuachana na sharti hili, tunatakiwa tuzingatie kwa umakini kauli ya Allah:

“Kwa yakini wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani katika duniana Akhera na amewaandalia adhabu ifedhedheshayo. Na wale wanaowaudhi Waislamu wanaume na Waislamu wanawake pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhuluma na dhambi zilizo dhahiri.” [Qur’an, 33:57-58].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close