4. Darasa La Wiki

Uhai ni Amana Utumie Kuandaa Akhera Yako

Uhai ni amana na neema waliyotunukiwa waja na Mola wao.Kwa ajili hiyo, kila mwanadamu anapaswa kulinda na kuchunga amana hii kwa kuitumia katika kutenda amali zinazompendeza na kumridhisha Mwenyezi Mungu. Kulifafanua hilo Allah Mtukufu anasema: “Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyeumba umauti na uhai ili awatahini nyinyi (wanadamu), ni yupi miongoni mwenu aliye mwema wa matendo” (Qur’an, 67:2). Licha ya upambanuzi huo, bado hali inaonekana kuwa mbaya kwa baadhi yetu ambao kwa makusudi tumekuwa tukiufisidi uhai wetu kwa kujitia upofu wa kutoziona amri za Allah na kuzitekeleza. Matamanio ya kidunia katika kupenda starehe na mambo ya anasa ndiyo sababu inayowafanya wengi waghafilike na kuikumbuka akhera. Ni kwa sababu hii watu hulazimika kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuchuma mazuri ya duniani. Hii ni ishara ya kuwepo kundi kubwa la watu walioigeuza dunia kuwa sehemu ya kwanza na ya mwisho ya maisha, wakiamini hakuna kitakachofuata baada ya kufa kwao. Lakini Allah anasema: “Ama yule atakayekiuka amri ya Mwenyezi Mungu. Na akapendelea maisha ya dunia kuliko ya akhera. Hapana shaka mafikio yake ni motoni” (Qur’an, 79: 37-39) Kwingineko, Waswahili husema: “Ponda mali kufa kwaja”. Mantiki ya msemo huu imekuwa ndiyo hoja ya watu wanaoamini kifo ni adui wa starehe hivyo kujipa fursa ya kustarehe kabla mauti hayajawafika. Hawa ni wale ambao huzidhulumu nafsi zao kwa kujitenga mbali na suala la kumkumbuka Mwenyezi Mungu, ili hatimaye wasilazimike kuitumia neema ya uhai katika kumtumikia. Kwa nini tusiipende sana dunia Kuishughulikia dunia na kuisahau akhera ni sawa na kuijenga nyumba moja na kuharibu nyingine. Kwa msingi huo, haifai Muislamu kuipenda zaidi dunia na kuipuuza akhera kwa kuwa hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Hii ina maana, mja hawezi kuitumikia akhera ipasavyo na wakati huohuo akaitumikia dunia. Ama mwenye kuvitumikia vyote viwili, dunia na akhera, kwa nguvu sawa basi kuna uwezakano mkubwa wa kukichukia kimoja na kukipenda kingine. Ikiwa unamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho basi jilazimishe kuifanyia kazi akhera yako. Lia juu ya wasiwasi wa nafsi yako, na uwe ni mwenye hofu ya kuiogopa Siku ya Hesabu (Kiyama). Ewe Muislamu, kumbuka uhai ni amana, hivyo unapaswa kuutumia kwa uadilifu na utii wa kufuata maamrisho ya Muumba wako. Pia, ni wajibu kujiweka mbali na anasa za ulimwengu na vitu visivyokuwa na faida. Na katika sifa za waumini wa kweli ni kujiepusha na mambo machafu, maovu na yenye kutia shaka (Shubuhaat). Kwa kufanya hivyo, utaisalimisha nafsi yako na hatari ya kufanya dhambi. Kuitumikia akhera ndiyo njia ya kutoshelezewa haja zako na Allah, na ili ufanikiwe tumia fursa ya uhai wako kufanya yafuatayo: Mosi, usitumie uhai wako kushiriki kwenye mijadala na malumbano yasiyo na tija kwani kufanya hivyo ni kujiandalia mazingira ya uasi na kujenga uadui na watu. Kuwa na subira wakati wote na kila mahali kwa kuwa uvumilivu ndiyo utakaokuongoza kwenye uadilifu. Pili, usijenge ukaribu na watu ambao mara zote huzungumzia mambo ya kidunia kwani kufanya hivyo kutaharibu ustawi na umakinifu wa dini yako na kuchafua moyo wako. Badala yake shikamana na kundi la wachamungu na watu wema na Allah atakufanyia wepesi katika maisha yako. Tatu, usiutumie uhai wako katika maasi na mambo machafu kwani kufanya hivyo ni kuifanyia hiyana amana ya Mwenyezi Mungu. Badala yake, jikurubishe kwa Allah kupitia matendo ya utoaji Zaka, sadaka, kusaidia masikini na mayatima nk. Juu ya hilo Allah anasema: “Ama mwenye kutoa kwenye mali yake, na akamcha Mwenyezi Mungu (kwenye huko kutoa).Tutamuongoza na kumuwafikisha kwenye njia za kheri na wema na kumrahisishia mambo yake,” (Qur’an, 92:5-7). Nne, Kumbuka kifo mara nyingi na Allah atakufanya uwe mwepesi wa kuitamani akhera. Ewe Muislamu, kumbuka uhai ni amana ya Mwenyezi Mungu katika ardhi yake, na sisi kama wanadamu ni watunzaji wa amana hiyo. Hivyo, mwenye kuutendea wema uhai wake atakuwa ametekeleza haki ya amana. Kadhalika, mwenye kuutumia vibaya atakuwa amefanya hiyana hivyo kustahiki adhabu. Kutokana na hilo, yatakiwa kuutendea haki uhai wetu kwa kujiepusha na kila chenye kupelekea kupata hasara miongoni mwa matendo na kauli. Na juu ya umuhimu wa amana ukiwemo uhai, Mwenyezi Mungu anatukumbusha: “Kisha mtaulizwa (Siku ya Kiyama) juu ya neema mlizopewa.” T u – m u o m b e Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wasikivu wa kauli na kuzifanyia kazi. H ivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wake Mkuu, Kassim Majaliwa ilitoa tangazo la kupiga marufuku pombe zijulikanazo kama ‘viroba’. Serikali imesema kuwa kuanzia Machi mosi mwaka huu, ni marufuku pombe hiyo kutumika na kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika. Serikali imechukua uamuzi huo kwa sababu ya madhara makubwa yanayoletwa na pombe. Kwa aina hii ya pombe, madhara yamekuwa makubwa zaidi kwani zimekuwa ni rahisi hata kwa watoto kutumia na pakiti zake ni huzagaa kila mahali na kuharibu mazingira. Na jambo baya zaidi ni kwamba pombe hizo zinanywewa hadharani kama vinywaji vingine halali kiasi kwamba ni rahisi kwa watu wengi kuzitumia. Sisi tunasema ni hatua nzuri na ya kupongezwa sana. Tunasema ni hatua ya kupongezwa kwa kuwa pombe kwa ujumla wake zina madhara makubwa na ndiyo maana dini tukufu ya Uislamu imekataza pombe. Kiafya, siyo siri pombe hizi zimewaathiri mno vijana wetu na hata kupelekea kupunguza nguvu kazi ya taifa. Athari za kiafya Mathalani katika upande wa afya, vijana wengi wamejikuta wanapata athari na madhara makubwa yasababishwayo na kemikali za sumu kwenye koo, utumbo na mfumo mzima wa kumeng’enya chakula na hatimaye kuumuka vitambi, mwili kupoteza uwezo wake wa kawaida wa kuchom a m a f u t a , k u s a b a b i s h a mrundikano wa mafuta tumboni, kunenepeana kupita kiasi, uwezekano wa kupata shinikizo la damu, kukabiliwa na maradhi ya hatari ikiwemo saratani. Tumbo la mlevi wa kupindukia hukabiliwa na maradhi ya vidonda vya tumbo, kulisababishia ini matatizo ikiwemo kusinyaa, kuharibu figo na uwezo wake wa kuchuja na kusafisha sumu kwenye damu, kuharibu neva, na kuchelewesha damu kufika kwenye mishipa ya ubongo kwa haraka, kudhoofika akili, kutojali, kushindwa kujidhibiti, kutetemeka hovyo, kuweweseka, kushindwa kutembea sawa sawa. Vilevile, athari nyingine za pombe ni kukosa uamuzi wa haraka, husababisha pia madhara kwenye tezi la kibofu cha mkojo kwa wanaume, uvimbe tumboni, kuvimbiwa, kichefuchefu, kukosa choo, kupoteza uwezo wa kuona vizuri, husababisha pia utasa kwa wanaume na wanawake, kupoteza uwezo wa kujamiiana kwa wanaume na wanawake, maumivu sugu ya kichwa, kupoteza kumbukumbu na nyingine nyingi. Athari za kijamii Lakini pia pombe hizo zimeongeza vitendo vya ukabaji, na wizi miongoni mwa vijana wengi huko mitaani kwani ule uwezo wao wa kufanya kazi hutoweka na hivyo kuwafanya waishi kwa vitendo hivyo. Hakika ndiyo maana imetajwa kuwa pombe ni mama wa maasi. Pia upatikanaji kirahisi wa pombe hizi umekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani hususani kwa madereva wa bodaboda na hata wa basi ya masafa marefu. Ukizungumzia vijana hawa wa bodaboda, wengi wao wamekuwa wakitumia mno pombe hizi kiasi kwamba wawapo njiani hupoteza uwezo fulani wa kiakili na kujiona wako peke yao barabarani. Matokeo yake ni kutokea kwa ajali zinazoambatana na vifo pamoja na ulemavu kwa watu wengi ikiwemo kupoteza nguvu kazi ya taifa letu. Ukiachia hayo, pombe hizi pia kama tulivyosema hapo awali kuwa zimekuwa zikitapakaa hovyo mitaani, zimekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya utoro kwa wanafunzi wengi huko shuleni na kuwafanya washindwe katika mitihani yao. Na siyo tu ufeli tu bali pia pombe hizo zimewafanya baadhi ya wanafunzi kuwa na utovu wa nidhamu na hata kuwa tishio kwa walimu wao. Ila kwa upande wetu, tunazidi kuiomba Serikali isiishie kupiga marufuku tu pombe hizo za viroba bali ipige marufuku aina zote za pombe bila kusahau kamari ambayo nayo imeshamiri sana siku hizi. Qur’an imekataza pombe Na hili la ubaya wa pombe limeshazungumzwa na Mwenyezi Mungu katika Qur’an (5: 90) kuwa: “Enyi mlioamini, hakika ya ulevi, na kamari na kuabudu masanamu, na kupiga ramli ni uchafu katika kazi ya shetani, basi jiepusheni navyo…” Wakati tukielekea kuhitimisha, tunatoa wito pia kwa jamii nzima kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha pombe hizo hazionekani tena mitaani au sehemu nyingine za wazi. Itashangaza sana kuona baadhi ya watu wakiendelea kuziuza pombe hizo licha ya athari kubwa zinazoonekana kwa vijana wetu. Hivyo basi, jamii nayo isikae pembeni na kuliona suala hilo ni la serikali tu kwani wanaoathirika na pombe hizo ni vijana wetu. Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunafanya kazi ya kuwakomboa vijana hawa kabla ulevi haujawasukuma kutumia dawa za kulevya. Hongera Serikali, tusiishie kwenye pombe za viroba tu Uhai ni amana utumie kuandaa akhera yako hutolewa na kuchapishwa,The Islamic Foundation, P.O. Box 6011 Morogoro, Tanzania, E-mail: imaanmedia3@gmail.com, Chumba cha habari: 0652 777 969 afisa masoko: 0785 500 502, TOVUTI: www.islamicftz.org Kwa maoni wasiliana na mwandishi kwa namba 0

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close