4. Darasa La Wiki

Tupupie kufanya heri miezi mitakatifu, tujiepushe na shari

Alhamdulillahi, tuko ndani ya mwezi wa Dhul–Qa’ ada, ambao kwa mujibu wa Kalenda ya Kiislamu (Al–Hijri) ni miongoni mwa miezi minne mitakatifu aliyotujulisha Allah ‘Azza Wajallah’ ndani ya Qur’ an: “Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni miezi kumi na miwili tangu siku aliyoumba mbingu na ardhi; katika hiyo minne ni mitakatifu, hiyo ndiyo dini ya sawa kwa hiyo msizidhulumu nafsi zenu ndani yake (miezi hiyo)”. [Qur’ an, 9:36].

Miezi Mitakatifu iliyokusudiwa ndani ya Aya hii ni Dhul–Qa’ada (Mfunguo pili), Dhul–Hijja (Mfunguo tatu), Muharram (Mfunguo nne) na mwezi wa Rajab, kama alivyosimulia Swahaba Mtukufu, Abu Bakr (Allah amridhie) katika Hadithi ifautayo: “Zama zimekamilisha mzunguko wake na imekuwa kama ilivyokuwa siku Allah alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na miwili na katika hiyo minne ni mitakatifu, mitatu imefuatana Dhul Qa’ada, Dhul– Hijja, Muharram na Rajab Mudharr ulio kati ya Jumaada (Aakhir) na Shaaban.” [Bukhari na Muslim].

Katika kuifafanua miezi hii minne, Wanazuoni wa fani ya historia (Tareikh) wamesema kuwa, Mwenyezi Mungu ameiteua miezi minne hiyo kuwa mitakatifu na kukataza watu kupigana vita ndani yake kwa sababu maalumu, nayo ni kuwawezesha Waislamu kwenda Makka kufanya ibada ya Hijja na Umra na kurejea nyumbani kwa amani.

Allah ameuteua mwezi wa Dhul–Qa’ada ili Waislamu waweze kusafiri kutoka kwao na kuelekea Makka bila ya skudhuriwa, na pia ameuchagua mwezi wa Dhul–Hijja kwa ajili ya kufanya ibada ya Hijja kwa amani. Kisha akautukuza mwezi wa Muharram ili Waislamu waweze kurejea nyumbani hali ya kuwa wamekamilisha ibada ya Hijja kwa amani. Ama mwezi wa Rajab, Mwenyezi Mungu ameutukuza kwa ajili ya kuwawezesha Waislamu kwenda Makka kuizuru nyumba yake (Ka’aba), na kwa ajili ya kufanya Umra. Pamoja na faida lukuki zinazopatikana ndani ya miezi hii, tulio wengi tumekuwa hatuipi umuhimu kama ilivyo kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na ndiyo maana tumekuwa tunatumia muda mwingi kushughulikia mambo yasiyo na faida.

Kwa hali hii, si ajabu wapo miongoni mwetu Waislamu ambao hawafahamu umuhimu na fadhila za miezi tuliyonayo. Hivyo basi, ipo haja kwa viongozi wa dini hususan Maimamu wa misikiti kuelezea faida zinazopatikana katika miezi hii sanjari na kuwahimiza Waumini wao kufanya mambo ya kheri. Zipo amali nyingi njema ambazo Muislamu anaweza kuzifanya, lakini jambo la msingi ni mtu kujilazimishakufanya heri kadiri awezavyo.

Allah Ta’ala anatuambia: “Basi Mcheni Mwenyezi Mungu kadiri muwezavyo (mwisho wa jitihada yenu), na sikieni, na tiini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndiyo waliofanikiwa.” [Qur’an, 64:16].

Kwa mnasaba wa Aya hii, ni vema kila Muislamu ajibidiishe na utekelezaji wa mambo mbalimbali ya heri kama vile kusoma Qur’an, kuzidisha ibada za sala na funga za sunna, kumuomba Allah msamaha na kutubia madhambi, kumtaja Allah kwa wingi, kusaidia masikini, kuwatendea wema majirani, marafiki na kupatanisha waliogombana.

Zaidi ya hapo tutambue kuwa, kila neema aliyoruzukiwa mja na Allah Ta’ala, itaulizwa Siku ya Kiyama. Hivyo basi, ndugu yangu katika imani, zinduka na anza sasa kuitumia vema fursa ya afya na uzima katika kumtumikia Allah kadiri itakavyowezekana kwani kufanya amali njema katika miezi hii kuna ujira mkubwa.

Ama Muislamu kumuasi Allah Ta’ala haijuzu katika miezi yote 12, isipokuwa katika miezi minne mitakatifu dhambi zake huwa ni kubwa zaidi. Juu ya kauli ya Allah: “Basi msidhulumu nafsi zenu humo (katika miezi mitukufu).’’ Imam Qatada amesema: “Dhulma itakayotendeka katika miezi mitakatifu ni mbaya na kubwa(au hatari) kuliko dhuluma itakayotendeka katika miezi mingine. Hakika dhuluma daima ni makosa, lakini Allah hufanya baadhi ya vitu kuwa ni vizito kuliko vingine kama anavyopenda….” [Tafsiri ya Qur’an–Ibn Kathir]. Yaliyoharamishwa katika Miezi Mitakatifu Miongoni mwa mambo yaliyokatazwa katika miezi mitakatifu ni watu kupigana vita.

Allah Mtukufu anasema: “…kupigana vita wakati huo (wa miezi mitakatifu) ni dhambi kubwa. Lakini kuzuilia watu wasiende katika njia ya Allah na kumkanusha yeye (Allah), na kuzuilia watu wasiende kwenye msikiti Mtukufu (Makka), na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Allah. Nafitina ni mbaya zaidi kuliko kuua….’’ [Qur’an, 2:217].

Kadhalika, imeharamishwa katika miezi mitakatifu watu kumshirikisha Allah kwa aina zote za shirk, kuiba, kuzini, kulewa, kudhulumiana,

kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, kusengenya, kusema uongo, na kadhalika. Hivyo, ni muhimu tuanze kujipinda kufanya ibada mbalimbali za wajibu na Sunna sambamba na kuacha yaliyoharamishwa kwa kuzingatia maonyoya Allah Aliyetukuka: “Enyi mlioamini, msivunje utukufu wa alama za Allah wala miezi mitakatifu…” [Qur’ an, 5:2].

Kwa hiyo, tujihimu kuitukuza miezi hii mitakatifu kwa sababu Allah ameiteua kwa kuipa hadhi maalum na katuusia kutokuzidhulumu nafsi zetu kwa kutenda maasi ndani yake.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close