4. Darasa La Wiki

Tumsaidie Rais kupambana na wabadhirifu

Ubadhirifu wa mali za umma ni tatizo la kimaadili linaloendelea kushika kasi hapa nchini na hivyo kurudisha nyuma jitihada za serikali za kuwaletea maendeleo wananchi.

Ubinafsi, tamaa ya mali na kutaka utajiri wa haraka haraka ni baadhi tu ya sababu zinazowafanya baadhi ya watendaji wa serikali kujihusisha na vitendo viovu vya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Ingawa hulka ya wengi ni kupata utajiri ili waishi maisha mazuri, lakini hulka hiyo imejikita zaidi katika mfumo wa ubepari, ambao hauangalii maslahi ya jamii kwa upana wake, bali maslahi ya mtu mmoja mmoja.

Leo hii, kila mtu anajaribu kutafuta mbinu ya kujitajirisha hata kama ni kwa gharama ya watu wengine. Mtu anathubutu kuiba mali za umma au shirika au kampuni anayofanyia kazi ili apate utajiri wa maramoja.

Ukichunguza kwa makini utakuta watumishi wa namna hiyo ni wale wavivu na wenye matarajio ya kupata fedha nyingi kando na mishahara wanayopokea.

Kubainika kwa ubadhirifu wa mabilioni ya fedha katika miradi ya ujenzi wa barabara za Kijichi Mwanamtoti na Kijichi Toangoma wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ni kielelezo cha kushamiri kwa vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma hapa nchini.

Miradi hiyo miwili imetajwa kuwa chini ya kiwango kulinganisha na thamani halisi ya fedha zilizotumika. Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kukagua miradi hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema haridhishwi na gharama zilizotumika katika mradi hiyo.

“Manispaa ya Temeke wameamua kutujengea mradi huu kwa kuongeza gharama kubwa za ujenzi. Tumeona namna mlivyoharibu fedha za nchi. Hatuwezi kujenga kilomita 1.8 ya lami kwa gharama ya shilingi bilioni 5.4 na hatuwezi kuwa na watumishi wa umma wa namna hii,” alisema Majaliwa akionesha kughadhibishwa na jambo hilo.

Kutokana na ubadhirifu huo, Waziri Mkuu Majaliwa aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Temeke kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watendaji wote waliohusika na ubadhirifu huo.

“Watu wote waliohusika warudishwe na wafikishwe mahakamani, hatuwezi kufanya mchezo, hizi ni fedha za walipa kodi,” alisema Majaliwa.

Huo ni mfano mmoja kati ya mingi unaoonesha ukubwa wa tatizo la ubadhirifu wa fedha za umma hapa nchini. Mara kwa mara taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imekuwa ikiibua madudu kuhusu matumizi ya fedha za umma katika sekta za afya, halmashauri na ujenzi wa miundombinu.

Baadhi ya watendaji wasio waaminifu wamekuwa wakitumia madaraka waliyopewa kufanya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo bila hofu wala woga. Tujiulize, watu hawa wanamkomoa nani kama siyo kujichelewesha wao wenyewe na familia zao kuyafikia maendeleo wanayoyatarajia?

Katika hotuba yake ya kulizindua Bunge la 12 mwezi April mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alitaja vipaumbele vya serikali anayoiongoza, kimojawapo kikiwa ni kupambana na rushwa, uhujumu uchumi, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Kwa maoni yangu, naona inawezekana kukomesha ubadhirifu, lakini hilo litatokana na nidhamu na uadilifu wa watumishi na viongozi wote wa serikali. Mambo haya mawili (nidhamu na uadilifu) yamesisitizwa sana katika vitabu vya Mwenyezi Mungu, yaani Qur’an, Taurat, Zaburi na Injili.

Mathalan, katika Sura ya Al– Israi (Qur’an, 17:26–27) Mwenyezi Mungu anasema: “…wala usitumie ovyo kwa fujo. Hakika wabadhirifu ni ndugu wa mashetani (wanamfuata Shetani). Na shetani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.”

Ubadhirifu ni dhambi kubwa inayoweza kumgharimu mtu Siku ya Kiyama. Mwenyezi Mungu anasema:

“Hakika sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayoyatanguliza na wanayoyaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asili lenye kubainisha.” [Qur’an, 36:12].

Aya hii tukufu inawakumbusha wanadamu kwamba chochote wanachokifanya katika maisha haya ya dunia kinaandikwa na Malaika kwenye kitabu cha kumbukumbu ya matendo ya waja.

Pamoja na ukweli huo ambao kwa bahati nzuri wengi wetu tunauamini, bado wapo watu wengi wanaoiba fedha za umma bila hofu wala woga. Siyo siri, wapo baadhi ya watumishi wanaofanya kazi za serikali kwa kutanguliza mbele manufaa na faida (maslahi) binafsi, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya utawala bora.

Kuwapo kwa tuhuma za upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo limekuwa ni jambo la kawaida hapa nchini, na ndio maana viongozi walioteuliwa na Rais Samia wamekuwa wakitoa matamko mbalimbali ya kuwaonya watumishi wa serikali wanaotanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wao.

Rai yangu kwa watumishi wa umma ni kwamba watekeleze wajibu wao kama walivyoahidi katika kiapo cha Maadili ya Utumishi wa Umma. Nasema hivyo kwa sababu uwajibikaji wa watendaji wa Serikali ni jambo muhimu mno katika utumishi wa umma kwani bila hivyo, miradi mingi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma za jamii itakwama na kusababisha adha kubwa kwa wananchi.

Kwa hakika, ubadhirifu ni jambo lisilokubalika kidini na kijamii, hivyo natoa tanbihi kwa watumishi wa umma kumrudia Mungu kwani nina hakika dini zote zina mafunzo yanayokemea ulaji rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.

Jamii inayokumbatia rushwa, ufisadi na ubadhirifu haiwezi kupiga hatua kimaendeleo. Upo msemo usemao:

“Ukitaka kufika haraka nenda peke yako na ukitaka kufika mbali nenda na wenzako.”

Kwa kuzingatia msemo huo, ni vyema pia viongozi wa dini wakatumia nafasi zao kukemea vitendo vya ubadhirifu. Wakifanya hivyo, lengo zuri la serikali la kukabiliana na wizi wa mali za umma litafanikiwa kwa kiasi kikubwa, na wao watakuwa sehemu ya harakati za kupambana na ubadhirifu

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close