4. Darasa La Wiki

Tofauti Kati ya Zaka na Kodi

“Zaka hutolewa mara moja tu kila mwaka na imewekwa kwa mujibu wa Qur’an Tukufu na haiwezi kubadilishwa na mtu yeyote. Zaka ni mfumo
wa kudumu wakati kodi haiko hivyo. Mfumo wake unaweza
kubadilika kulingana na haja na wakati.”

Msomaji mmoja wa gazeti Imaan ameniuliza kupitia ujumbe mfupi wa simu kama zaka nayo ni kodi? Hakika hili ni swali gumu. Tumekuwa wepesi katika kuifananisha zaka na kodi nyingine zinazotozwa na serikali, ingawa dhana hizo mbili, kimsingi ni tofauti sana.

Naogopa kuifananisha zaka na kodi, ingawa katika makala yangu iliyotangulia, niliiangalia zaka kama moja ya mapato ya serikali ya Kiislamu na hivyo kuonekana kama kodi.

Nilifanya hivyo kwa sababu wakati mwingine tunakosa maneno sahihi ya Kiswahili kuwasilisha dhana za Kiislamu kwa ufanisi zaidi. Lakini, yote kwa yote, zaka ni kodi, kama tunaivyofahamu maana ya kodi katika mifumo ya uchumi isiyo ya Kiislamu.

Hivyo basi, nami nalipeleka swali hili kwa Sheikh Shaaban Mussa katika ukurasa wake wa Fatawa ndani ya gazeti hili adhimu, kwa kuwa siyo sahihi sana kuliangalia jambo hili kwa mtazamo wa kiuchumi peke yake, bila ya kuwa na miwani ya kiitikadi na kisharia. Ubavu wa kuogelea kina cha bahari hiyo miye sina. Hivi Sheikh ni sahihi kuiita zaka kodi?

Katika makala zilizotangulia, niliainisha kodi kama mfumo ambao serikali zinautumia katika kukusanya fedha kwa ajili ya kugharamia matumizi ya serikali hizo na huduma nyingine muhimu za kijamii.

Tuliainisha pia zaka kama kodi ya mali ambayo watu wanawajibika kulipa asilimia 2.5 ya mali yao ambayo imekaa mwaka mzima. Mali za Zaka zinahifadhiwa mahali maalumu kwenye Bait ul-Mal (hazina ya serikali) na haitumiki isipokuwa kwa vipengele nane ambavyo vimetajwa ndani ya Qur’an.

Sasa leo wapendwa wasomaji wangu, nimeona tuangalie tofauti kati ya zaka na kodi, bila ya kusema kama zaka ni kodi au la. Yaani tuangalia tu jinsi dhana hizi mbili zinavyotofautiana, kwa kuwa huwa tunazichanganya bila ya kujua mpaka ulipo.

Zaka na kodi

Kwanza, zaka inahusika zaidi na dini na kodi inahusika na serikali. Kwa msingi huo tu, si rahisi zaka na kodi vikaenda pamoja. Ni tofauti katika maeneo mengi, ingawa kuna mfanano katika baadhi ya maeneo.

Wakati zaka ina utukufu wa kidini, kodi haiko hivyo. Kodi inakusanywa kutoka kwa raia wote katika nchi. Serikali inakusanya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi nzima, wakati zaka inakusanywa kwa Waislamu tu tena wenye uwezo na waliyofikisha vigezo vya kutoa zaka.

Zaka hutolewa mara moja tu kila mwaka na imewekwa kwa mujibu wa Qur’an Tukufu na haiwezi kubadilishwa na mtu yeyote. Zaka ni mfumo wa kudumu wakati kodi haiko hivyo. Mfumo wake unaweza kubadilika kulingana na haja na wakati.

Zaka inakokotolewa kwa asilimia 2.5 ya kipato cha mwaka cha mtu au familia. Kinyume chake, Serikali zina kanuni na taratibu maalumu za kuweka viwango vya kodi. Wakati hakuna mabadiliko ya asilimia iliyowekwa katika Zaka, serikali zina haki ya kubadili kanuni au mfumo wa kutoza kodi kila wakati kulingana na malengo yake.

Pia kuna tofauti katika vyanzo vya Zaka na Kodi. Wakati Zaka ina vyanzo maalumu, vyanzo vya kodi vinabadilika kulingana na mahitaji. Kodi inakuja moja kwa moja (direct) au kwa njia isiyo ya moja kwa moja (indirect). Zaka inatolewa kwenye mali au mapato yaliyofikia kiwango.

Kuna masharti maalumu ya kutoa zaka. Pia zaka inasambazwa kwa watu maalumu tu wakiwemo masikini, wenye madeni, walioajiriwa kukusanya fedha katika njia ya Mwenyezi Mungu na msafiri na pia kwa lengo la kuwaachia huru mateka.

Wakati zaka siyo lazima kwa wasio na uwezo, kodi ni lazima kwa raia wote. Bila ya kujali kama ni tajiri au masikini, wote lazima walipe kodi. Pia tofauti na zaka, serikali zinalazimisha kodi kwa raia. Zaka pia ni njia ya wokovu kwa wale wanaolipa.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close