4. Darasa La Wiki

Tiba ya gonjwa la kutokuwa na qinaa

Kwa tafsiri ya wengi wetu, matajiri ni watu wanaomiliki mali, fedha au vitu vingi. Lakini hakika ni kwamba, tajiri ni yule mwenye kukinai.

 Kama mtu ana bilioni moja lakini analalamika kwa sababu hajapata bilioni 10, huyu bado ana safari ndefu kufikia utajiri. Mwengine anaweza kuwa na milioni 50 lakini akawa na utulivu nafsini mwake kwa sababu anatosheka (qinai) .

Aghalab, mwenye kumiliki mapesa mengi huku akiwa haridhiki wala kushukuru, huishi maisha ya mawazo mengi na kuangukia kwenye magonjwa ya moyo. Ni kwa sababu hii nchi zinazosifika kwa utajiri ndizo zinazoongoza kwa raia wake kujinyonga. Jiulize kwa nini hali iko hivyo?

Utakuta mtu anataka kununua kila gari linalotoka. Au mwanamke anataka kila aina ya urembo mpya ili kushindana na wenzake.

 Ukiwa hivyo, wewe bado ni masikini. Kama unajiona ni tajiri, basi unaishi katika utumwa wa utajiri. Usipende kushindana na kila anayekuzidi kipato ikiwa hujui nini cha maana unachotafuta baada ya kufikia kiwango chake.

 Utakuta mtu kajawa na mawazo kibao kisa anamhusudu rafikiye anayemiliki msururu wa magari hali yeye analo moja tu! Asilolijua ni kwamba, kila mtu kakadiriwa kipato chake. Kulazimisha ambalo hujapangiwa, kutakutia majonzi kila uchao.

Hatukatazwi kutafuta na kujitahidi kusogea kimaendeleo, lakini je unatambua unachokitafuta? Ni kweli tunao utajiri wa nafsi?

 Inaelekea tumesahau ushauri wa Kiigizo Chetu kuwa anayetaka utajiri qinaa kinamtosha. Je umeelekeza macho yako kwa aliyekuzidi tu kipato au unamwangilia pia aliye chini yako? Unaweza kukuta mtu ana uwezo mkubwa sana wa kifedha na mali, lakini ajabu yule ambaye ni masikini zaidi yake anaishi kwa raha kwa sababu hashindani na mtu kwa mambo ya kidunia. Na hii ndio siri kubwa wengi tumeshindwa kuielewa.

 Tulipoamrishwa washindane wenye kushindana ndani ya Qur’an, haikumaanishwa kushindania dunia, bali Akhera. Maswahaba walikuwa wakipendelea wenzao wafanye au wachukue vitu kwenye mambo ya kidunia, ila kwenye Akhera walikuwa wanashindana wanavyoweza kushindana.

 Kumbuka kisa cha Swahaba mkubwa, Sayyidna Umar aliyejaribu kumshinda mwenzake Sayyidna Abubakr (Allah awaridhie) katika nyanja nyingi kuanzia kwenye kuchangia mali zao kwenye dini mpaka katika matendo mengine ya kiibadakwa ajili ya Akhera yao – na hao ndio watu wabora zaidi baada ya Mitume.

 Kumbuka kisa cha Swahaba aliyeenda kuomba kulala kwa Swahaba mwenzake kwa siku kadhaa ili achunguze anayofanya usiku hadi akasifiwa na Mtume kuwa ni mtu wa peponi.

 Halafu uzuri ukikusudia kufanya mambo kwa ajili ya Akhera yako, unajikuta Allah anakusahilishia kwenye dunia yako pia. Ni sawa na kumuomba mtu akuletee maji, utakuta anakuletea na bilauri japo uliomba maji tu.

 Ila sasa ukiikusudia dunia tu bila kuangalia Akhera ambayo ndiyo yenye maisha marefu kwetu, unajikuta unapoteza la umuhimu na kuhangaikia lenye maslahi mafupi na wakati mwengine unaweza usifanikiwe.

 Mara ngapi tunasikia tajiri fulani amejitundika kisa faida yake ya mamilioni ya dola aliyozoea kupokea mwisho wa mwaka imepungua, sikwambii kama angefilisika kabisa. Hayo ndiyo madhara ya ukosefu wa qinaa au utajiri wa nafsi.

 Hatukatazwi kutafuta dunia, lakini lisiwe lengo letu na tukasahau la msingi tuliloletewa hapa duniani. Kila unachofanya hapa duniani, hakikisha unakusudia kuwa ni ibada. Uwe na nia ya kumridhisha Allah Aliyetukuka kwa kuwa ndio lengo alilotuumbia.

 Miliki mali za kutosha lakini hakikisha zinatumika katika kumridhisha Allah. Ukishakuwa na mali nyingi, usifanye israfu wala ubakhili. Kuwa na matumizi ya kati na kati ili usiathiri watu walio chini ya uangalizi wako.

 Usitumie muda wote kwa ajili ya kutafuta tu hadi ikawa huna muda wa kufanya ibada za lazima kwa ajili ya dini yako. Usiwe mtafutaji ukakosa muda wa kuswali jamaa kwa wakati, kujifunza dini yako au kukutana na familia yako kwani hapo utakuwa unaishi utumwani na ushatoka kwenye lengo la kuumbwa kwako. Kwa kumalizia, tujikumbushe hadithi iliyosimuliwa toka kwa Salamah bin ‘Ubaidullah bin Mihsan Al-Ansari (Allah amridhie) kwamba baba yake amesema:

“Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Yeyote anayeamka akiwa vizuri kiafya, akiwa salama na kuhisi ulinzi nafsini mwake, akiwa na chakula cha siku ni kama amemiliki dunia nzima.” [Sunan Ibn Majah, mjeledi wa 5, kitabu Na. 37, hadith 4280].

Maneno kama haya tukiyatambua na kuyafanyia kazi tutaishi kwa raha na tutaishinda dunia. Tumia fungu lako la ziada kuwekeza kwa ajili ya Akhera yako.

Maswahaba walishinda sio kwa kuwa wana elimu kubwa ya sekula, au walimiliki silaha nzito sana bali walifuata dini kwa yakini, wakawekeza katika Akhera zaidi ya dunia. Allah atuongoze tuweze kuyasikia maneno na kuyafanyia kazi mazuri yake

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close