4. Darasa La Wiki

Soko la Ramadhan limefungwa, lakini si mwisho wa biashara

Waislamu tunapoingia katika misimu mbalimbali inakuwa kama tumeingia katika soko la bidhaa nyingi na nzuri, na lililochamka kwa harakati za wateja. Katika soko hili, wafanyabiashara hupata fursa ya kuuza bidhaa zao kwa haraka na kwa bei ya juu

Masoko haya yanatofautiana na tuliyoyazowea ambapo wateja ni wengi. Kwa soko hili, mteja ni mmoja tu: Mwenyezi Mungu

Aidha, baada ya mteja huyu kuzinunua bidhaa huzihifadhi, huziongezea ubora na faida kisha amewaahidi kuwarudishia wenyewe wakati ambapo watakuwa wanazihitaji sana (Siku ya Kiyama).

Mwenyezi Mungu anasema: “Na chochote cha kheri mnachokitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu mtakikuta mbele ya Mwenyezi Mungu kikiwa bora na ujira mkubwa zaidi..” [Qur’an, 73: 20].

Tunapofanya biashara na Allah Ta’ala, tunatakiwa tutahadhari mno dhidi ya kutumia aina yoyote ya ghushi (ubabaishaji). Kwanza, Yeye, Mola wetu, hapendi bidhaa isiyo na kiwango. Pili, anatujua vyema kuliko tunavyojijua wenyewe, na hatuna namna yoyote ya kumdanganya

Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) anasema “Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri, basi hakubali ila kizuri.” [Muslim]. Pia, akasema: “Mwenyezi Mungu anapenda mmoja wenu akifanya amali yoyote aifanye kwa vizuri.” [Abu Ya’laa].

Hivi karibuni kwa siku 30, tulikuwa katika soko la Ramadhan tukifanya biashara. Kwavile soko lilikuwa la muda mfupi tu, ilitarajiwa kila mfanya biashara (Muislamu) amejipange mapema kukusanya bidhaa kwa ajili ya mteja wake, Mola wetu, ambaye ni tajiri mno. Anaweza kununua bidhaa (ibada) za wafanyabiashara (Waislamu) wote duniani wa zama zote bila ya kufilisika.

Alhamdulillah, tumeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara baadhi wakiwa wamechangamkia fursa na wakashindana kuuza bidhaa nyingi usiku na mchana. Wengine walikuwa katika hali ya wastani – wakishughulika na ibada baadhi ya muda na kuzembea muda mwingine.

Lakini – kama kawaida – walikuwepo wazembe waliojisahau katika viwanja vya soko, wakashindwa kuuza bidhaa zao hadi zimedoda. Kundi hilo la mwisho, aghlabu, walikumbushwa na wenzao juu ya kufunguliwa soko hili lakini waliendelea kulala.

Waliofanya biashara ya kweli

Waliofaidika ni wale walioshtushwa na taarifa ya kufungwa kwa soko, wakalitumia vema hadi linafungwa. Bidhaa walizouza Waislamu hawa ni pamoja na sala za jamaa, Qiyam Ramadhan, sadaka, usomaji Bidhaa nyingine ni pamoja na dhikri na dua, kufuturisha, kufariji wasiojiweza, kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Kama tulivyoeleza, soko hili huwa wazi kwa msimu mdogo kila mwaka. Amepata faida aliyepata na amekula hasara aliyezembea.

Hata hivyo, ingawa soko la Ramadhan limefungwa, usiwe mwisho wa kutangaza na kuuza bidhaa zetu ambazo tuna uwezo wa kuzipata. Fursa za kuuza bado zipo, Allah, Tajiri kuliko matajiri wote tayari kununua bidhaa hizo kwa bei nzuri

Ukarimu tuliouonesha wa kulishana chakula usiishie hapa. Malori yaliyojaza vyakula yakiwafuata wanyonge mpaka vijijini na kuwasambazia misaada hiyo, yaendelee kwani wahitaji wapo mwaka mzima na sio Ramadhan tu. Misikiti iendelee kun’gaa na kupendeza kwa Waumini kusali jamaa

Ramadhan imeondoka lakini Bwana wa Ramadhan yupo haondoki. Anataka tumuabudu ibada endelevu. Mwenyzi Mungu hapendi na hazitaki ibada za kimsimu (za ubabaishaji) hazitaki. Yeye anatujua zaidi kuliko tunavyojijua sisi, na anaangalia tunachofanya.

Tuendelee kufanya biashara na Allah

Allah mtukufu anasema: “Hakika wale wanaosoma kitabu cha Mwenyezi Mungu na wakasimamisha sala na katika yale tuliyowapa wakatoa kwa siri na kwa dhahiri; hao wanatamani biashara isiyododa. Ili awape ujira wao kamili na kuwazidishia fadhila zake, hakika Yeye ni Mwingi wa msamaha na Mwingi wa shukran.” [Qur’an, 35: 29-30].

Biashara ya siku sita

Baada ya kuagana na Ramadhan, Waislamu tunatakiwa kufanya biashara na Allah kwa muda wa siku sita katika Shawwal (Mfunguo Mosi). Bidhaa tunayotakiwa kumpelekea Allah katika siku hizo ni swaumu

Kufunga sita si ibada ya faradhi, lakini ni sunna iliyotiliwa mkazo mkubwa. Hivyo, si vyema Muislamu kuizembea. Katika kuonesha umuhimu wa bidhaa (funga) hii, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Mtu yoyote atakayefunga Ramadhan kisha akafuatizia siku sita katika Shawal, huwa kama amefunga mwaka mzima.” [Muslim]

Katika rehema za Allah kwa waja wake ni kuwawekea Sunna katika kila ibada ya faradhi ili huunga mapungufu yaliyojitokeza. Baada ya Faradhi ya Ramadhan, kuna siku sita za mfunguo mosi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close