4. Darasa La Wiki

Simu zilivyotusahaulisha kumuabudu Allah

Simu za mkononi zimekuwa ni kitu cha kawaida siku hizi. ‘Smartphones’ kama zinavyofahamika na wengi zimeleta mapinduzi makubwa katika kuboresha mawasiliano na zinachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kiwango kikubwa.

Watu wengi wana uwezo wa kutumia simu zilizounganishwa katikamtandao wa intaneti na wanakwenda nazo kwenye shughuli mbalimbali. Hata hivyo, bahati mbaya simu hizi za mkononi pia zimekuwa chanzo cha kuharibu uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu.

Jamii yetu inakabiliwa na hatari kubwa inayotokana na teknolojia mbalimbali za kisasa katika jamii yetu, ambazo kwa sababu yake baadhi ya Waislamu wanakosa muda wa kumtumikia Muumba wao. Mathalani, wapo Waislamu wanaoamka mapema asubuhi lakini hata hivyo wanashindwa kuhudhuria misikitini kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Swala ya Alfajiri.

Badala yake, watu hawa, mapema asubuhi, hukimbilia kufungua simu kujua habari zilizojiri katika mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook, Twitter, Instagram na mingineyo. Yaani, hawajamshukuru Mwenyezi Mungu japo hata kwa kusema ‘Alhamdu Lillah’.

Hii inathibitisha ni jinsi gani baadhi yetu tulivyozipa simu nafasi ya Mwenyezi Mungu ndani ya nyoyo, fikra na maisha yetu kwa ujumla.

Si lengo langu kupinga matumizi ya simu, lakini nataka tuweke uwiano mzuri na wenye tija baina ya mambo muhimu ya kiibada na maisha yetu ya kawaida. Ni kwa kufanya hivyo ndiyo tunaweza kujenga uhusiano mwema na Muumba wetu.

Muislamu na simu za mkononi

Simu za mkononi mbali na kuleta faida, pia zimeleta madhara katika maisha ya Waislamu ambapo baadhi yao wamekuwa wakipoteza muda mwingi kufuatilia maisha ya watu kupitia mitandao ya kijamii na wameghafilika kabisa na utekelezaji wa ibada muhimu za Swala, Dhikri na kusoma Qur’an.

Japokuwa hii ni tabia ya mtu binafsi, lakini kiujumla tunasema, teknolojia ya simu imerahisisha mno mawasiliano kiasi cha kuleta madhara katika maisha ya Muislamu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Kwa sababu ya kuthamini sana simu, baadhi ya watu huona tabu kusaidia ndugu zao lakini wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kununua vifurushi vya maongezi na intaneti kwa ajili ya matumizi ya mtandao. Hivi ndiyo kusema, tumekosa staha ndani ya nafsi zetu kiasi cha kuzifanya simu kuwa ndiyo Mungu wetu?

Simu za mkononi na ibada ya Swala

Pamoja na kuwepo kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia bado tunapaswa kusimamisha Swala tano kwa ukamilifu. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an: “Basi, ole wao wanaoswali, Ambao wanapuuza (wanazisahau) Swala zao.” [Qur’an 107:4-5]. Licha ya maonyo haya, wengi wetu tumekuwa tukitekeleza ibada ya Swala kimazoea na bila ya kuchunga adabu, sharti na taratibu zakemara nyingi kwa sababu ya haraka ya kukimbilia simu. Moja ya adabu zilizosahaulika na Waislamu wengi ni kuingia msikitini bila ya kuzima simu jambo ambalo huleta usumbufu, kero na maudhi kwa Waumini hasa pale simu inapoingia na kutoa milio ya miziki.

Kuingia msikitini bila simu ni miongoni mwa matatizo makubwa yanayoendelea kujitokeza ndani ya misikiti yetu hivi sasa kiasi cha kuchangia kukosekana utulivu, unyenyekevu na ufanisi wa ibada miongoni mwa Waislamu. Imekuwa ni jambo la kawaida kwa Maimamu wengi wa zama hizi kuwaamrisha Waumini wao kuzima simu wakati wa Swala. Hata hivyo, hilo sio jukumu la msingi la Imamu bali lililo wajibu kwa Imamu ni kuwasisitiza Waumini wanyooshe safu bila kuacha mapengo baina ya mtu na mtu.

Katika hili, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Kwa hakika kunyoosha safu ni sehemu ya usimamishaji sahihi wa Swala, na kuweni karibu na nyoosheni safu zenu,” [Bukhari na Muslim]. Pamoja na hayo, yafaa tutambue kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mkubwa kuliko kitu chochote hivyo ni wajibu kwa kila Muislamu kudiriki ibada ya Swala msikitini na kujiepusha na kila chenye kuvuruga Swala za watu ikiwa ni pamoja na kuzima simu.

Katika hali ya kuonya, Allah Mtukufu anasema: “Na wale wanaowaudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri,” [Qur’an 33:58].

Ikiwa ukweli ndiyo huo, kwanini hatutii agizo la kuzima simu zetu wakati wa Swala ilihali tunaweza kufanya hivyo katika vikao na mikutano ya kijamii na ile ya kiserikali? Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe miongoni mwa wenye kusikia maneno na kufuata yaliyo mazuri.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close