4. Darasa La Wiki

Riziki inatoka kwa Allah peke yake!

Ufahamu kwamba ‘Rizq’ iko mkononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake ni moja ya nguzo za ‘Aqidah’ ya Kiislamu. Ufahamu huo pia, unainua mwenendo mzima wa Muumini kuelekea kumridisha Allah ‘Azza wa Jalla’ kwa kadri inavyowezekana.

Kama hiyo haitoshi, ufahamu kwamba riziki iko mkononi mwa Mwenyezi Mungu unapanua zaidi maono ya Muislamu na kumfanya afikiri tofauti kuhusu tamaa ya mali, na pia awe na subira katika hali ya umaskini na aweze kuikabili hofu ya ufukara.

Vilevile, Ufahamu huo, unaimarisha hamasa ya harakati za kutafuta riziki, lakini pia bila ya kuzifanya harakati hizo kuwa ndiyo lengo kuu la maisha ya Muislamu linalokwaza majukumu yake mengine na pia, unachochea ndani ya Muislamu hamasa ya kujitoa muhanga, kiasi kwamba ataachana na harakati za kutafuta Riziki ili kutekeleza majukumu mengine muhimu.

Huo ndiyo msimamo wa Muislamu yule anayefahamu kiukweli na kukubali kikamilifu kwamba riziki iko mikononi mwa Allah ‘Azza wa Jalla’ peke yake.

Wanaomini riziki iko mikononi mwa binadamu

Na msimamo huo uko kinyume kabisa na wale ambao ufahamu wao wa riziki una kiwingu na mkanganyiko wakiamini riziki iko mikononi mwa binadamu. Akili zao mara zote zimezongwa na mawazo ya kuongeza harakati za kutafuta riziki, kiasi kwamba hawajipi nafasi ya kufanya mambo mengine. Wakati wote wana muda wa harakati za kutafuta riziki, lakini hawana muda kwa ajili ya ibada na kulingania Uislamu.

Hawa wanaamini kuwa, harakati zao hizo ndizo pekee zitakazoongeza riziki zao. Mawazo yao yote yamejaa harakati hizo, bila ya kuacha nafasi kwa ajili ya mambo mengine muhimu.

Wakiitwa kwenye majukumu mengine watayatekeleza kwa kiasi kile tu ambacho hakiingiliani na harakati zao za kutafuta riziki. Wakiitwa kwenye harakati za kusimamisha Dini, kwa kuzingatia mbinu aliyofundisha Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie], watainua mikono yao juu kwa kung’aka, wakisema, “Imani yetu ni dhaifu!” au watafanya bila ya moyo wa dhati, huku mawazo yao yote yakihangaishwa na dunia.

Hebu sote tuweke mbele ya akili zetu kwamba, riziki inatoka kwa Allah ‘Azza wa Jalla’ peke yake. Maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ndani ya kitabu chake kisichokuwa na shaka, yanathibitisha, bila tone la shaka, kwamba, Yeye peke yake ndiye anayetoa riziki kwa kila roho aliyoiumba. Mwenyezi Mungu anasema:

Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndiyo tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa Mchamungu.” [Qur’an, 20: 132].

Allah ‘Azza wa Jalla’ amesema mahali pengine:

Na kuleni katika alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu, halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.” [Qur’an, 5: 88]. Amesema tena mahali pengine: “Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.” [Qur’an, 24: 38].

Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema pia kuhusu riziki: “Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengenezea njia ya kutokea. Na humruzuku kwa njia asiyoitarajia.” [Qur’an, 65:2-3]. “Na Hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha.”[Qur’an, 11:6].

Tuzitafakari aya hizi kwa kina, tuzielewe maana zake, tujisalimishe kwa maana hizo na tubadili mwenendo wetu kwa mujibu wa aya hizo. Kwa hiyo, si tu kwamba Allah ‘Azza wa Jalla’ alijua fulani na fulani watapewa riziki, kwa hiyo riziki itakuwa imeandikwa na imeshapangwa, bali zaidi ya hivyo ni ukweli kwamba Mkono Wake peke yake ndiyo unaotoa riziki!

Kwa hakika, Allah ‘Azza wa Jalla’ ndiye ‘Razzaaq’ [Mtoa Riziki]. Anampa riziki yule amtakaye. Na Yeye ndiye anayepanua riziki hiyo kwa yule amtakaye, na anayepunguza riziki hiyo kwa amtakaye. Hakuna ‘Razzaaq’ zaidi Yake. Hebu sote tufahamu amri ya kufanya harakati za kutafuta riziki, kwa kuifahamu riziki yenyewe.

Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema: “Yeye ndiye aliyeidhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. “ [Qur’an, 67: 15].”

Na itakapokwisha Swala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa. “[Qur’an, 62: 10]. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu ndiye ‘Razzaaq’.Yeye pekee ndiye anayetoa Riziki, na si mwingine yeyote.

Allah ‘Azza wa Jalla’ ameamrisha watu watembee na watawanyike katika ardhi, wakifanya harakati za kutafuta riziki. Hata hivyo, hiyo haina maana kwamba kufanya harakati ndiyo sababu ya kupata riziki! Kuanzia hapa ndipo kile kiwingu na mkanganyiko kinapoweza kutokea. Jitihada siyo inayotoa riziki bali ni moja ya sababu zakuweza kupewa riziki na Mwenyezi Mungu.

Mfanyabiashara anaweza kujitahidi sana kupata faida, lakini akaishia kula hasara. Mwekezaji wa kiwanda anaweza kujitahidi, lakini bidhaa zake alizozalisha zikafeli sokoni na akapata hasara. Kwa upande mwingine, anayerithi mali, anayechukua ‘Luqtah’ [hazina iliyotelekezwa], anayepata hiba [zawadi], zaka au sadaka – hawa wanapata riziki bila ya jitihada.

Vilevile mtu anayepata manufaa ya hukumu ya ‘Nafaqah’ [kuhudumiwa kifedha] dhidi ya yule anayewajibika kutoa ‘Nafaqah’ hiyo, pia anapata riziki bila ya kujitahidi. Vile vile kwa walemavu, watu dhaifu na wale wenye mapungufu ambao wanahudumiwa na dola, au wale ambao dola inawapa ardhi, hawa wote wanapata riziki bila ya kufanya jitihada na ni ushahidi kwamba kufanya jitihada siyo sababu ya kupata riziki bali ni njiabmojawapo ambayo Allah ‘Azza wa Jalla’ anaitumia kutoa riziki.

Kwa hiyo, tufikirie machaguo yetu kuhusu kujitahidi kupata riziki kwa mujibu wa muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake [rehema za Allah na amani zimshukie]. Tuiweke vizuri hii katika fikra zetu kwamba aliyefanikiwa siyo yule aliyejitahidi sana usiku na mchana kutafuta riziki, na kupuuza amri zingine katika Dini yake. Hapana. Aliyefanikiwa ni yule anayeuthamini Uislamu, anayefanya jitihada na atakayeridhika na kile ‘Allah Azza wa Jalla’ anachompa.

Amr bin al-As [Allah amridhie] amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu [rehema za Allah na amani zimshukie] amesema: “Amefanikiwa yule aliyeukubali Uislamu, ambaye ameruzukiwa kiasi cha kutosheleza mahitaji yake na ameridhika na kile ambacho Allah amempa.”[Muslim].

Badala ya wakati wote kuhangaika na kujuta kwa kupoteza fursa za kupigania riziki, hebu tuswali tu na kushukuru kwa chochote kile ambacho Allah ameturuzuku ambacho kinatosheleza mahitaji yetu na kutuimarisha.

Badala ya kujipinda kupita kiasi katika harakati za kutafuta riziki kwa gharama za majukumu mengine, basi tuwe kati kwa kati katika kutafuta riziki, ili kila jukumu linalotuhusu kama Waislamu tulipe muda wa kutosha kulitekeleza. Badala ya kumuonea gere yule mwenye milima ya mali, ambayo ataulizwa na Mwenyezi Mungu, hebu tumuonee gere yule ambaye ameridhika na kile alichoruzukiwa na Allah ‘Azza wa Jalla’. Tusijaze fikra zetu wasiwasi kuhusu riziki na nyoyo zetu maumivu kuhusu kupungua kwa riziki. Tuwe na yakini kwamba riziki zetu ziko mikononi mwa Allah ‘Azza wa Jalla’ peke yake.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close