4. Darasa La Wiki

Ria, adui namba moja wa ibada

Duniani, watu hufanya mambo mbalimbali ya kheri kwa malengo tofauti. Miongoni mwao, wapo waja wema ambao hufanya mambo ya kheri kwa utakasifu wa nia na kutaraji malipo kutoka kwa Allah.

Lakini, kwa upande mwingine, wapo wafanyao mema kwa malengo ya kupata maslahi ya kidunia. Imethibiti kutoka kwa Abu Sa’id (Allah amridhie) kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) aliwaendea wakati wakijadiliana kuhusu Dajjaal, akawaambia:

“Je, niwajulisheni kile ninachokihofia zaidi kwenu kuliko (hatari za) Dajjaal?” Wakasema: “Ndio (tujulishe).” Mtume akawaambia: “Tahadharini na shirk iliyojificha. Mtu anasimama kuswali, anaipamba na kuiremba sala yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama.” [Sunan Ibn Majah]

Maneno ‘shirk iliyojificha’ yaliyotumika kwenye hadith hapo juu yana maana ya ria au kujionyesha. Katika mtazamo wa sharia ya Uislamu, neno ria lina maana ya kufanya matendo yanayompendeza Allah lakini kwa nia ya kuwaonesha watu ili uonekane mwema au upate maslahi fulani kutoka kwao.

Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa ria ni kufanya amali njema kwa lengo la kuwaridhisha watu. Ndio kusema kwamba, mtu atendaye mema kwa kutaraji kupata manufaa ya kilimwengu, mema hayo hugeuka na kuwa matendo ya kishetani.

Hakika ria ni kirusi hatari kinachoweza kuiangamiza ikhlas ya mja, na hivyo kumkosesha fursa ya kulipwa thawabu za matendo mema Siku ya Kiyama.

Aghalabu, kirusi hiki huwashambulia watu wenye desturi ya kufanya wema kwa lengo la kutafuta utukufu, vyeo, shukrani au kusifiwa na watu. Mbali na kuidhuru Ikhlas, pia ria ni sababu ya mtu kutumbukia kwenye dhambi ya shirk.

Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Hakika ninachokihofia kwenu zaidi ni shirk ndogo.” (Maswahaba) wakauliza: “Ni ipi hiyo shirk ndogo?” Mtume akasema: “Ria.” Allah Mtukufu atasema Siku ya Kiyama wakati akiwalipa waja kwa mujibu wa amali zao: “Nendeni kwa wale mliokuwa mkijionyesha kwa amali zenu duniani kisha tazameni. Je, mtakuta kwao jazaa (malipo)?” [Ahmad].

Ni kwa muktadha huo, haijuzu Muislamu kufanya jambo jema kwa lengo la kuwaridhisha watu kwani Allah amewaandalia adhabu kali watu wa aina hiyo. Allah anasema katika Qur’an:

“Wanaotaka maisha ya dunia na mapambo yake tutawapa huku duniani (ujira wa) vitendo vyao kamili, humu wao hawatapunjwa. Hao ndio ambao hawatakuwa na kitu katika akhera ila moto na wataruka patupu waliyoyafanya katika dunia hii, na yatakuwa bure waliyokuwa wakiyatenda.” [Qur’an, 11:15–16].

Aya inabainisha kuwa, yeyote mwenye kufanya ria katika amali zake hana malipo akhera. Hivyo anayetaka kujiepusha na ria anapaswa kutanguliza Ikhlas katika matendo yake.

Lakini licha ya ubainifu huo, wapo baadhi ya ndugu zetu ambao hutenda kheri na huku wakizifuatisha na masimulizi. Katika hao wapo wanaojifaharisha kwa kusema: “Kama si msaada wangu, fulani angeumbuka”. Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu, watu wa aina hii, katu hawatopata fadhila za Mola wao isipokuwa hasara ya duniani na Akhera.

Zaidi Allah anasema: “Anayetaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi atende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi.” [Qur’an, 18:110].

Ni ukweli kuwa, pasipo na Ikhlas pana ria, na palipo na ria hapana Ikhlas. Kwa munasaba huo, yafaa tutekeleze amali zetu kwa ajili ya Allah kama ilivyothibiti katika Sharia ya dini.

Allah anawasifu Waumini wenye kutenda kheri na huku wakitaraji malipo ya akhera: “(Husema nyoyoni mwao wanapowapa chakula watu): Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (tu). Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. Hakika sisi tunamuogopa Mola wetu hiyo siku yenye shida na tabu.” [Qur’an, 76:8–10].

Ewe mja wa Allah, jiepushe na ria wakati unapotekeleza amali zako na kusudia kufanya mema kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah. Hakuna faida kwa mtu mwenye kutenda amali kwa ria isipokuwa kupata manufaa machache ya duniani na madhara makubwa akhera.

Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) anafahamisha kuwa: “Katika siku ya hukumu (Kiyama), vitendo vyote vilivyofanywa (duniani) vitahudhurishwa mbele ya Allah. Vitendo vilivyofanywa kwa ajili ya Allah vitatengwa. Na vitendo vingine vilivyofanywa kwa nia nyingine mbalimbali vitatupwa motoni.” [Baihaqi].

Kulingana na Hadith hii, mja anayefanya ibada kwa ajili ya kumridhisha Allah, anakuwa amehifadhi matendo yake mahala salama. Kinyume chake ni kutenda wema kwa ajili ya kuwaridhisha watu na hivyo kujikosesha fursa ya kulipwa thawabu na Allah.

Kwa kuzingatia hayo, yafaa kila Muislamu ajibidiishe katika kutenda amali nyingi za heri kwa kutaraji kupata radhi za Allah.

Utawajuaje watendao mema kwa ria

Ria hudhihiri kwa mtu mwenye kudumu na hali nne:

Mosi: Mwenye kuacha kufanya ibada au jambo la kheri kwa sababu ya kukosolewa au kutosifiwa katika utendaji wake.

Pili: Mtu kuonesha utulivu, unyenyekevu na adabu pindi anapotekeleza ibada mbele za watu, ilihali akiwa faraghani huzifanya katika hali ya uvivu na haraka.

Tatu: Mtu kupendelea kutoa sadaka ili watu wamuone.

Nne: Kuwatendea wema watu kwa kutaraji msaada wao pindi atakapowahitajia. Kuhusiana na hayo Allah anasema:

“Enyi mlioamini! Msibatilishe sadaka zenu kwa masimulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa ria (kujionyesha) kwa watu, wala hamuamini Allah na siku ya mwisho. Basi hali yake ni kama hali ya jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likafikiwa na mvua kubwa na kubaki tupu. Basi hawatakuwa na uweza (wa kupata) chochote katika walivyovichuma; na Allah hawaongozi watu makafiri.” [Qur’an, 2:264].

Inachukiza na kughadhabisha kuona mtu anamsaidia binadamu mwenzie, na kisha anaaza kumsimulia kwa watu. Tunamuomba Allah Mtukufu azitakase amali zetu kutokana na ria na atujaalie kuwa na Ikhlasi katika matendo yetu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close