4. Darasa La Wiki

Njia za kujikinga na wasiwasi

Kutafakari na kutaamali ni silka (sifa) ambazo mtu huzaliwa nazo kwa ushahidi wa kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) aliposema:

“Majina yanayoendanana na uhalisia wa mwanadamu ni Harith na Hammam.” [Bukhari katika Al–Adab Al– Mufrad].

Jina Harith lina maana ya mtendaji wa amali. Na jina Hammam lina maana ya mtu anayefikiri kwa utashi. Fikra hizo zinaweza kuwa sahihi au batili.

Kuna wakati Waislamu hupatwa na hofu wanapokumbana na mambo yenye kutatanisha na matokeo yake hugawanyika makundi mawili. Kundi la kwanza ni la Waislamu wanaoogelea katika dimbwi la wasiwasi na woga kiasi cha kukanusha mafundisho ya Kiislamu na misingi yake. Tunamuomba Allah atuepushe na hali hiyo.

Kundi la pili ni la Waislamu ambao hupatwa na wasiwasi katika dini, jambo linalowafanya wengi wao wabweteke na kuzituhumu nafsi zao kwa ukafiri na unafiki. Lililo wajibu kwa Waislamu ni kulinda silka na maadili ya dini, hasa ikizingatiwa kuwa zama tulizonazo zimetawaliwa na itikadi potofu za kidini na desturi mbaya.

Hivyo, kuna umuhimu wa kumuomba Allah atuepushe na itikadi potofu na desturi mbaya. Tusiache kusoma Surat Falaq na Surat Nnas.

“Sema: ninajikinga kwa Mola wa watu. Mfalme wa watu. Muabudiwa wa watu. Kutokana na shari ya wasiwasi (wa shetani) aendaye kisirisi kwa hila. Atiaye wasiwasi katika nyoyo za watu. Miongoni mwa majini na watu.” [Qur’an, 114:1–6].

Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie) walipokuwa wakipatwa na wasiwasi walimwendea Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) na kumwambia:

“Ewe Mjumbe wa Allah! Hakika katika nafsi zetu kuna fikra ovu zinazotupitia ambazo ni vigumu kuzisimulia. Hatupendi kuwa na fikra hizo wala kuzizungumzia.” Mtume akawaambia: “Ni kweli (fikra ovu) zimewapitia, na hiyo ndiyo imani ya kweli.” [Muslim].

Katika kuidadavua hadith hii, Sheikh Al–Islami Ibn Taymiya (Allah amrehemu) amesema:

“Hadith haimaanishi kuwa wasiwasi ndiyo imani ya kweli, bali wasiwasi ni katika vitimbi vya shetani. Imani ya kweli ni kile kitendo cha nafsi kuchukia wasiwasi.” [Taz: ‘Al– Imaan cha Ibn Taimiya,’ uk. 268].

Sheikh Ibn Taymiya anaendelea kusema: “Watu wote hupatwa na wasiwasi lakini wengi wao wanauendekeza wasiwasi na kujikuta wametumbukia katika dimbwi la ukafiri au unafiki. Kando na hao, wapo Waislamu ambao hawahisi chochote katika nyoyo zao pindi wanapopata matatizo kutokana na kugubikwa na mzigo mkubwa wa dhambi. Ni ukweli kuwa Waislamu wengi wanaotekeleza ibada ya sala hupatwa na wasiwasi ndani yake. Hii ni kwa sababu Iblis (shetani aliyelaaniwa) humghasi zaidi mja pindi anapojikurubisha kwa Mola wake Mlezi.”

Hivyo, kama tunataka kujikinga na wasiwasi hatuna budi kutumia njia zilizoelekezwa na sharia ya Uislamu. Hebu sasa tutaje njia hizo za kujikinga na wasiwasi na mashaka.

Mosi: Kujiepusha na fikra na wasiwasi wa shetani

Muislamu anatakiwa afikirie zaidi mambo yenye faida kwa jamii kama alivyosema Sheikh Ibn Taymiya (Allah amrehemu): “Tahadhari! usimuwezeshe shetani kutawala fikra na utashi wako. Shetani atakuharibia na atapandikiza fikra za uharibifu, wasiwasi na ataweka kizuizi usiweze kufikiria mambo yenye faida kwako ilihali wewe mwenyewe ndiyo umemkaribisha katika moyo wako.” [Taz: ‘Al– Fawaid,’ uk. 169–170].

Pili: Kujisalimisha na kunyenyekea kwa Allah

Uislamu ni kujisalimisha na kunyenyekea kwa Allah Ta’ala kwa kufuata maamrisho yake na kuacha makatazo yake yote kama alivyofundisha Mtume (rehema za Allah na amani imshukie).

Allah Mtukufu anasema: “La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe (Muhammad) kuwa ndiye muamuzi katika yale wanayohitilafiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wanyenyekee kabisa.” [Qur’an, 4:65].

Na katika Hadith iliyosimuliwa na Abdullah bin Umar, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema: “Hatoamini mmoja wenu mpaka matamanio yake yawe ni kufuata niliyokuja nayo (mimi Muhammad).” [Kitaab Al–Hujjah].

Hakika kukubali kwa dhati mafundisho ya Qur’an na Sunna za Mtume huondosha shaka moyoni. Wasomi wa taaluma ya falsafa walipokataa kufuata muongozo wa Uislamu walipata hofu na mashaka makubwa. Hilo limethibiti katika kauli ya wema waliopita ambao wamesema:

“Watu wenye mitazamo ya kifalsafa hupata mashaka makubwa wakati wa kukata roho.”

Tatu: Kuwa na yakini juu ya mafundisho ya dini

Yakini ni hali ya kuwa na imani au ithibati isiyo na chembe ya shaka juu ya kuwepo kitu au jambo lisiloonekana machoni. Kwa muktadha huo, Muislamu anapaswa kukubaliana na mafundisho ya dini yake bila shaka yoyote.

Na hii (yakini) ndiyo sifa kubwa ya waumini wa kweli kama anavyobainisha Allah ‘Azza Wajallah’:

“Hakika Waumini ni wale waliomuamini Allah na Mtume wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakapigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allah. Hao ndiyo wakweli.” [Qur’an, 49:15].

Yakini inapokita mizizi katika moyo, mtu hujawa na furaha na matumaini na huondokewa na hofu, chuki, woga, huzuni, wasiwasi na majonzi.

Aina mbili za ugonjwa wa wasiwasi

Kuna aina kuu mbili za ugonjwa wa wasiwasi (anxiety disorder). Kuna wasiwasi unaotokana na upungufu wa elimu, na kuna wasiwasi unaosababishwa na mashaka, simanzi au hofu moyoni.

Akitolea mfano suala la udhu, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema: “Mmoja wenu akipata kinachomtia shaka katika tumbo lake kuwa anatokwa kitu (mkojo au upepo kwenye utupu wake) au la, asitie udhu mwingine hadi atakapokuwa na yakini kuwa amesikia sauti yake au kuhisi harufu yake.” [Muslim].

Naye, Imam Ibn Qayyim (Allah amrehemu) amesema katika kitabu chake cha Madarij As–Salikiin:

“Hakika wanazuoni wa fani ya sharia wamesisitiza uyakinifu katika kanuni kuu ya misingi ya kifiqhi inayosema, ‘Yakini haiwezi kupuuzwa kwa sababu ya kuwepo shaka.” Kanuni hii hutumika katika masuala yote ya kisharia (Fiqh).

Yanayosababisha yakini katika moyo

Sheikh Al–Islami Ibn Taymiya (Allah amrehemu) amesema: “Yakini inapatikana katika mambo mengi. Kwanza, ni kuizingatia Qur’an, pili kuzingatia aya zinazoizungumzia nafsi na tatu kufanya amali njema kwa mujibu wa viwango vya elimu.” Kufanya amali njema kwa mujibu wa viwango vya elimu huleta ithibati na utulivu katika moyo wa muumini.

Hakika njia bora zaidi ya kuondosha waiwasi na mashaka ni kujikinga na shari za shetani. Na katika kuelezea ubaya wa shetani, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema:

“Shetani humjia mmoja wenu na kumuuliza, ‘Ni nani aliyeumba kadha na kadha?’’

Kisha Shetani huuliza, ‘Ni nani aliyemuumba Mola wako mlezi?’” Kisha Mtume akasema: “(Shetani) atakapofika huko, jilindeni na shari zake.” [Bukhari]. Na katika riwaya ya Muslim, Mtume amesema: “Atakayekutana na hali hiyo aseme, ‘Nimemuamini Allah.’”

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close