4. Darasa La Wiki

Ni msiba ushirikina unapohusishwa na biashara!

Ipo dhana potofu kwamba kutumia uchawi (ushirikina) kunasaidia kuvutia wateja katika biashara. Katika kusikiliza na kusoma kwangu, sijakutana na utafiti ama maandishi yoyote rasmi yanayodhihirisha kiusawa (fair verification) nafasi ya ushirikina katika mafanikio ya mtu kibiashara.

Wataalamu wa masuala ya biashara, taasisi za maendeleo, wanadini na watu wa kada ya kawaida wanasisitiza kuwa ushirikina hauna mchango katika mafanikio ya mtu si tu katika biashara bali hata katika nyanja nyingine. Pamoja na hayo, je ni kweli kuwa ushirikina haupo? Je, mioyo ya watu inaamini nini kuhusu hili?

Ukweli ni kwamba watu wengi wanaamini uwepo wa imani za kishirikina katika biashara, ingawa ni wachache wanaokiri kuutumia. Hata hivyo, idadi ya wanaofika kwa waganga wa kienyeji kutaka ndumba za kuwatajirisha inaongezeka siku hadi siku.

Jambo la watu kutumia ushirikina katika biashara haliwezi kuthibitishwa au kukanushwa kirahisi lakini licha ya ugumu huo vipo visa, tetesi na stori nyingi kuhusu ushirikina kwenye biashara.

Mathalani, katika miezi ya karibuni kuliripotiwa tukio la mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Fredius Philibert Kibengo (38) kumuua mama yeke mzazi kwa kumkata shingoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Ilidaiwa kuwa siku chache kabla ya mauaji hayo, mtuhumiwa alikwenda nchini Burundi kutafuta dawa za kuongeza utajiri na aliporejea alimueleza mkewe masharti aliyopewa. Mkewe hakuafiki masharti hayo.

Mbali na tukio hilo, tumekuwa tukisikia habari na tetesi za watu kumiliki misukule ambayo inatumika kuwafanikisha kibiashara kwa kuiba fedha kutoka kwa wengine. Imani hii ya misukule, majini ama ndumba kutumiwa kuiba fedha inaitwa chuma ulete.

Haitakuwa busara kwa viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanasiasa na wanahabari kukaa kimya au kutoa majibu mepesi kwa uovu kama ambao una athari mbaya kwa jamii.

Lakini je, kuna ukweli kiasi gani kuwa ushirikina unaweza kumfanikisha mtu kibiashara? Jibu linaweza kuwa ndio lakini sio kwa dawa anazopewa bali masharti ya udhibiti wa matumizi anayopewa.

Wakati mwingine mganga wa kienyeji anaweza kumpiga marufuku muombaji wa dawa za kuongeza utajiri kufanya mapenzi nje ya ndoa jambo ambalo linazuia kupotea kwa mali. Mganga anajua kuwa ni vigumu mfanyabiashara uwe na kimada halafu usihonge, haiwezekani. Na sote tunafahamu kuwa kuhonga kunapoteza fedha na kupunguza mtaji.

Waganga wengi pia huwapiga marufuku waombaji wa dawa za kuongeza utajiri kuvaa nguo nzuri na kulala mahali pazuri. Hapa kuna janja! Kwa mujibu wa saikolojia ya walaji (consumer behaviours) mtu anapomiliki pesa hujikuta anatamani kununua vitu vingi hata visivyokuwa na umuhimu.

Mganga anapomkataza mtu huyu asile wala kuvaa vizuri, ‘technically’ anakuwa anapambana na tabia ya kupenda kutumia ovyo. Waganga wa kienyeji wanafahamu kuwa pasipo kumdhibiti kisaikolojia mfanyabiashara huyu, anaweza kutumia ovyo hela ya mtaji na kujikuta biashara haikui. Ikiwa mtu hafanyi ‘shopping’ za gharama, hali vyakula vya anasa, ni wazi kuwa pesa nyingi zitabaki kwenye mzunguko na hivyo mtaji na biashara kwa ujumla vitakua.

Kiini cha tatizo

Ukosefu wa elimu sahihi ya biashara hupelekea watu wengi kusaka utajiri kwa njia za kishirikina. Wasichokijua watu wengi ni kwamba, kanuni nyingi zinazotumiwa na waganga wa kienyeji zipo katika sayansi ya biashara pia.

Kuna wakati waganga huwaambia wateja wao kuwa ili wapate wateja wengi katika biashara, waweke dawa katika milango ya kuingilia na kisha waongee vizuri na kila mteja anayeingia. Suala la kumjali mteja na kumchangamkia aingiapo eneo la biashara huzalisha wateja wengi, wazuri na wa kudumu.

Hii ni kanuni katika sayansi ya biashara na kamwe dawa iliyotundikwa haina maana kwa mfanyabishara. Kutokana na baadhi yetu kuendekeza imani za kishirikina biashara nyingi zimekuwa si za kudumu ama endelevu.

Cha kusikitisha ni kwamba wafanyabiashara wengi wanaotumia ndumba katika biashara zao hawana mfumo wa uendeshaji (business management system). Biashara ndiyo wao na wao ndiyo biashara.

Kwa kuwa mganga alimwambia: “Weka dawa hii kwenye droo ya mauzo na hakikisha haishikwi na yeyote”, mfanyabiashara analazimika kuwapo eneo la biashara muda wote ili asivunje masharti.

Biashara bila ushirikina inawezekana

Inawezekana kabisa mfanyabiashra kuepuka uchawi (ushirikina). Hapa nitataja mambo matatu mbayo mfanyabiashara akiyafanya atapata mafanikio anayoyatarajia.

Kwanza: Kumuamini Mwenyezi Mungu

Kila kitu (kinachoonekana au kisichoonekana) kimeumbwa na Mwenyezi Mungu, Mtawala wa kila kitu. Maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya kitabu chake kisichokuwa na shaka, yanathibitisha, bila tone la shaka, kwamba, Yeye peke yake ndiye anayetoa riziki kwa kila roho aliyoiumba.

Mwenyezi Mungu anasema: “Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndiyo tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa Mchamungu.” [Qur’an, 20: 132].

Mungu anasema mahali pengine: “Na kuleni katika alivyokuruzukuni Mwenyezi Mungu, halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.” [Qur’an, 5: 88].

Amesema tena mahali pengine: “Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.” [Qur’an, 24: 38].

Tuzitafakari aya hizi kwa kina, tuzielewe maana zake, tujisalimishe kwa maana hizo na tubadili mwenendo wetu kwa mujibu wa aya hizo. Imani za kishirikina zinachukua nafasi kubwa katika jamii kwa sababu watu hawana suluhu ya changamoto zinazowakabili.

Kwa mfano, ukosefu wa mvua unaotokana na watu kukithirisha madhambi, huwafanya watu wa jamii husika kuhusisha tatizo hilo na imani za kishirikina.

Pili: Kujielimisha

Ili kukwepa mawazo au uhusishwaji wa tukio fulani na imani za kishirikina, mtu anapaswa kujielimisha kuhusu tukio husika. Kwa mfano, ili kutohusisha kifo na ushirikina, mtu anapaswa kusoma sababu za kisayansi za kifo cha mtu husika n ahata takwimu za maradhi hayo.

Tatu: Kutafuta ushauri

Ili kupunguza uwezekano wa kupata hasara katika biashara mtu anapaswa kuomba na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu kabla ya kuanzisha biashara

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close