2. Deen4. Darasa La Wiki

Nafasi ya mama katika kuunda jamii yenye furaha

Hebu mfikirie mtu huyu aliyekubeba tumboni mwake kwa miezi tisa katika hali ya unyonge, kisha akakuzaa kwa tabu, akakukumbatia kifuani mwake na akashumu (akanusa) harufu yako, na akazihisi pumzi zako zikikariri (kuingia na kutoka).

Tunamzungumzia mama, ambaye maadui wa Mwenyezi Mungu wamemuwekea siku moja tu ya kumuadhimisha, jambo ambalo linakwenda kinyume na desturi za Kiislamu.

Ukirejea historia ya Uislamu (Tareikh) utabaini kuwa, Allah Mtukufu alimtuma Nabii Muhammad (rehema za Allah na amani imshukie) kuja ulimwenguni kuuhusisha Uislamu ulioasisiwa na Mitume waliomtangulia, akamkuta mwanamke akiishi chini ya mazingira na kivuli cha ukandamizaji.

Mwenyezi Mungu kupitia mfumo sahihi wa maisha (Uislamu), ambao dhamana ya uongozi wake alimpa Nabii Muhammad (rehema za Allah na amani imshukie) akamuondolea mwanamke unyonge, udhalili, dhuluma, uonevu na unyanyasaji ule.

Uislamu umemjengea mwanamke mazingira bora, kanuni na sheria ambazo zita– muhakikishia uhuru, usalama, amani , haki na usawa katika jamii yake na kumkomboa kutoka katika aina zote za utumwa.

Nafasi ya mama katika Uislamu

Katika Uislamu, mwanamke (mama) ni kiumbe aliyepewa hadhi na cheo cha kipekee kutokana na umuhimu wake katika kuilea familia. Kwa hiyo, mama ni moyo wa familia, pia mama ni nguzo muhimu katika kulinda na kuendeleza haki na ustawi wa watoto katika ngazi ya familia ambayo ndio kitovu cha jamii.

Kwa kifupi ni kwamba, Uislamu ni dini inayomjali, kumuheshimu na kumtukuza mwanamke wakati wote iwe usiku, mchana, wiki, mwezi hadi mwaka.

Nafasi ya mama katika malezi ya familia

Nafasi ya mwanamke/mama katika familia ni pamoja na kuwapa watoto malezi ya kiroho (kidini), kiafya, kiakili na kitabia. Kidini, watoto wote wanahitaji muongozo wa Qur’ an na Sunna sahihi za Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) ili waishi maisha ya mfano bora katika jamii.

Nasema hivyo kwa sababu, kiakili watoto ni wadadisi, hujifunza kwa kuiga. Kihisia, watoto wadogo huonesha hisia zenye nguvu ambazo baadae hutawala matendo yao. Kwa ajili hiyo, wazazi wanapaswa kutoa baraka kwa watoto wao siyo kutoa laana. Kama mzazi watazungumza maneno mabaya kwa mtoto wake ni mtu gani ana haki zaidi kwangu kuishi naye vizuri? Mtume alijibu: Ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni mama yako. Yule mtu akauliza tena: Kisha ni nani? Mtume akajibu: Kisha ni baba yako” (Imepokewa na Bukhari na Muslim).

Na katika riwaya nyingine imesemwa: “Ewe Mjumbe wa Allah! Nani ana haki zaidi kwa mimi kusuhubiana naye kwa wema?” Mtume aka jibu: “Ni mama yako, kisha mama yako, kisha mama yako, kisha baba yako, kisha wale walio karibu nawe kijamaa.”

Katika kuisherehesha Hadithi hii, Imam Qurtubiy amesema: “Mama anastahiki wema na hisani zaidi kuliko baba, na amemtangulia baba katika mashindano hayo.” Hii inatokana na shida na uzito anaopata mama katika kubeba mimba, kisha kujifungua, kunyonyesha, kulea, kuuguza na kumkuza mtoto katika hatua za mwanzo.

Tunajifunza kupitia Hadithi hizi kuwa, Uislamu haujampendelea mama bali umempa haki yake anayostahiki kulingana na wajibu wake.

Hii ndio sababu Uislamu umelifanya suala la kumtukuza na kum– uenzi mama kuwa ni wajibu upasao kutekelezwa na kuendelezwa kikamilifu katika siku zote za mwaka na siyo kuteua siku moja kwa ajili ya kumuadhimisha mama.

Hii ndio tofauti iliyopo kati ya dini ya Allah (Uislamu) na m i f u m o mbalimbali ya maisha iliyobuniwa na kufumwa na wanadamu wenyewe katika nchi zao. Hadhi na heshima ya mama katika Uislamu inajionesha wazi katika kauli ya Allah ‘Azza Wajallah” isemayo: “Na Tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumuachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.” (Qur’ an, 31:14).

Pia, imesimuliwa kutoka kwa Anas (Allah amuwie radhi) kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Amepata hasara mtu aliyekuwa mkubwa kisha wazazi wake wawili au mmoja wao yu hai, na asiwe sababu ya yeye kuingia Peponi.” (Taz: ‘Tuhfat Al–Ahwadhiy,’ 5/550).

Na katika riwaya nyingine, Mtume amesema: “Amepata hasara, amepata hasara, amepata hasara mtu ambaye wazazi wake wawili au mmoja wao wamefikia umri mkubwa (wa uzee) naye yu hai na asiingie peponi (kwa sababu ya kutowafanyia wema).” (Ahmad).

Ndugu yangu Muislamu, tambua kuwa kuwafanyia wema wazazi kunaendelea hata kama mzazi mmoja au wote wawili wamefariki. Wema huo unaweza kuuendeleza kwa kuwaombea dua, kuwatolea sadaka, kuwahijia na kadhalika.

Na katika moja ya mafundisho yake kwa waume, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuusia kwa kusema: “Muumini aliyekamilika kwa imani ni yule mwenye tabia njema, na mbora wenu ni yule aliye mbora kwa wake zake kitabia.” (Abu Daud na Tirmidhiy).

Na katika Hadithi nyingine, Mjumbe wa Allah amesema: “Mwanamke ameumbwa kwa ubavu, na sehemu iliyopinda ya ubavu ni juu yake, ukijaribu kuunyoosha utauvunja, na lau utauacha utaendelea kupinda, nakuusieni (kuwafanyia wema) wanawake.” (Bukhari na Muslim).

Nukta muhimu:

Ukisoma historia ya Swahaba Alkhansaa (Allah amuwie radhi), utaona umuhimu na nafasi ya mwanamke katika Uislamu na jamii kwa ujumla. Swahaba huyu alifahamika mno kutokana na ustadi wake mkubwa katika kutunga mashairi, pia alisifika kwa haiba nzuri iliyojaa fadhila, tabia njema, ushujaa na subira. Inasemekana hakukuwapo mwanamke aliyekuwa hodari wa kutunga mashairi kama yeye.

Ilipofika wakati wa vita vya Qaadisiya, Al–khansaa alidhihirisha subira yake pale alipowausia watoto wake kwa kuwaambia maneno haya mazito: “Enyi watoto wangu, naapa kwa Yule Ambaye hakuna Apasaye kuabudiwa ila Yeye, nyinyi ni watoto wa baba mmoja, sikumhini baba yenu, mmesilimu kwa kutii, mmehama kwa hiyari yenu, ….mtakapoamka kesho ‘Insha Allah’ kwa salama, nendeni vitani mkapigane na maadui zenu, kwani mnajua aliyowaandalia Allah. Tambueni kuwa nyumba ya milele (Pepo) ni bora kuliko nyumba ya kutoweka (Dunia).

Aliposikia habari ya kuuawa kwa watoto wake, alisema: “Namshukuru Allah Aliyetukuka, ambaye amenifanya mtukufu kwa sababu ya kufa kwao mashahidi.”

Na miongoni mwa haki alizopewa mwanamke ni haki ya kumhifadhi mkimbizi na kumpa amani mtu mwenye hofu aliyefanyiwa uadui katika nchi yake. Mwanamke wa Kiilsamu anaposaini mkataba wa amani na mtu yeyote (awe Muislamu au kafiri), mkataba huo unapaswa kuheshimiwa na Waislamu wote.

Si ruhusa kwa yeyote kutengua au kuhujumu mkataba huo kwa njia yoyote ile. Imepokewa Hadithi kutoka kwa Imam Muslim kwamba, Ummu Hanii (Allah amuwie radhi) alikwenda nyumbani kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) na kumpa habari ya mtu aliyemuomba hifadhi na amani. Mtume aliridhia jambo hilo kisha akasema: “Uliyempa wewe hifadhi ya amani ni kama tumempa sisi.” (Taz: ‘Alwafii fil Al–wafayati,’ 1/1459).

Allah amemtukuza mwanamke

Kama ambavyo Uislamu umempa mwanaume haki na uhuru wa kutoa maoni, pia Uislamu umempa mwanamke haki ya kutoa maoni na kusikilizwa katika mijadala, vikao na mikutano mbalimbali.

Mathalan, katika Aya iliyopo katika Surat Mujadala (Qur’ an: 58:1), Allah Ta’ala anamjibu mwanamke aliyekuwa akizozana na mumewe kwa kusema: “Mwenyezi Mungu amekwishasikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (Qur’an, 58:1).

Naam! Huyo ndiye mama, ambaye tangu enzi na enzi ameendelea kuwa msingi wa maisha yako. Basi humshukuru mama yako walau kwa kumfanyia wema na hisani?

Show More

Related Articles

Back to top button
Close