4. Darasa La Wiki

Mwanadamu na neema ya kulia

Moja ya maumbile yanayomtawala mwanadmu ni kucheka na kulia. Mwanadamu mwenye akili timamu akipata jambo la kumfurahisha hucheka, na akipata sababu ya kulia hulia.

Ni kawaida kabisa kuwaona watu wazima (wanaume na wanawake) wakitekwa na maumbile haya na kulia, tena hadharani. Katika Qur’an tunajifunza kwamba, aliyeumba kilio na kicheko ni yule yule aliyemuumba na kumpa umbo bora, naye ni Allah mtukufu.

“Naye ndiye achekeshaye alizaye.” [Qur’an, 53:43].

Kwa maana nyengine, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba vyanzo vya kucheka na vyanzo vya kulia. Tunapoiwasilisha mada kama hii kwa wasomaji wetu tunakuwa na lengo la kukumbuka neema nyingi na kubwa juu yetu, kwa kuwa Allah ametutaka tuzitaje na kuzisimulia.

Pia, makala hii inatusaidia kujifunza jinsi Allah Mtukufu alivyojitambulisha kwetu kwa njia zote, kama alivyosema katika Qur’an anasema:

“Tutawaonesha ishara zetu katika anga za mbali na hata katika nafsi zao mpaka iwabainikie ukweli, je haitoshi kuwa mola wako ni mjuzi wa kila kitu.”

Watu wengi hudhani kwamba kulia ni kuonesha udhaifu hasa ikiwa muhusika ni mtu mzima. Lakini uhakika hutubainikia pale tunapoelewa sababu zinazomfanya mmoja wetu kumwaga machozi na kulia hata kama mbele za watu.

Sababu na faida za kulia

Mtoto mdogo anapoonekana analia haishangazi sana kwani ukiziachilia mbali sababu tulizozitaja hapo juu, ana sababu nyingine za kitoto zinazomfanya aangue kilio. Mwenzake anaweza kumwambia tu: “Basi usije nyumbani kwetu” akalia. Au anaweza kumpiga mwenzake akalia yeye. Lakini mtu mzima akilia watu lazima watauliza: kulikoni?

Kuna sababu nyingi zinazowafanya watu walie. Sababu hizo ni pamoja na kufikwa na misiba, kama vile kuondokewa na mtu wa karibu, kupata maumivu makali mwilini, kufikwa na majanga kama vile kuteketea nyumba, shamba ama duka nk.

Mtu pia anaweza kulia kutokana na hofu iliyosababishwa na kutishwa ama kujisikia hana amani. Kadhalika, anaweza kulia kwa hofu ya kirorho na unyenyekevu kupitia ibada tofauti: dua, kusoma au kusikiliza Qur’an au mawaidha.

Kulia kwa kumuhofu Allah ilikuwa ndiyo mwenendo wa Mtume pamoja na Masahaba wake. Tunaelezwa kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alilia aliposomewa Qur’an na Abdallah bin Masoud (radhi za Allah zimfikie).

Mtume, katika hadith iliyosimuliwa na Anas, pia alikuwa akiwahimiza Masahaba kulia kwa ajili ya Allah kwa kusema:

“Lau mngelijua niyajuwayo mngelicheka kidogo na mkalia sana” basi masahaba wakafunika nyuso zao wakinguruma kwa vilio. [Bukhari na Muslim].

Na kutoka kwa Abuu Huraira (radhi za Allah zimshukie) amesema: amesema Mtume wa Allah :

“haliingii motoni jicho lililomwaga machozi kwa kumuhofu Allah labda maziwa yarudi katika chuchu zake..” [Tirmidhi].

Katika Qur’an na Sunna kama tulivyogusia-kuna msisitizo mkubwa wa kulia kwa ajili ya kumuogopa Mwenyezi Mungu. Na kutajwa kwamba, kufanya hivyo humsogeza mja katika radhi na rehema za mola wake. Allah Ta’la katika kutaja sifa za waja wake wema anasema:

“Na huporomoka kwa vichwa vyao chini wakilia na kuwazidishia unyenyekevu.” [Qur’an, 17 :109]

Bali machozi Mtume ameyaita ni “rehema” au “huruma” kama anavyoeleza Anas (radhi za Allah ziwe juu yake) “ nikiwa pamoja na Mtume tuliingia kwa mlezi wa mwanawe Ibrahima (alipokuwa mgonjwa), Mtume akamshika akambusu na kumnusa.

Kisha tukaenda tena akiwa anakata roho, macho ya Mtume yakawa yanatoa machozi, Abdurahman bin Awfi akamuuliza: na wewe pia (unalia) yaa rasoulallah? Mtume akasema:

“ ewe mwana wa Awf, machozi haya ni huruma aliyoiweka katika nyoyo za wenye huruma, jicho latoa machozi, na moyo unahuzunika, lakini hatusemi ila linalomridhisha Mola wetu, nasi kwa kutuondokea Ibrahim tunahuzunika.” [Bukhari].

Katika hadith hii na zinazofanana nayo tunajifunza kufaa kulia wakati wa msiba lakini bila ya kusema ya kumuudhi Mwenyezi Mungu. Kuna mara nyengine mtu anaweza kulia kwa sababu ya furaha kubwa iliyomfika. Chukua mfano wakati wa kumpokea jamaa yake aliyekuwa ughaibuni kwa muda mrefu!

Faida za kulia

Umuhimu na faida za kutoa machozi ama kulia ni nyingi. Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba, kilio cha wakubwa ni mrejesho wa utotoni. Saa nyengine watu wazima hulia kwa sababu wameona haja ya kuonewa huruma na walio karibu nao kama ilivyokuwa utotoni kwao. Na wanalia kwa vile hawapati njia nyengine ya kuzima joto la nafsi zao au kufikia malengo yao ila kutoa machozi. Hali hii hujitokeza zaidi kwa akinamama.

Wanasema pia: kulia -kwa mwanamume na mwanamke- ni njia bora salama ya kuirejesha hali ya kiafya katika nafasi yake. Ni pale mtu anapokuwa katika huzuni, simanzi na masononeko. Kilio huondoa mada zinzoudhuru mwili iwapo zitabakia kwa muda mrefu. kwani kilio huzidisha mapigo ya moyo kama mazoezi ya kuilainisha mishipa ya kifua na mabega. Na ndiyo mana mtu akimaliza kuli hujisikia raha kwa kuwa mapigo ya moyo yanarudi katika mwendo wake wa kawaida.

Si unawaona baadhi ya watu wakilia kilio cha kwikwi wakimaliza tu wanarudi katika mazungumzo ya kawaida na hata wanacheka?!

Kwa hiyo, wataalamu wanashauri kwamba, unapojisikia kulia, usizuie machozi. Kwani machungu, hasira na misononeko ya roho hutiririka (hutoka) pamoja na machozi na kuipumzisha nafsi. Hapa inadhihirika zaidi hekima ya Allah kuwafanya wanadamu walie. Mtu anaweza kuonekan analia anapoagana na mtu aliemzoweza, awe jamaa, rafiki au labda mwanafunzi mwenzake, wanapoagana baada ya kumaliza masomo.

Naam, kwa hiyo tujifunze kuwa, kulia mara nyingi kunakuwa na sababu za msingi kwa kweli –licha ya kwamba ni maumbile- pia ni neema kubwa kutoka kwa muumba wetu mtukufu inayotokana na athari ama mguso wa moyo. Na huzingatiwa kuwa ni ibada iwapo asili yake ni kumuhofu Allah.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close