2. Deen4. Darasa La Wiki

Mwaka 1441 Hijriya: Tuazimie kutekeleza sala tano ipasavyo

Kama tujuavyo, ibada ya kwanza kuhesabiwa Siku ya Kiyama ni sala. Sala ikiwa nzuri (ikikamilika), amali zilizobakia zitakuwa nzuri; na ikiwa mbaya amali zote zitakuwa mbaya. Ni kwa kutambua hilo, Uislamu unaihesabu sala kama ibada muhimu katika maisha ya Muislamu.

Katika kuonesha umuhimu na nafasi ya sala, Allah Mtukufu anasema ndani ya Qur’an: “Na popote uendako geuza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu, na popote mlipo geuzeni nyuso zenu upande uliko msikiti huo (Al– Kaaba)…” [Qur’an, 2: 150].

Miongoni mwa umuhimu, faida na fadhila za sala ni mja kujenga uhusiano wa karibu na Mola wake. Lakini kwa masikitiko makubwa wengi wetu tumekumbwa na changamoto katika kuitekeleza ibada hii, licha ya ukweli kwamba sala ndio nembo na kielelezo cha imani na utambulisho wa Muumini.

Katika hili, akina baba wanahusika kwani wao ndio ambao mara zote huonekana wakihudhuria misikitini huku wakiziacha familia zikiwa hazitekelezi wajibu huo. Kadhalika, wapo wanaoacha sala kwa kisingizio cha kutingwa na shughuli nyingi za utafuataji riziki.

Mbali na hao, pia kuna Waislamu wengine ambao huacha sala kwa sababu tu hawataki kupitwa na mechi za soka katika runinga. Ukifanya utafiti mdogo utagundua kuwa, wakati wa mapumziko ya mechi baadhi ya watu huchepuka na kwenda msikitini kutekeleza ibada ya sala.

Hali hii inawafanya wasali kwa kudonoadonoa kama kuku anavyodonoa mtama. Kwa sababu ya kupuuzia sala ambayo ndiyo njia ya kujiepusha na mambo maovu na machafu, wengi hujikuta wamezama katika mambo ya upuuzi na pumbao. Subhanallah!

Adabu za sala

Sala ndio msingi mkuu wa imani ya Kiislamu kama alivyosema Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie): “Hakika baina ya mtu na shirki na kufru, ni kuacha sala.” [Muslim]. Swali ni je, vipi tuitekeleze sala ili tupate kufaulu? Jawabu la swali hili ni kwamba, tunachotakiwa ni kusimamisha sala na si vinginevyo.

Kusimamisha sala ni tofauti na kusali. Kusimamisha sala ni kusali kwa kufuata kisawasawa sharti na nguzo zake zote; kunyenyekea na kuihudhurisha nafsi katika sala. Ukiacha jambo moja katika haya utakuwa hujasimamisha sala bali umesali tu.

Na bila shaka Mwenyezi Mungu atawaadhibu watu wanaopuuza sala kama anavyosisitiza katika Aya hii: “Basi, adhabu (kali) itawathibitikia wanaosali ambao wanapuuza sala zao (hawazisimamishi kisawasawa).” [Qur’ an, 107:4–5].

Tathmini ya sala zetu

Tumekwishaona adabu za sala katika Uislamu, hivyo ni jukumu letu kufanya tathmini ya kina katika sala zetu zote ziwe za faradhi ama za sunna. Tukusudie/tuazimie kuzitekeleza sala ipasavyo ili tuweze kupata mafanikio yake, vinginevyo, tutakuwa tunajiandalia maangamivu na hasara hapa duniani, kaburini na kesho Akhera.

Pamoja na hayo, tunapaswa pia kuzipima sala zetu kama zinatuepusha na mambo machafu au la. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an: “Bila shaka sala (ikisaliwa vilivyo) humzuilia (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na maovu, na kwa yakini ndani ya sala kuna kumkumbuka Mwenyezi Mungu kuliko kukubwa kabisa, na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.” [Qur’an, 29:45].

Hatari ya kusali kwa kudonoadonoa

Katika sunna za Kabliya, baadiya na sala ya Tarewehe katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wengi wetu tunasali kwa haraka sana kiasi cha kushindwa kuutuliza mwili wote sehemu tunapopaswa kufanya hivyo. Baadhi ya Maamuma tunawatangulia Maimamu wetu katika vitendo, ama tunakwenda sambamba nao.

Baadhi ya maimamu wanasoma sura fupi fupi kwa haraka (kama vile Surat Ikhlas) na kuwafanya maamuma/ wanaowafuata washindwe kumaliza kuisoma Surat Fatha. Hata pale zinaposomwa sura ndefu kwa lengo la kumaliza juzuu, zinasomwa haraka haraka bila ya adabu.

Kifupi ni kuwa, katika sala nyingi za Tarawehe hakuna unyenyekevu isipokuwa tunadokoadokoa tu nguzo mbalimbali katika sala nzima.

Kudokoadokoa sala ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo sharia na nguzo za sala, kutokuwa na khushui (unyenyekevu), kutokujituliza katika sala mahala inapopasa, kutokukamilisha visomo, kutozingatia tunachosema, na kadhalika.

Katika Hadithi ndefu iliyopokewa na Imam Bukhari na Muslim, Swahaba Abi Hureira (Allah amuwie radhi) amesimulia kwamba, kuna mtu aliingia msikitini, ambamo Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alikuwa amekaa, akasali rakaa mbili kisha akaja kwa Mtume na kutoa salamu. Mtume akajibu salamu yake kisha akamuambia: “Rudi tena ukasali kwani hukusali.”

Yule mtu akarudi, akasali (rakaa mbili) kama alivyofanya awali. Kisha akaja tena kwa Mtume na kurudia kutoa salamu. Mtume akajibu salamu yake na kumumbia: “Rudi tena ukaswali kwani hukusali.” Yule mtu akarudi, akasali (rakaa mbili) kama alivyofanya awali, kisha akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume akamuitikia kwa mara nyingine kisha akarejea kusema: “Rudi tena ukasali kwani hukusali.” Mtu yule akasema: “Naapa kwa Yule ambaye amekutuma wewe kwa haki, Ewe Mtume wa Allah, sijui vyovyote isipokuwa hivi, nifundishe.”

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema: “Ikiwa unasimama kwa ajili ya sala, sema, ‘Allahu Akbar’. Halafu soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur’an, kisha rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka uwe umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika sijida yako. Kisha kaa mpaka uwe umetulia katika kikazi chako. Kisha sujudu mpaka uwe umetulia katika sijida yako. Na uwe unafanya hivi ndani ya sala yako yote.”

Hivyo, ikiwa tunataraji kupata radhi za Allah, yatupasa tutekeleze ibada ya sala kama alivyoelekeza Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) katika Hadithi tuliyoitaja hapo juu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close