4. Darasa La Wiki

Muhimu ni kufia njiani, si lazima kufika

Baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kuhamia mji wa Madina, ni Maswahaba wachache tu waliobakia Makka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo maradhi na uzee. Miongoni mwa Maswahaba hao ni Dhwamratu bin Jundub (Allah amridhie) ambaye alishindwa kuvumilia joto la jangwani na mashaka mengine ya safari, na hivyo akaamua kubaki Makka.

Kwa sababu ya mapenzi yake makubwa kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), Dhwamratu alikata shauri naye kuanza safari ya kuelekea Madina ili kuungana na Mtume. Hata hivyo, alipokuwa katikati ya safari, akazidiwa na maradhi, akafahamu kuwa kifo kimekaribia.

Dhwamratu alijua kuwa hatoweza kufika katika mji wa Madina kuungana na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na Maswahaba wenzake (Allah awaridhie), hivyo akasimama na kupiga kiganja chake cha mkono kwenye kiganja kingine na kusema: “Ewe Mola wa haki, hiki ndicho kiapo changu cha utii kwako.” Kisha akapiga tena kiganja chake na kusema: “Na hiki ndiyo kiapo changu cha utii kwa Mtume wako (Bay–a).” kisha akaanguka chini, akafariki. Baada ya tukio hili, Jibril aliteremka na kumfahamisha Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kile kilichotokea, kisha ikashuka kauli ya Allah Ta’ ala:

Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata mahala pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na anayetoka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.” (Qur’ an, 4:100).

Na imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Twabraniy kuwa: “Dhwamra bin Jundub alipotoka nyumbani kwake aliiambia familia yake: “Nitoeni katika ardhi ya washirikina mnipeleke kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).” Naye akafia njiani kabla ya kufika (Madina), ndipo ikateremka aya hii.” (Taz: ‘Tafsir Ibnu Jariir/Ibnu Kathiir/ na Twabrani). Imam Albaniy (Allah amrehemu) amesema kuwa hadithi hii ni Hasan.

MAFUNDISHO YA TUKIO HILI
Si muhimu kukamilisha jambo, muhimu ni kuanza

Kuna mambo mengi yenye manufaa katika dini ya Allah na katika maisha yetu. Mara nyingi hutokea watu kushindwa kuyafikia mafanikio kwa sababu ya ugumu au ukubwa wa jambo lenyewe. Watu wengi hukata tamaa hata kabla ya kuanza jambo na hivyo wanashindwa kufanya mambo makubwa yenye manufaa kwa dini na dunia yao. Tunayo mifano mizuri ya kutuzindua katika hili ya kutufanya tutende, tuanzishe na tuweke misingi bora na imara ya kufikia malengo tunayojiwekea.

Lakini, hata kama tutashindwa kukamilisha maazimio tuliyojiwekea; kwa uwezo wa Allah, watatokea watu wengine watakaokamilisha. Wakikamilisha kazi, na sisi pia, mchango wetu katika kuindeleza dini au kuwainua watu katika maisha yao, bila shaka utakuwepo.

Kwa upande wa masuala yanayofungamana na elimu, tuna mifano mingi inayothibitisha kuwapo watu walioanzisha miradi mikubwa na ya maana itakayoinufaisha jamii ya Kiislamu bila kujali kama wataweza kukamilisha miradi hiyo, lakini kwa sababu walifanya hayo kwa utakasifu wa nia, Allah aliwajaalia waja wake wengine kukamilisha miradi hiyo kutokana na umuhimu wake na manufaa yake.

Ni dhahiri kuwa kama walioanzisha miradi hiyo wangetathmini mwisho wa kazi hiyo na ugumu wake, basi wasingeanza kuifanya kwani safari ya kuikamilisha ingekuwa ndefu mno. Katika mifano hiyo, tunaona namna Sheikh Muhammad al–Amiin Ashanqiytwiyyu, alivyoanza kutafsiri Qur’ an. Katika tafsiri yake mashuhuri inayoitwa ‘Adhwaaul-bayaan fii tafsiiril Qur’an bil Qur’ an’, Sheikh Ashanqi-ytwiyyu alifanya kazi kubwa akitafsiri Qur’ an kwa Qur’ an, kazi ambayo hakuweza kuimaliza mpaka umauti ulipomkuta akiwa ameishia Surat Mujadala. Hatimaye tafsiri hiyo ya ikakamilishwa na mwanachuoni mwingine, Sheikh Muhammad Atwiyya Salim.

Kadhalika, tunapoitazama tafsiri ya Jalaalain, tunaona kuwa imetafsiriwa na wanachuoni wawili. Baada ya mmoja wao kufariki, mwingine akaiendeleza. Awali tafsiri hiyo inayojulikana kwa jina la ‘Tafsiirul Jalaalain’ iliandikwa na Sheikh Jalaaluddin al-Mahalliy na kumaliziwa na Jalaaluddin Assuyuutwiy. Hivi ndivyo ambavyo Muislamu anatakiwa kuanzisha safari ya jambo adhimu litakalounufaisha umma.

Kuwa na maazimio ya kweli katika kuitekeleza haki

Kuna wakati mwanadamu hufanya mema na wakati mwingine hutenda maovu. Kuyumba huku kunaonesha kuwa bado watu hawajafikia maazimio ya kweli ya kudumu katika safari ya kufikia mambo ya kheri waliyoyaazimia au kuhakikisha wnakufa hali ya kuwa wamo ndani ya matendo ya kheri na yaliyo bora.

Allah Aliyetukuka anasema:
“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.” (Qur’an, 3:102). Na katika hali ya kutuhamasisha kudumu katika njia (dini) yake, Allah Ta’ala anatuambia: “Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie yakini (mauti).” (Qur’an, 15:99).

Katika kuitafsiri ya aya hii, Sheikh Albaaniy (Allah amrehemu) amesema, njia ya kuelekea kwa Allah ni ndefu, lakini si muhimu kufika mwisho wake bali muhimu ni kufa ukiwa katika njia hiyo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close