4. Darasa La Wiki

Moyo wa Muislamu una hofu na matumaini!

Siyo ajabu ukaona mtu asiyeamini akiishi katika huu ulimwengu akiwa amesahau kabisa kuhusu maisha baada ya Akhera. Yaani, hana hofu hata chembe ya nini kitamtokea akifa. Huyu amekana kabisa rehema za Allah ‘Azza wa Jalla’ ikiwemo kuumbwa, huku pia akikanusha uwepo wa Mwenyezi Mungu.

Mtu huyo ameyageuza matamanio yake kuwa mungu na amejikabidhi kwa Shetani ambaye amemvutia na kumpambia ulimwengu na raha zake. Shetani amemshawishi mtu huyo kwa matamanio ili kuridhisha hisia zake na mahitaji bila ya kikwazo au hofu.

Huyo ni asiyeamini. Vipi hali ikiwa hivyo kwa Muislamu? Vipi Muislamu akifuata njia ya asiyeamini, yaani asiwe na habari kabisa na Akhera na hatima yake huko? Hakika hilo litakuwa ni jambo la ajabu sana, kama ilivyo ajabu iwapo Muislamu akiishi hapa duniani bila kuzingatia Sharia na hukumu za Muumba wake!

Muislamu ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu kama Mola wake, Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Qur’an Tukufu kama Kitabu na katiba yake; anawezaje kuishi wakati Uislamu ukiwa umeondolewa kwenye maisha yake, isipokuwa kwa vitendo vichache vya ibada!?

Vipi Muislamu huyo anaweza kuishi kwenye mfumo wa kikafiri ambao unamlazimisha kuwa mbali na Mola wake na kukaa mbali na muongozo wake? Vipi Muislamu anaishi maisha ambayo wakati wote anakimbizana kutafuta mahitaji yake hadi moyo wake unakufa na kupoteza hofu ya Mwenyezi Mungu? Kwa nini Waislamu wengi wameachana na biashara nzuri na kung’ang’ania biashara hatari inayowaletea hasara? Kwa nini hawazingatii Akhera na wamekamatwa na ulimwengu huu usiodumu?

Kwa nini mioyo ya walio wengi imekuwa migumu kiasi kwamba hawaogopi matokeo ya dhambi wanazotenda? Na unawaona ama wanakuwa kiburi kwa ushauri wanaopewa, huku majivuno ya dhambi yakiwa yamewakamata?

Au ndio tuseme wanategemea rehema za Mwenyezi Mungu, wakidai: “Mwenyezi Mungu ni msamehevu na mwenye huruma,” kwa hiyo hawajali kabisa madhara dhambi zao, ziwe kubwa au ndogo.

Imesimuliwa na Abu Huraira (Allah amridhie) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema kwamba, Mola wake amesema: “Kwa Utukufu Wangu, sitawaletea waja wangu mara mbili ya hofu na mara mbili ya ulinzi. Iwapo ataniogopa katika huu ulimwengu nitamlinda Siku ya Kufufuliwa, lakini iwapo alijihisi yuko salama kutoka Kwangu ulimwenguni, nitamfanya awe na hofu Akhera.” Watu hawa hawaelewi hadithi hii ya kiungu? Hawatafakari maneno yake?

Kiapo cha Mola wao kwa Utukufu Wake hakiwatikisi? Wanaishi vipi kwa usalama katika ulimwengu huu bila ya hofu ya Muumba, halafu watarajie kuishi kwa usalama ule ule Akhera? Waletewe mara mbili ya ulinzi kwa pamoja? Kwa hakika, hilo haliwezi kutokea, na Allah ‘Azza wa Jalla’ ameapa kwa Utukufu Wake kutoleta hayo pamoja kwa waja Wake!

Muislamu, kwa hiyo, lazima atarajie mazuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ambavyo pia lazima aogope adhabu Zake. Ili atembee vyema katika ulimwengu huu, Muislamu lazima aunganishe hayo mawili mpaka atakapokutana na Mwenyezi Mungu.

Yaani, Muisamu anatakiwa atembee katika ardhi akitafuta halali katika vitendo vyake na kuepuka haramu, akimuogopa Mola wake, akitafuta malipo Yake. Pia, asidanganywe na kazi yake akidhani kwamba ndiyo mkombozi wake na kusahau rehema za Mwenyezi Mungu.

Imesimuliwa na Anas bin Malik (Allah amridhie), kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimuona kijana mmoja aliyekuwa anakufa na kumuuliza: “Unajisikiaje?” Akajibu: “Nina matumaini na Allah, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, lakini nina hofu na dhambi zangu.” Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisema: “Vitu hivyo viwili (matumaini na hofu) havikai pamoja kwenye moyo wa mtu aliye katika hali kama hii, isipokuwa Allah atampa kile alichokuwa anatumaini na kumuweka mbali na kile alichokuwa anakihofu.”

Hivi ndivyo Muislamu anavyopaswa kuwa: mwenye hofu na mwenye matumaini. Hofu na matumaini kwa Mwenyezi Mungu vinamsukuma mtu kwenye matendo mema na kutarajia mazuri kutoka kwa Allah ‘Azza wa Jalla’ na rehema Zake, nayo hiyo ndiyo njia ya kuepuka Moto na kuingia Peponi.

Hiki ndicho Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alichowasiliana na umma wake na ndicho alichotaka kupandikiza kwenye nyoyo za Maswahaba wake na Waislamu wote. Aliwahakikishia kwamba, wanapaswa kumuhofu Mwenyezi Mungu na kutojihisi wako salama wakati wanapojiondoa na kujiweka mbali na muongozo wa Mola wao. Wanapaswa kumtegemea, na kumuomba awafanye wawe madhubuti, kama alivyokuwa akifanya yeye.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa mara kwa mara akimuomba Mwenyezi Mungu kuudumisha moyo wake kuwa madhubuti katika dini Yake na utiifu Kwake! Huyu ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kipenzi Chake, ambaye Allah ‘Azza wa Jalla’ amemsamehe yale yaliyopita katika makosa yake na yatakayofuata, na ameahidiwa Pepo! Vipi sisi?!

Sisi tuko daraja la ngapi kutoka kwa Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) ambaye aliunganisha hofu na matumaini na alikuwa anajua vyema ukubwa wa jambo hili, na kwa hiyo alimuabudu Allah ‘Azza wa Jalla’ kama anavyopaswa kuabudiwa na akazawadiwa Pepo Yake?

Muislamu anapaswa kukosa furaha kama anatenda dhambi, kama anazembea wajibu au anapuuza jambo lolote la dini yake. Pia, lazima awe na hofu katika maisha yake yote na ghadhabu za Mwenyezi Mungu na kisasi chake. Vilevile, lazima ahofie mateso ya Moto. Hofu hii ndiyo taa inayoangaza moyo wake, na kwa hivyo ikimuondoka moyo huu utaharibika, na mmiliki wake atapotea, na vitendo vyake vitafisidika. Muislamu leo anawezaje kuhakikisha kwamba Mola wake amemridhia na kuishi katika huu ulimwengu bila ya hofu ya hatima yake Akhera?!

Vipi Muislamu anaweza kusonga mbele katika ulimwengu huu, wakati amepuuza jambo hili muhimu, la kuwa na hofu, ambalo linamlinda dhidi ya kutenda dhambi na kumzuia kufuata matamanio? Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema:

“Hakika adhabu ya Mola wako yafaa kutahadhari nayo.” [Qur’an,17:57].

Hofu inamtaka kufanya matendo mema na kuacha makatazo, lakini bila ya kuingia kwenye ile hofu iliyokatazwa ambayo inasababisha kukata tamaa na kutoka kwenye rehema za Mwenyezi Mungu. Allah Azza wa Jalla anasema:

“Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa makafiri.” [Qur’an, 12:87].

Muislamu analenga kupata radhi za Mwenyezi Mungu, upendo Wake, na malipo Yake na kuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Allah Azza wa Jalla anasema: “Hakika wale walioamini na wale waliohama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndiyo wanaotaraji rehema za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 2:218].

Hamu ya Muislamu ni matumaini yake ya kumridhisha Mola wake, kitu ambacho kinamsukuma kuendelea kutenda mema, kwa hiyo anashindana katika mema na anajipinda kuongeza utii wake kwa Allah ‘Azza wa Jalla’. Moyo wa Muislamu umeambatana na Pepo na rehema zake, na anajitahidi kuilazimisha nafsi yake iwe kama vile Mwenyezi Mungu alivyowaahidi wachamungu Akhera. Lazima awe na moyo unaoishi upendo wa Allah ‘Azza wa Jalla’, na unaoruka kama ndege na mbawa zake!

Ibn al-Qayyim (Allah amrehemu) amesema: “Moyo katika njia yake kuelekea kwa Mwenyezi Mungu ni kama ndege, ambapo upendo ni kichwa chake, na hofu na matumaini ni mbawa zake.”

Hofu na matumaini ni mbawa za moyo wa Muislamu. Hawezi kuruka na kufikia lengo lake iwapo atapoteza mojawapo. Wakati Muislamu anapokamata Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kusoma aya zake, anaogopa na kujawa hofu anapofika katika aya zile ambazo Allah ‘Azza wa Jalla’ amewaahidi Makafiri na wanafiki na anakuwa na wasiwasi asiwe mmoja wao.

Na wakati anaposoma aya ambazo Mwenyezi Mungu anawaahidi Waumini neema na kuwa pamoja na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), anafurahia hiyo na anajitahidi kufikia daraja ya watu hao na anamuomba Mola wake kumfanya mmoja wao.

Kwa hiyo, Muislamu lazima awe katikati ya hali mbili, hali ya hofu na hali ya matumaini. Kama nafsi yake itamzidi na kumvuta kwenye dhambi, lazima akumbuke hofu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Na kama nafsi hiyo itampeleka mbali na matendo mema, lazima arejee kumkumbuka Mwenyezi Mungu na rehema Zake na msamaha Wake.

Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema: “Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao – hata miongoni mwao walio karibu mno – na wanataraji rehema zake na wanaihofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako yafaa kutahadhari nayo.” [Qur’an, 17:57].

Leo, Waislamu duniani wanaishi katika mfumo ambao unatenganisha dini kutoka kwenye maisha! Huu ni mfumo wa kikafiri ambao haumuhofu Mwenyezi Mungu wala hautumai rehema zake! Huo ni mfumo wa kidhalimu ambao una chuki na dini hii na wafuasi wake! Waislamu wanakubali vipi jambo hili! Vipi tutakuwa salama na adhabu ya Mwenyezi Mungu?

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close