4. Darasa La Wiki

Mdhukuru Allah Aibariki Nyumba Yako

Dhikri au kumtaja Allah ndiyo uhai na usafi wa nyumba ya Muislamu. Utekelezaji wa jambo hili ni kielelezo cha kufikia lengo la kuitakasa nyumba dhidi ya maadui na viumbe waovu. Kinyume chake ni kutomdhukuru Allah kunakopelekea shida na balaa ndani ya nyumba. Kuipenda na kuikumbatia dunia ni moja ya sababu inayowafanya wengi waghafilike na na ibada ya kumtaja Mwenyezi Mungu. Lakini Allah Mtukufu anasema: “Mwenye kughafilika na utajo wa Mwenyezi Mungu, tunamfanya Shetani kuwa ndiye rafiki yake,” (Qur’an, 43:36). Aya hii ni ushahidi juu ya kuwepo idadi kubwa ya watu wanaosibiwa na magonjwa ya husda, kijicho, kurogwa, uchawi na kukosa raha ya maisha kunakotokana na kuwa mbali na dhikri. Kuepuka haya, kila Muislamu anapaswa kujibidiisha na kusoma Qur’an, na dhikri nyinginezo kadiri awezavyo. Kwa kufanya hivyo ndiyo mja ataweza kuhifadhika na kila aina ya balaa na misukosuko. Dini Tukufu ya Uislamu inawahimiza wafuasi wake kudumu na ibada hii kama njia ya kuwanusuru na giza na maangamizi ya duniani na akhera. Mwenyezi Mungu anakumbusha: “Enyi mlioamini! Mdhukuruni Allah kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni asubuhi na jioni. Yeye na Malaika wake ndiyo wanakurehemuni ili kukutoeni gizani na kukupelekeni kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini…” (Qur’an, 33:41-43). Na katika hadithi, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) anatuambia: “…Hakufanya binadamu kitendo kinachomuepusha zaidi na adhabu ya A l l a h k u l i k o k u m t a j a Allah”(Twabrani). Ndugu Muislamu, kusoma Qur’an ni jambo unalopaswa kuliwajibikia ili kuifanya nyumba kuwa na baraka. Abu Huraira (Allah amuwie radhi) anaripoti kuwa, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Msifanye nyumba zenu makaburi kwani nyumba inayosomwa Suratul-Baqarah haingii Shetani” (Sahihi AlJaami’i). Tambua na fahamu kuwa, dhikri ndiyo njia ya kukuondeshea wasiwasi, hofu na woga uwapo nyumbani, ofisini, sokoni au matembezini. Kwenda kinyume na hivyo ni kujiingiza kwenye maangamizi na dhiki ya duniani na akhera. Pamoja na ukweli huu, ni Waislamu wachache ambao hutumia muda wao katika kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Katika kuelezea umuhimu wa dhikri, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Maneno mawili yanayopendeza kwa Mola, mepesi katika ulimi, mazito katika mizani, nayo ni subhanaallah wabihamdihi, subhanaallahil adhwiim”, (Bukhari na Muslim). Ni hasara iliyoje kwa Muislamu kupitwa na siku nzima bila ya kumtaja Mola wake walau kwa uchache. Mfano wa suala hili tunaweza kuupata kupitia baadhi yetu ambao huthubutu kuingia majumbani bila kusoma dua, na kinyume chake tumekuwa tunaingia huku tukiimba na kupiga makofi bila kutambua kuwa, kufanya hivyo ni kumkaribisha Shetani katika nyumba. Kuhusiana na hilo, Mtume amesema: “Anapoingia mtu nyumbani kwake, akawa ni mwenye kumtaja Allah wakati wa kuingia na wakati wa kula basi husema Shetani kuwaambia wenzake, ‘Tumekosa kula wala kulala humu leo’” (Muslim). Ni muhimu kuiwajibisha nafsi katika kumtaja Mwenyezi Mungu mara kwa mara. Na kwa ajili hiyo kila mmoja ajenge mazoea ya kuitamka Bismillah na kutoa salaam wakati wa kuingia nyumbani na kula chakula ili kumnyima Shetani nafasi ya makazi na chakula ndani ya nyumba yake. Kwingineko Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) anatuambia: “‘Hivi niwaambieni habari ya matendo yenu bora, na ambayo ni masafi mno, mbele ya Mola wenu, na ambayo ni ya juu mno katika daraja zenu, na ambayo ni bora kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, na ambayo ni bora kuliko kukutana na adui zenu, mkawapiga shingo zao, nao wakakupigeni shingo zenu?’ Wakasema Maswahaba, ‘Ndio’. Akasema Mtume, ‘Ni kumtaja Mwenyezi Mungu’” (Ahmad). Epuka kutenda haramu nyumbani kwako Kujitenga na mambo yaliyoharamishwa ni katika namna ya kuifanya nyumba kuwa na baraka. Miongoni mwa mambo ya haramu ambayo Muislamu anapaswa kuyaepuka ni kusikiliza muziki, kuweka picha za viumbe kwenye kuta, kuangalia video zisizozingatia maadili, kunywa pombe na mengineyo. Kwenda kinyume na hivyo ni kushirikiana na Shetani Iblis katika kutenda maovu ndani ya nyumba. Kwa hali, hii tunawajibika kuziepusha nafsi zetu na muelekeo mbaya wa kuikumbatia haramu. Hii itatusaidia kuzitakasa nafsi pamoja na nyumba zetu ili kuishi katika hali ya utulivu, usalama na amani. Nasaha hizi ni ukumbusho kwa yeyote mwenye kutafuta suluhu ya dosari mbalimbali zinazoweza kujitokeza ndani ya nyumba. Tumuombe Mwenyezi Mungu atuepushie mitihani na matatizo katika nyumba zetu, na pia atusaidie tuweze kufuata njia za kisheria katika kutafuta suluhu ya matatizo. Aamiin

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close