4. Darasa La Wiki

Mbinu tisa za kuepuka maasi

Allah ‘Azza Wajallah’ anasema: “Hakika sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayoyatanguliza na wanayoyaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asili lenye kubainisha.” [Qur’ an, 36:12].

Aya hii tukufu inawakumbusha wanadamu kwamba chochote wanachokifanya katika maisha haya ya dunia kinaandikwa na Malaika kwenye kitabu cha kumbukumbu ya matendo ya waja.

Pamoja na ukweli huo ambao kwa bahati nzuri wengi wetu tunauamini, bado wapo watu wengi wanaomuasi Mungu bila hofu wala woga. Shirk, uchawi, kula riba, kula mali za yatima, kula rushwa na kuwaasi wazazi wawili ni baadhi tu ya madhambi makubwa yanayofanywa na watu wengi duniani.

Baadhi yetu tunatamani kuacha maovu haya na mengineyo, lakini tunashindwa kuyaacha kwa sababu hatujui tutumie njia gani kuyaepuka. Kutokana na unyeti wa suala hili, nimeona ni vema nikujuze mbinu tisa (9) ambazo zinaweza kukusaidia kuyaepuka maasi. Sasa tutaje mbinu hizo za kuepuka maasi.

Mosi, nia njema

Mwanadamu anatakiwa aazimie moyoni kuacha maasi. Nasema hivyo kwa sababu, siku zote moyo ndiyo unaomsukuma mtu kutenda maovu. Qur’ an inasema:

“Hakika nafsi (kazi yake) huamrisha maovu isipokuwa ile iliyorehemewa na Mola wangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni msamehevu na mwenye kurehemu.” [Qur’ an, 12:53].

Hivyo, kama tunataka kuzitakasa (kuzisafisha) nafsi zetu ni lazima tumrudie Allah kabla ya kufikwa na umauti. Wanadamu hatupaswi kuyarudia maasi kwani kufanya hivyo kutapelekea kuongezeka kwa majanga zaidi duniani.

Pili, tafakari athari ya dhambi

Unapotaka kufanya jambo unapaswa kutafakari kwanza faida na hasara ya jambo lenyewe. Kama lina faida jiulize, jambo hili ni halali mbele ya Allah? Na je, siyo dhambi mbele ya Allah? Kama ni la dhambi hupaswi kulifanya kwa sababu Allah anachukia madhambi.

Mtu anapotenda dhambi anakuwa ameikataa asili yake na kukubali kuwa chini ya shetani. Kwa hiyo, ikitokea umetenda dhambi, basi chukua hatua ya kutubu ili kuepuka ghadhabu za Mwenyezi Mungu.

Tatu, epuka vichocheo vya maasi

Tabia nyingi mbaya huchangiwa na watu au mazingira fulani. Ikiwa una marafiki wanaokushawishi kutumia dawa za kulevya, kuzini au kunywa pombe, basi waepuke.

Ndugu Muislamu, ukitaka maisha mazuri, jitenge mbali na vichocheo vya dhambi kwani Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema:

“Yeyote aachaye jambo kwa ajili ya Allah, basi Allah humbadilishia chenye kheri zaidi kuliko hilo (aliloliacha).” [Ahmad].

Lakini fahamike kuwa, uchamungu si kuzidisha mema tu, bali pia kuepukana na maasi na kudumu katika kufanya mambo mema. Na ili mtu aweze kudumu katika utiifu wa Allah, ni lazima ajiepushe na maasi.

Nne, anza taratibu

Mara nyingi tabia uliyoizoea ni vigumu kuiacha kwa siku moja. Hivyo jitahidi kuiacha taratibu mpaka ipotee kabisa. Kwa mfano, kama umezoea kuangalia picha za ngono mitandaoni, anza kukaa mbali na tovuti zinazojihusisha na masuala ya ngono.

Kuacha maasi ni jambo gumu linalohitaji subira na uvumilivu wa hali ya juu. Na maana ya subira ni kubakia katika utiifu, kuacha maasi na kuridhika na makadirio (mpango) wa Mwenyezi Mungu.

Mjumbe wa Allah amesema: “Hakuna yeyote aliyepewa zawadi bora na iliyo kunjufu zaidi kuliko subira.” [Bukhari na Muslim]. Kadhalika, wema waliotangulia (Salafi) wamesema: “Hakika subira ni nusu ya imani.” Kwa hiyo, Muumini anapaswa kuwa na subira na uvumilivu katika kuacha maasi kwani hiyo ndiyo ngazi ya kuufikia uchamungu.

Tano, jiwekee malengo

Kuweka malengo kuna faida kubwa sana maishani. Moja ya faida hizo ni kumuwezesha mtu kudhibiti mwelekeo wa mabadiliko katika maisha yake ikiwamo kuacha maasi.

Kwa mfano, unaweza kuamua kununua au kufanya mambo yenye faida kupitia pesa ambazo huko nyuma ulikuwa unazitumia kwa ajili ya kucheza kamari, kununua sigara, pombe na vitu vingine vya haramu. Haya ni mfano tu wa malengo ambayo unaweza kujiwekea na yakakuongoza na kukuhamasisha kuacha maasi.

 Sita, jipe kazi au ratiba ngumu

Mara nyingi watu hufanya maasi pale wanapokuwa hawana kazi. Binadamu anapokaa bila kazi, mwili na akili yake hujitafutia kazi nyingine za kufanya ambazo kimsingi siyo nzuri.

Lakini akijiwekea ratiba ngumu, hatopata nafasi ya kulewa, kufanya zinaa, kusengenya, kutumia dawa za kulevya na kadhalika. Hivyo, hakikisha unajiwekea ratiba ngumu itakayokuchosha ili usipate muda na nguvu za kufanya mambo ambayo si mazuri.

Saba, jikumbushe faida za kuacha maasi

Kuacha maasi kuna faida kubwa kwa muumini, ikiwamo kuhuisha imani na kumfanya mtu kuwa mchamungu. Lakini ifahamike kuwa, uchamungu si kuzidisha mema tu, bali pia kuepukana na maasi na kudumu katika kufanya mambo ya kheri.

Nane, epuka marafiki wabaya

Kudumu katika uongofu si jambo rahisi, linahitaji mtu mwema wa kukusaidia, la sivyo shetani atachukua nafasi yake. Kwa maana hiyo, ukitaka kudumu katika utiifu ni lazima utafute rafiki mwema atakayekuhamasiha kufanya mambo ya kheri. Mtume amesema:

“Mfano wa rafiki mwema na rafiki mbaya ni kama mfano wa muuza misk (mafuta mazuri) na mhunzi (mwenye kupuliza moto). Muuza misk, ima atakufukiza harufu nzuri au kununua kutoka kwake, na ima utafurahia harufu nzuri kwake. Na mhunzi, ima atachoma nguo zako au utapata harufu mbaya kutoka kwake.” [Bukhari na Muslim].

Katika ufafanuzi wake kuhusu hadithi hii, Imamu Nnawawi (Allah amrehemu) amesema:

“Mtume alilinganisha rafiki mzuri na muuza misk kwa sababu, mtu anayeshikamana na rafiki mzuri mwenye tabia ya upole na elimu, atapata faida kutoka kwake.”

Tisa, tafuta msaada na ushauri

Mbinu nyingine inayoweza kukusaidia kuacha maasi ni kutafuta msaada wa ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kama vile Masheikh, viongozi wa dini, wazazi, wataalamu wa ushauri na kadhalika.

Hitimisho

Kwa hakika kuacha maasi kunawezekana ikiwa mtu atafanya maamuzi na kuweka mipango na mikakati sahihi. Kwa kutumia mbinu nilizozieleza hapo juu, naamini kwa uwezo wa Allah utaweza kuyakabili maasi

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close