4. Darasa La Wiki

Matamanio ya nafsi yanavyosababisha uasi

Ibada ni asili ya mwanadamu kama anavyosema Allah ‘Azza Wajallah’ katika aya mashuhuri: “Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu.” (Qur’an, 51:56). Lakini kwa sababu ya kuwapo vita baina ya haki na batili na mivutano mikubwa baina ya kambi mbili hizi kunapelekea wakati mwingine mizani kutetereka na mambo kuharibika hasa pale nguvu ya kishetani ya batili inapoonekana kushika hatamu katika jamii.

Hali hii inadhihirika wazi pale tunapoangalia masuala mbalimbali likiwamo la watu kudumu katika maasi, ambayo msingi wake ni kufuata matamanio ya kupita na starehe za muda.

Jamii inayopigia upatu au kuunga mkono masuala ya pumbao na tamaa za nafsi ni jamii ya watu wajinga, na kupitia ujinga wao huamini kuwa wataendelea kuwapo ulimwenguni. Ama jamii yenye watu wanaojitambua huwa hawashughulishwi na kufuata matamanio kwa sababu wanafahamu huo.ni mtego anaoutumia shetani (Iblis) katika kuwanasa wanadamu. Aidha, kufuata

matamanio ni jambo linalotia upofu na kuwafanya watu waiache haki na njia (dini) sahihi. Qur’ an Tukufu imejaa mifano mingi ya watu waliokuwa wanafuata matamanio yao na kupelekea kungamizwa. Miongoni mwa hao ni watu (kaumu) wa Nabii Lut (amani ya Allah imshukie) ambao waliangamizwa kwa kosa la liwati, yani wanaume kujamiiana wenyewe kwa wenyewe na kuacha wanawake ambao ni twahara kwao kindoa.

Mfano mwingine ni watu wa Nabii Shuaib (amani ya Allah imshukie) walioangamizwa kwa kosa la kupunja katika vipimo na mizani. Jamii hizi na nyingine nyingi ziliangamizwa kwa baada ya kushindwa kutanabahi hadi pale kutamani kulipokuwa ni sehemu ya maisha yao.

Hii inathibitisha kuwa uasi ni jambo baya na lenye madhara kwa jamii nzima. Mwenyezi Mungu ameweka mipaka na anataka tusiichupe kwani licha ya sharia zake kuwafikiana na mahitaji ya binadamu, sharia hizo hazitegemei shauku na matamanio ya kibinadamu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na lau kuwa haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.” (Qur’nan, 23:71).

Vile vile Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Watazuka watu katika umma wangu ambao watakuwa wamejaa matamanio kama ugonjwa wa kuambukizwa na mnyama unavyozagaa mwili mzima na kuathiri mishipa na viungo vyote.” (Abu Daud).

Kwa kuzingatia hayo, Muislamu anatakiwa ajisalimishe katika matakwa ya Allah Muumba na Mtume wake. Hilo ni jambo rahisi mno kwa waumini hasa ikizingaziwa kuwa asili ya mwanadamu ni kupendelea kheri na kuchukia maovu (Nafsi zimeumbwa kupendelea kheri).

Vyovyote iwavyo, kufuata matamanio ni kwenda kinyume na fitra (maumbile ya mwanadamu) na ndio maana kunaleta madhara na maangamizo. Mitume na Manabii (Amani iwe juu yao) waliletwa ulimwenguni kwa sababu moja kubwa, nayo ni kuwatoa watu katika ibada ya matamanio na kuwapeleka kwenye ibada ya Allah, kuamini upweke wake, kutekeleza amri zake na kujiepusha na makatazo yake.

Hivyo Muislamu fanya hima urudi katika fitra sahihi na jiepushe na kufuata matamanio. Tambua kila starehe ina mwisho wake, na kila neema ni yenye kupita (haitodumu). Dunia hii uliyopo sasa ni mfano wa kivuli chako; ukisimama husimama, na ukikifuata hukukimbia. Ikiwa walijua hilo vipi unafurahia umri (maisha) ilihali hujui umebakisha muda gani wa kuishi. Je, wewe ni katika wanaofuata matamanio?

Wanazuoni wametaja tabia na wasifu wa watu wenye kufuata matamanio, na wale wanaopendelea zaidi kufuata rai na maoni yao kuliko sharia za Uislamu na amri zake. Moja ya tabia za watu hawa ni kwamba wanadharau, kukejeli na kupinga amri za Uislamu. Baadhi yao wamefikia kiwango cha kuifanyia mzaha Qur’ an, Sunna za Mtume na wale wanaoshikamana na viwili hivyo.

Watu wa matamanio pia wanajulikana kwa tabia yao ya kuwatusi na kuwavunjia heshima Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie), na badala yake huwasifu na kuwatukuza wale wanaokubaliana na matakwa, hamasa na shauku zao.

Katika kulizunguzia hilo, Ibn Rajab (Allah amrehem) anasema: “Madhambi yanafanywa kwa sababu ya kupendelea matamanio zaidi kuliko mapenzi ya Allah na Mtume wake. Uzushi katika dini ni matokeo ya kupendelea matamanio zaidi kuliko sharia za Allah, na hii ni hatari zaidi. Iwapo akili imeshazoeshwa matamanio, kuitoa akili hiyo nje ya matamanio ni kugumu.”

Tabia nyingine ya watu wa matamanio ni kwamba wao hawafuati Sunna za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) katika matendo yao ya ibada, desturi na hali zao. Hawa ndio aliowataja Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’an pale aliposema:

Na katika watu wapo wanaobishana juu ya Allah bila ya elimu, wala uongofu, wala kitabu chenye nuru. Anayegeuza shingo yake ili kupoteza watu waache njia ya Allah. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuungua. (Ataambiwa). Hayo ni kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yako. Na hakika Allah si dhalimu kwa waja.
(22:8-10).

Ukitafakari kwa kina mambo haya utagundua kuwa wale wanaofuata matamanio wamemezwa na ujinga wa kujivunia yale yasiyobaki kwa ajili yao wala wao kubaki kwa ajili ya hayo. Kwa msingi huu, muislamu ana wajibu wa kuzingatia, kukubali na kutekeleza kwa nia na ikhlasi mafundisho ya dini na kuyakimbia matamanio.

Na lau kuwa haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.” (Qur’ an, 23:71).

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close