4. Darasa La Wiki

Malipo ya kumshukuru Allah

Kutoka kwa Abdur–Rahman bin Awf (Allah amridhie) amesimulia kuwa, siku moja Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) alitoka haraka nyumbani kwake na kuelekea kwenye eneo la bustani yake aliyoitoa sadaka. Alipofika eneo hilo alielekea kibla kisha akaporomoka chini na kusujudu sijda ndefu mpaka akadhania kuwa Allah amechukua roho yake.

Abdur–Rahman alimsogelea Mtume akamuona amenyanyua kichwa chake kisha akauliza:

“Ni nani wewe?” Akasema: “Mimi ni Abdur– Rahman bin Awf.” Mtume akamuuliza: “Una jambo gani?” Abdur– Rahman akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Umesujudu sijda ndefu mpaka nikadhania kuwa Allah amechukua roho yako ukiwa ndani ya sijda.” Mtume akasema: “Hakika Jibril amenijia na kunibashiria (kunipa habari njema). Jibril ameniambia, ‘Hakika Allah ‘Azza Wajallah’ amesema, yeyote atakayekuswalia nami nitamswalia, na yeyote atakayekutakia amani (kukutolea salamu), nami nitamtakia amani.’” Basi nikamsujudia Allah sijda ya kumshukuru, [Ahmad].

Mafunzo ya tukio hili: Sijda ya kumshukuru Allah

Allah amewawekea waja wake ibada mbalimbali kwa ajili ya kujikurubisha kwake. Mja anapofikiwa na habari njema au kupata jambo lenye manufaa makubwa katika dini au dunia anatakiwa atangulize shukrani kwa Allah ‘Azza Wajallah’ kwa kufanya ibada.

Na miongoni mwa ibada nyepesi ambazo mja anaweza kuzifanya kila siku, ni sijda ya shukrani ambayo huchukua nafasi kubwa katika ibada za Muislamu. Kusujudu (sijda) ya shukrani ni kielelezo cha utii, heshima na shukrani ya mja kwa Mola wake Mlezi.

Zipo neema nyingi za Allah ambazo watu wanazitumia katika maisha yao ya kila siku. Hata hivyo si watu wote ulimwenguni wanaozishukuru neema za Allah. Tulio wengi tumekuwa tukifurahia neema za Allah kwa njia ya maovu na maasi.

Sharia Tukufu ya Kiislamu inamtaka Muumini kumshukuru Allah baada ya kupata habari njema zenye kufurahisha. Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alisujudu baada ya kupokea habari njema kutoka kwa Jibril (amani ya Allah imshukie). Alisujudu (sijda) ya shukrani kwa sababu alitambua fadhila kubwa anazozipata mtu mwenye kutekeleza sijda hiyo.

Kipi kilimfurahisha Mtume?

Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) alifurahishwa na bishara njema aliyopewa na Malaika Jibril. Jambo la kwanza ambalo Jibril alimbashiria Mtume ni kuinuliwa daraja lake, utajo wake na kupata ujira mkubwa kutokana na kuswaliwa (kutakiwa amani) kwa wingi na watu wa umma wake.

Jambo la pili alilobashiriwa ni wingi wa thawabu ambazo watazipata watu wa umma wake pale watakapokuwa wanamswalia na kumtakia amani. Jambo muhimu la kuzingatia hapa ni kwamba, ujira huu mkubwa unaopatikana kwa mja kumswalia Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) ni lazima uzingatie taratibu alizofundisha Mtume, ikiwamo kutumia matamshi (maneno) yaliyothibiti wakati wake na wakati wa Maswahaba (Allah awaridhie).

Malipo ya kumswalia Mtume

Allah kwa fadhila zake na ukarimu wake humswalia mara kumi yule mwenye kumswalia Mtume mara moja. Hii inaonesha daraja na hadhi kubwa aliyonayo Mtume mbele ya Allah ‘Azza Wajallah’.

Lakini malipo ya kumswalia Mtume hayapatikani kwa watu kucheza na kurukaruka hovyo kwa madai ya kuonesha upendo mkubwa kwa Mtume. Kumswalia Mtume ni ibada ambayo mafundisho yake yamethibiti tangu enzi za wema waliotangulia, enzi ambazo watu walimpenda zaidi Mtume na kufuata muongozo na maelekezo yake.

Wema waliotangulia hawakufanya yale ambayo Waislamu wengi katika zama hizi wanayafanya katika suala zima la kumswalia Mtume.

Umuhimu wa kushukuru

Kuna namna nyingi za kumshukuru Allah ‘Azza Wajallah’ kwa neema mbalimbali alizotutunuku. ‘Al– hamdulillah’ ni neno mashuhuri ambalo hutamkwa na watu wengi wanapofanikisha mambo yao au kuepushwa na majanga na matatizo. Mwenye kutamka neno hili kwa nia thabiti na Ikhlas anakiri kuwa alichokipata au alichokikosa ni neema kutok a kwa Allah ‘Azza Wajallah’.

Njia nyingine ya kuonesha shukrani kwa Allah ni kusujudu sijda ya shukrani. Allah anatuambia:

“Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.” [Qur’an, 14:7].

Kushukuru ni sifa waliyojipamba nayo Mitume na Manabii wa Allah (amani iwashukie wote). Allah amemsifu Nabii Nuhu kwa sifa njema ya kushukuru pale aliposema:

“Enyi kizazi tuliowachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye (Nuhu) alikuwa mja mwenye shukrani.” [Qur’an, 17:3].

Namna ya kusujudu sijda ya shukrani

Sijda ya shukrani haina tofauti na sijda nyingine anazosujudu mtu katika sala. Sijda hii haina dua maalumu. Mtu atasujudu sijda moja kama anavyosujudu sijda ya kisomo na atasoma dhikri kama ile anayoisoma katika sala za faradhi au Sunna

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close