4. Darasa La Wiki

Maadili ya Kiislamu yatuongoze katika kila nyanja ya Maisha

KILA jamii ina maadili. Wakristo, Wahindu, Wapagani, Wamagharibi, Wakomunisti wote wana maadili kutokana na miongozo ya vitabu vyao. Hata wanataaluma mbalimbali nao wana maadili yao. Mfano, kuna maadili ya ualimu, udaktari, unesi, uhandisi, uanahabari, uanasheria na kadhalika.

Dini tukufu ya Kiislamu nayo ina maadili yake. Kinachofanya maadili ya Kiislamu kuwa bora zaidi kuliko maadili mengine yote ni kuwa chanzo chake ni Mwenyezi Mungu, Muumba wetu. Maadili ya Kiislamu yanayotokana na Yule aliyetuumba, anayetujua vema na anayejua kila jambo lenye maslahi na lenye madhara kwetu. Si hivyo tu, maadili ya Kiislamu yanamuongoza Muumini wa dini hii katika kila nyanja ya maisha yake, ikiwemo katika taaluma aliyoichagua.

Hii maana yake ni kuwa wanataaluma wa Kiislamu – wakiwemo waandishi wa habari wa Kiislamu, walimu, madaktari na wahandisi – hawahitaji kutegemea maadili yaliyotungwa na wanadamu katika utekelezaji wa kazi yao, bali wanaweza kupata muongozo bora zaidi na sahihi kutoka kati kavyanzo vya Kiislamu.

Maadili ya Kiislamu

Maadili ya Kiislamu ni tabia, mwenendo wa Kiislamu. Neno tabia kwa Kiarabu ni ‘akhlaq’ (wingi wa khuluq). Inasemwa kuwa neno hilo ‘akhlaq’ lina uhusiano wa karibu na maneno ‘khaaliq’ (Muumba) na ‘makhluq’ (kiumbe). Kwa hiyo, maadili (tabia) yanahusiana na kujenga mahusiano mema kati ya Muumba na viumbe wake na kadhalika kati ya viumbe wenyewe kwa wenyewe.

Sehemu kubwa ya ujumbe wa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa walimwengu, kupitia matendo na maneno yake, ni mafundisho juu maadili mema. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema:

“Na hakika wewe una tabia tukufu.” [Qur’an, 68:4].

Hakuna shaka kuwa maadili ya Kiislamu yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustaarabu wa dunia; na kwa hali ilivyo sasa, maadili hayo ya dini hii tukufu ya Kiislamu ni muhimu mno katika kurejesha tabia na mienendo miema iliyoporomoka mno kote duniani.

Vyanzo vya maadili ya Kiislamu

Maadili mazuri na bora kabisa ya Kiislamu yaliyojaa utu, wema, upendo, kujaliana, kuhurumiana, kuheshimiana, kuhifadhiana na ambayo wanadamu wote tunapaswa kuyafuata yanatokana na Kitabu Kitukufu cha Qur’an na Sunna za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Katika kutujuza msingi wa maadili ya Uislamu, Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an.

“Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka! Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi, wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo.” [Qur’an, 16:90- 91].

Qur’an inasema, mbora miongoni mwa watu ni yule anayeenzi maadili ya Uislamu na kuyalingania kwa wengine ili nao wawe wenye kufuata maadili hayo.

“Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?” [Qur’an, 41:33].

Hebu tuone baadhi ya aya katika Qur’an Tukufu zinazotaja maadii mbalimbali.

“Enyi mlioamini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 49:12].

Katika aya nyingine, Qur’an inasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Mwenyezi Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” [Qur’an, 4:58].

Katika Qur’an [5:8], Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndiyo kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.”

Mtume, mfano na kiigizo chema cha uadilifu

Na inaelezwa katika Qur’an kuwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) alitumwa kufundisha wa kimaadili, kama inavyoelezwa:

“Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” [Qur’an, 21:107].

Kwa mujibu wa aya hiyo, tunaona wazi kuwa maadili ya Kiislamu siyo tu yanaelezewa katika kitabu kitakatifu cha Qur’an bali pia yanafafanuliwa kupitia mienendo na tabia tukufu za Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Kupitia rekodi ya tabia na mwenendo mwema wa Mtume, sisi kama wanadamu tunapata kiigizo bora zaidi. Mtume Muhammad mwenyewe (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye ndiye mwanadamu mwenye tabia njema zaidi amesema:

“Nimetumwa kukamilisha (kufundisha) tabia njema.” [Ahmad].

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema tena: “Wema haupatikani ila kwa tabia njema.” Akasema tena Mtume katika hadith iliyopokelewa na Abu Dardaa: “Hakuna kitu kizito katika mizani ya Muumini siku ya Kiyama kuliko tabia njema. Hakika Allah humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya.” [Tirmidhi].

Na katika hadith iliyopokewa na Abu Huraira. Mtume aliulizwa ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: “Kumcha Allah na tabia njema.” Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni, akasema: “Kinywa (mdomo) na utupu.’[Tirmidhi].

Ukiacha vyanzo hivyo vikuu, pia kuna Ijmaa (makubaliano ya wanazuoni) na Qiyaas, yaani kitendo cha wanazuoni kulitolea hukumu jambo ambalo halijatajwa moja kwa moja katika Qur’an na Sunna kwa kutumia hukumu ya jambo jingine. Kwa kuyajua haya, shime Waislamu tujitahidi kurejea na kuishi katika maadili ya Uislamu, maadili bora kabisa ambayo yatatengeneza maisha yetu ya duniani na Akhera

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close