4. Darasa La Wiki

Kutenda Kheri Ndiyo Ulinganiaji Bora, Na Wenye Tija

Ulinganiaji ni katika matendo matukufu na yaliyo bora zaidi mbele ya Allah Ta’ala. Muislamu atakapoweza kutekeleza ibada hii ipasavyo atakuwa amehuisha kazi ya Mitume na Manabii, nayo ni kuwalingania watu katika njia ya Allah. Allah Mtukufu anawausia waumini juu ya kushikamana na ibada hii tukufu: “Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kheri na wanaoamrisha mema na wanakataza maovu. Na hao ndiyo waliofanikiwa,” (Qur’an, 3:104). Ni wazi kuwa mwanadamu anahitaji ukumbusho wa mara kwa mara ili kuhuisha imani ya kumtambua na kumtii Mola wake. Na juu ya kuwahamasisha watu jambo, wengi huamini lugha ya vitendo kuwa ndiyo yenye nguvu zaidi kuliko maneno. Historia ya Uislamu inathibitisha tabia ya Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) ya kulipa wema kwa ubaya uliotendewa hata kwa wasiokuwa Waislamu pindi walipomkosea. Mwenendo huu ndiyo uliopelekea wengi wao kusilimu. Na katika kufanikisha azma yake, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) aliwaonyesha Maswahaba zake mfano mwema wa tabia nao wakimfuata kwa kumuiga na kufuata nyayo zake kimatendo na kauli. Ajabu ni kwamba Waislamu wengi wa zama hizi hawafahamu kuwa tabia njema ndiyo silaha aliyoitumia Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) katika kuwalingania watu. Qur’an Tukufu inatueleza jinsi tabia na matendo mema ya Mtume vilivyosaidia kuzivuta nyoyo za wasiokuwa Waislamu hadi wakaukubali Uislamu na kuufuata. Hivyo, ili kuleta tija katika kazi ya ulinganiaji yatupasa kujibidiisha na utekelezaji wa matendo mema kabla ya kuwafuata wengine na kuanza kuwalingania. Hii ni kwa sababu lugha ya vitendo ni yenye nguvu zaidi kuliko maneno. Kwa kurejea historia za waja wema (Salafi), tunaweza kupata mifano ya kuigwa katika maana nzima ya tabia na matendo mema. Mtume Muhammad (rehema na amani ya Allah zimshukie) alikuwa mstari wa mbele katika kuwahimiza Maswahaba (radhi za Allah ziwashukie) kushikamana na tabia njema. Allah anamsifu Mtume wake kwa kumuambia: “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndiyo umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia” (Qur’an, 3:159). Aya inajulisha kuwa, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) alikuwa ni mwenye kuwalingania watu katika njia ya Mwenyezi Mungu kupitia matendo mema na lugha nzuri na laini hadi akafanikiwa kupata kundi kubwa la wafuasi. Wengi tunasahau kuwa, kuzidisha matendo mema ya Kiislamu ni bora kuliko mazungumzo ya muda mrefu yahusuyo dini. Haipaswi kwa Muislamu kuwa mlinganiaji hodari wa kuwahimiza watu kufanya mambo mema na huku haoneshi vitendo juu ya kile anachokisema. Katika kutuonya na tabia hiyo, Allah anasema: “Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda?” (Qur’an, 61:2). Ukweli ni kwamba maadili yetu na sheria vimepoteza chanzo pekee cha nguvu yake, na ndiyo maana si ajabu kuwasikia wajuzi wa dini (Masheikh na Maimamu) wakiwaambia watu: “Fuateni maneno yangu msifute vitendo vyangu”. Ni juu ya kila mmoja kuwalingania watu kwa kutumia maneno mazuri, uadilifu, hekima na pia kujipamba na tabia njema. Ndugu Muislamu, tambua ulinganiaji ni jukumu letu, na kila mmoja atahukumiwa kwa kuacha majukumu yake binafsi ya ibada, na majukumu ya kijamii likiwemo la ulinganiaji. Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) amesema: “Mwenye kulingania kheri atapata ujira mfano wa ujira wa wenye kufuata bila kupungua ujira wao chochote, na mwenye kulingania katika upotevu atapata madhambi mfano wa madhambi ya watakaomfuata bila kupunguziwa madhambi yao chochote” (Muslim). Jambo muhimu kwetu ni kushikamana na matendo mema yaliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Anasema Allah Mtukufu: “Ni nani mwenye kauli nzuri kuliko yule mwenye kulingania kwa Allah na akafanya matendo mema na akasema mimi ni katika Waislamu” (Qur’an, 41:33). Yafaa kufahamu, Uislamu ni dini iliyosheheni desturi zinazokubaliana na akili na kumpa mtu uongofu. Pia ni dini inayobeba maendeleo yanayofaa kwa hali, mahala na zama zote kutokana na Sharia zake kukidhi hali na mahitaji ya jamii na katika nyanja zote. Ili kufikia malengo hatuna budi kuwalingania watu kupitia matendo yetu mema, na kwa kufanya hivyo ndiyo tutakuwa walinganiaji bora. Tumuombe Allah atuongoze katika njia iliyonyooka, atuweke mbali na upotovu, na pia akubali na kuyaridhia matendo yetu Siku ya Kiyama.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close