4. Darasa La Wiki

Kunufaisha watu ni sehemu ya ibada

Manufaa ya wengi ni mambo yenye manufaa makubwa kwa jamii. Mfano wa mambo hayo ni kuchimba kisima, kujenga msikiti na kujenga/ kukarabati barabara. Mwenye kufanya mambo haya, atapata malipo (thawabu) mema kutoka kwa Allah lakini pia atainufaisha jamii kwa kiwango kikubwa.

Jukumu moja kubwa la wanadamu kwa Muumba wao ni kuhakikisha wanamuabudu yeye pasina kumshirikisha na chochote. Hilo limebainishwa wazi na aya ya 56 katika Surat Adh–Dhaariyat pale Mwenyezi Mungu anaposema:

“Na sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.” [Qur’an, 51:56].

Katika kutekeleza jukumu hili, ni lazima kwanza tuelewe maana ya ibada kwa undani wake. Hii itatusaidia kuitumia misimu ya kheri katika kufanya ibada zilizoamrishwa na Allah, ambazo kimsingi ndiyo lengo la kuwapo kwetu hapa duniani.

Wanazuoni wa Kiislamu wametufahamisha maana halisi ya ibada kwa aina zake zote. Mmoja wa wanazuoni hao, Shaikhul Islami Ibnu Taymiya (Allah amrehemu) ameifafanua ibada kwa kusema:

“Ibada ni jina lililokusanya kila analolipenda MwenyeziMungu na kuliridhia katika kauli na matendo ya siri na ya dhahiri.”

Kwa maana hiyo, kila jambo ambalo Allah ametuamrisha kulitenda ni ibada. Ama matendo ya kawaida yaliyoruhusiwa na sheria kama vile kula, kunywa na kuvaa yatahesabiwa kuwa ni ibada ikiwa mtu atayafanya kwa nia safi na ikhlas.

Sisi Waislamu tuna mambo mengi ya kufanya ambayo yanaweza kutuongezea uzito katika mizani yetu ya mambo mema Siku ya Kiyama.

Ukiacha ibada tulizofaradhishiwa na Mola wetu kuzitekeleza ikiwamo sala, zaka, funga, hijja na nyinginezo, yapo matendo mengi ambayo tunaweza kuyafanya na katanua wigo wa kumuabudu Allah Mtukufu hata tukiwa katika harakati za maisha yetu ya kila siku.

Lakini pia tunaweza katanua wigo wa kumuabudu Allah kwa kuwasaidia wajane, yatima, kuwazuru wagonjwa, kuhudhuria mazishi, kuamrisha mema na kukataza maovu, kujibu salamu, na kadhalika.

Kuwanufaisha watu

Miongoni mwa mambo ambayo tunatakiwa kuyafanya katika maisha yetu ya kila siku ni kuwanufaisha watu. Na manufaa tunayoyazungumzia hapa yamegawika sehemu kuu mbili, ambazo ni; mosi, manufaa binafsi na pili manufaa ya wengi.

Manufaa binafsi

Haya ni mambo yanayomnufaisha mhusika yeye mwenyewe na si mtu mwingine. Mathalan, mtu anapotekeleza ibada ya sala, funga, zaka au hijja, thawabu zinazopatikana kutokana na ibada hizo zinamhusu yeye mwenyewe, na hakuna yeyote awezaye kunufaika na sala au funga ya mtu huyo.

Manufaa ya wengi

Haya ni mambo yenye manufaa makubwa kwa jamii. Mfano wa mambo hayo ni kuchimba kisima, kujenga msikiti na kujenga/ kukarabati barabara. Mwenye kufanya mambo haya, atapata malipo (thawabu) mema kutoka kwa Allah lakini pia atainufaisha jamii kwa kiwango kikubwa.

Aina hii ya manufaa (manufaa ya wengi) ina nafasi kubwa katika maisha ya kijamii na ni eneo pana ambalo Muislamu anaweza kulitumia katika kumuabudu Allah na kufikia malengo ya ibada.

Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) ametuambia: “Yeyote atakayemtatulia Muumini shida miongoni mwa shida za kilimwengu, Allah atamtatulia shida katika shida za Siku ya Kiyama. Na yeyote atakayemfariji Muislamu kwa tatizo, Allah atamuondoshea uzito miongoni mwa mazito ya Siku ya Kiyama. Na atakayemsitiri Muislamu, naye atasitiriwa na Allah Siku ya Kiyama.” [Bukhari na Muslim].

Na imeelezwa kwamba, mtu anayepuuza haki za baadhi ya makundi katika jamii ni sawa na mtu anayeikanusha Siku ya Malipo (Kiyama).

Allah alimuuliza Mtume wake (rehema za Allah na amani zimfikie):

“Je, umemuona yule anayekadhibisha dini (asiyeamini malipo ya Akhera)? Huyu ni yule anayemnyanyasa yatima, na wala hahimizi kuwalisha masikini.” [Qur’an, 107:1–3].

Hawa (masikini na yatima) ni watu wanaohitaji msaada na uangalizi katika maisha yao, na yeyote anayewadhulumu au kuwapuuza bila shaka atapata adhabu chungu Siku ya Kiyama.

Kupata upendo wa Allah

Mtume amesema: “Mtu mwenye kupendwa zaidi na Allah ni yule mwenye kufanya wema na kuwanufaisha zaidi watu.” [Ibnu Abidduniya].

Dini Tukufu ya Uislamu imekokoteza na kuusia mno kusaidiana katika mambo ya kheri, hivyo yatupasa kufanyia kazi kauli ya Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) aliposema:

“Watu wanaopendwa zaidi na Allah ni wale wenye manufaa kati yao, na matendo yapendezayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni furaha unayoingiza katika moyo wa Muislamu, au kumuondolea matatizo, au kumlipia deni, au kumuondoshea njaa…” [Twabaraniy].

Kupitia hadith hizi tunagundua kuwa, Muislamu ana mambo mengi ambayo akiyafanya yanaweza kumuingiza peponi. Imethibiti katika mapokeo sahihi kwamba mwanamke kahaba alimkuta mbwa akihaha (kwa kiu) karibu na kisima. Alipoona anakaribia kufa kwa kiu, alivua kiatu chake akakifunga kwenye shungi lake akamchotea maji na kumnywesha. Allah akamsamehe mwanamke huyo madhambi yake. Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) akisema:

“Mwanamke fulani aliadhibiwa kwa sababu alimfungia paka hadi akafa kwa njaa. (Mwanamke huyo) aliingizwa motoni (kwa sababu) alipomfungia (paka ndani) hakumpa chakula, wala hakumnywesha maji, wala hakumwacha aende akale wadudu ardhini.” [Bukhari na Muslim].

Kutokana na hadith hii, yafaa kutambua kuwa dunia ni shamba la kupandia mazao ya Akhera, na bila shaka shamba hili litastawi na kutoa mazao bora kwa kupatikana hima ya kuwasaidia viumbe wa Allah. Ni kwa sababu hiyo, Uislamu unatuhimiza kuwafanyia watu hisani ya kadiri ya uwezo wetu ili kupata fadhila za Allah ‘Azza Wajallah.’

Allah ametuamrisha tushikamane na ibada na wakati huohuo tufanye mambo ya kheri pale anaposema:

“Enyi mlioamini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema ili mfanikiwe.” [Qur’an, 22:77].

Ni vema tukaitazama jamii kwa mtazamo huu ili tutumie fursa zilizopo katika kujikurubisha kwa Allah.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close