4. Darasa La Wiki

Ibada zinalingania umoja na kupinga faraka

Uislamu umeweka mfumo wa ibada mbalimbali kwa lengo la kuzitakasa nafsi na roho kutokamana na uchafu uovu. Mfumo wa ibada pia humpandisha mtu mpaka afikiye kwenye daraja za juu za utimamu wa kiutu na hatimaye awe kama taa inayowaangazia watu njia na aweze kuishi na jamii yake kwa usalam na amani.

Kadhalika, mfumo wa ibada pia humsukuma mja afanye juhudi kubwa katika kuwaita watu katika umoja, kuonya dhidi ya migawanyiko na kupinga faraka. Ukiiangalia falsafa ya ibada katika Uislamu, utaona inasisitiza na kutuelekeza katika maana hizo.


Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Kila kitu kina nguzo, na nguzo ya dini ni sala, na nguzo ya sala ni unyenyekevu.”

Ibada ya sala
Tuchukue mfano wa sala. Sala ina athari kubwa katika kuwalingania watu katika umoja na hili linajitokeza pale Waislamu wanaposimama kwenye safu zilizoungana, ambapo habaguliwi wala hajikwezi mtu dhidi ya mwenzake. Aidha, katika sala, hatujali tofauti za jinsi, na hadhi. Katika kutilia nguvu suala hili la umoja kati ya Waislamu, Uislamu umeweka sharia ya sala ya jamaa ili Muislamu aweze kujumuika na Waislamu wenzake na hatimaye umoja na mshikamano uweze kupatikana baina yao.

Vilevile, Sunna za Mtume nazo zimekuja kuhimiza sana umoja, ikiwemo mfano neno la Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Kila kitu kina nguzo, na nguzo ya dini ni sala, na nguzo ya sala ni unyenyekevu.”

Siku moja, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), aliitaja sala, na akasema: “Mtu atakayeihifadhi sala, sala itakuwa nuru, hoja, na mtetezi Siku ya Kiyama. Na mtu asiyeihifadhi sala, sala haitokuwa nuru kwake wala hoja, wala nusura Siku ya Kiyama; na katika Siku ya Kiyama atakuwa pamoja na Qarun, Firauni, Hamana, na Ubeya bin Khalaf.”

Kwa kuwa ibada mbalimbali katika Uislamu, licha ya kutofautiana katika utekelezaji wake, zina athari kubwa kwenye mfumo na mwenendo wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla; basi ibada ya sala, kutokana na umuhimu wake, ina athari kubwa zaidi. Sala hukata mizizi ya roho mbaya kwenye nafsi, na kustawisha mizizi ya roho nzuri. Sala huhimiza matendo mema, na humzuwia mtu dhidi ya matendo maovu. Vilevile, sala huamsha hisia za huruma na upendo.

Ni kwa msingi huo ndiyo maana sala ikawa ibada ya sala hurudiwa mara nyingi, na kushirikisha kundi kubwa la watu, na wote wanatakiwa wasali kwa namna inayotakiwa. Kwa kujipamba na maadili na sifa hizo tulizozitaja ambazo ni athari ya sala, familia hujikuta zikiambukizwa tabia na sifa nzuri, na hatimaye jamii nzima kujikuta ikiwa imeshikamana na kuwa na mrengo na hatima moja, kimaadili, kidesturi, kihisia, na kadhalika katika machungu, matumaini.

Ni kwa kujipamba na sala ndio utakuta mja mwenye nguvu anamsaidia dhaifu, na mkwasi anamsaidia fukara, mkubwa anamheshimu mdogo, na wakubwa wanawahurumia wadogo. Tabia hizi ndio zinazodhihirisha muundo unaotakiwa na Qur’an: “Hakika Waumini ni ndugu.” [Qur’an 49:10].

Kama ibada ya sala ndiyo inayotuibulia maadli haya, bila shaka kuitekeleza kwa jamaa kunaongeza wigo wa faida kwenye nafsi na hivyo kuweza kuidhibiti akili na moyo kuelekea katika utii wa Allah.

Unauonaje mjumuiko huu wa sala ya jamaa, unaokusanya waja waliogawanyika, si katika jambo jingine bali kumuabudu Mwenyezi Mungu, huku wakiwa wamejipanga na kunyoosha mistari yao mbele ya Muumba wao, wakitenda harakati zao kwa mpangilio, wote wakiwa wameachana na ubaguzi wa kutengenezwa, na kuzirarua tofauti mbalimbali.

Utaona tajiri anasimama pembezoni mwa fakiri, mwenye nguvu pembeni mwa mnyonge, mtawala pembeni ya mtawaliwa – wote wakiwa wanamtukuza Mwenyezi Mungu, na hawana wakitakacho isipokuwa radhi za Allah. Nyuso zao zinapomoka ardhini kumsujudia Allah, na migongo na shingo zao zinainama kwa kumnyenyekea Allah. Hawana wanayemuangalia wala wanachokitafuta isipokuwa radhi za Allah. Hawaitikii isipokuwa wito wa Allah, na wameizingira meza ya ibada ya Allah, wakizitibu nafsi zao na hadaa za dunia, maovu, na aibu za dunia.


Nguzo ya zaka, ni kati ya mihimili muhimu ya jamii ya Kiislamu, iwapo italindwa, kwani huduma ya zaka huunganisha kati ya tabaka la mafukara na matajiri na pia huwafanya matajiri kuwa na huruma kwa mafukara

Kwa hakika, mkusanyiko wa kiroho wa aina hii unastahili zaidi kuziunganisha roho kabla ya viwiliwili. Ibada ya sala huwafanya watu wawe na hisia moja, moyo wa kuhurumiana, na kujikuta mvuke wa imani unafuka na kuondosha maradhi ya choyo, chuki, na mkondo wa upendo kutawala, na kutokomeza chuki na bughudha.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amezibainisha fadhila kubwa zinazopatikana kwenye ibada ya sala, aliposema: “Sala ya jamaa inaizidi sala ya mmoja wenu, kwa daraja 25.”

Ibada ya zaka
Kuna pia ibada ya zaka ambayo nayo inawalingania watu katika umoja na kupiga vita faraka. zaka ni mfumo wa kifedha wa kijamii, lakini pia ni miongoni mwa ibada kuu zinazoingiza uchamungu kwenye moyo wa mja, na kumuandaa awe mja mtakasifu kwa Mola wake, na raia mwema kwenye jamii yake. Kutoa zaka hakutofautiani na kusimamisha sala, zaka ni kati ya ibada zinazotekelezwa na Waumini na wachamungu. Mwenyezi Mungu amewasifu watoa zaka katika Qur’an kwa kusema: “Na ambao wanatoa Zaka.” [23:4].

Nguzo ya zaka, ni kati ya mihimili muhimu ya jamii ya Kiislamu, iwapo italindwa, kwani huduma ya zaka huunganisha kati ya tabaka la mafukara na matajiri na pia huwafanya matajiri kuwa na huruma kwa mafukara. Huruma hii ya walionacho kwa wasio nacho inachagiza kutenda kutenda wema. Kadhalika, zaka huwafanya watu wawe na huruma kwa mafukara, na hatimaye huleta upendo, kuheshimiana na kujaliana.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close