4. Darasa La Wiki

Huruma ya Allah kwa viumbe wake

Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Allah alipomzamisha Firauni baharini, Firauni alisema, ‘Nimeamini kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila yule waliyemwamini wana wa Israil.’”

Malaika Jibril (amani imshukie) akamwambia: “Ewe Muhammad! Lau ungeona namna nilivyoshindilia udongo kinywani mwa Firauni kwa kuchelea asije kusema kitu kitachofanya Allah amrehemu!” [Tirmidhi].

Na imepokewa katika riwaya nyingine kwamba, Jibril alishindilia udongo wa baharini kwenye kinywa cha Firauni kwa kuchelea asije kusema ‘Laa Ilaaha Illa Allah’, tamko ambalo lingepelekea kupata huruma ya Allah. [Tirmidhi]. Hakika Jibril anatambua jinsi huruma ya Allah inavyoweza kumfikia mtu yeyote, ndiyo maana akashindilia udongo kwenye kinywa cha Firauni ili kuondoa uwezekano wa kudirikiwa na rehema za Allah.

Mafunzo ya tukio Tukio hili linatufundisha kuwa kuchupa mipaka katika kumuasi Allah ni jambo linalochukiwa na Malaika. Firauni ni miongoni mwa watu waliokubuhu na kufurutu ada kutokana na hadhi (cheo) na uwezo wa kimali aliyokuwa nao, lakini hatimaye aliangamizwa.

Qur’an Tukufu imemzungumzia Firauni kama mfalme muovu aliyewaamrisha watu wamuabudu yeye badala ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Firauni alikuwa mfalme mwenye kiburi na kujikweza kwa sifa asizokuwa nazo.

Huyu (Firauni) alijiita mungu na akawataka watu wote wamtii na kumnyenyekea yeye. Hakika watu wengi walifuata amri zake kwa kuogopea kuuawa. Allah anasimulia harakati alizozifanya mtawala huyu wa Misri ya kale kwa kusema:

“Basi (Musa) akamuonyesha (Firauni) aya (miujiza, ishara) kubwa kabisa. Lakini akakadhibisha, na akaasi. Kisha akageuka nyuma na kufanya juhudi (kukanusha haki). Akakusanya watu kisha akanadi. Akasema, ‘Mimi ndiye mola wenu Mlezi mkuu.’” [Qur’an, 79:20–24).

 “Na Firauni akanadi kwa watu wake, akasema: “Enyi watu wangu! Kwani ufalme wa Misri si wangu! Na hii mito inapita chini yangu? Je, hamuoni? Au mimi si bora kuliko huyu (Musa) ambaye ni dhalili na wala hawezi kujieleza waziwazi.” [Qur’an, 43:51–52].

Kiburi cha Firauni

Qur’an Tukufu imeelezea kwa undani kisa cha Firauni, kiongozi dhalimu aliyewadhulumu watu wake na kumzuia Nabii Musa (amani ya Allah iwe juu yake) kuwalingania watu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu.

Mwenendo huu wa Firauni ulimchukiza sana Malaika Jibril (amani imshukie). Jibril hakutaka Firauni apate r e h e m a ya Allah k w a sabab u alikubuhu katika kumuasi Allah ‘Azza Wajallah’. Kadhalika, Nabii Musa (amani ya Allah imshukie) alimuomba Allah aufunge moyo wa Firauni na jeshi lake mpaka pale watakapokumbana na adhabu yenye machungu.

Nabii Musa alisema kumwambia Allah: “Mola wetu Mlezi! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali katika maisha ya dunia. Hivyo wanawapoteza watu na njia yako. Mola wetu Mlezi, zifutilie mbali mali zao na zifunge nyoyo zao wasiamini mpaka waione adhabu chungu. Allah akasema, ‘Maombi yenu yamekubaliwa. Basi simameni sawasawa, wala msifuate njia za wale wasiojua.’” [Qur’an, 10:88–89].

Huruma ya Allah

Mwenye kufanya uovu, kisha akajuta na kutubia, Allah humkubalia toba yake na kumsamehe madhambi yake. Allah ameahidi kumsamehe yeyote mwenye kutubia na kufanya mambo mema.

Pamoja na kulitambua hilo, Malaika Jibril alishindilia udongo kwenye kinywa cha Firauni ili asipate wasaa wa kujuta kwa aliyoyatenda na hatimaye kupata rehema za Allah baada ya kumuasi Allah kwa miaka mingi, kuwadhalilisha watu na kuwatesa kwa vipigo na kuwakata viungo.

Jibril alijua kuwa Allah ni mwingi wa kusamehe, hivyo akahisi kuwa anaweza kumsamehe Firauni bila kujali ukubwa na uzito wa madhambi aliyoyafanya. Allah anasema katika Hadithul Qudsy:

“Ewe mwanadamu, hakika wewe kila unapoendelea kuniomba na kunitarajia, nitakusamehe dhambi ulizonazo na wala sijali. Ewe mwanadamu, hata kama madhambi yako yakifika katika mawingu (yatakuwa mengi kiasi cha kufika katika mawingu), kisha ukaniomba msamaha, nitakusamehe.” [Tirmidhi].

Ubora wa Kalimat Tawhid (Laa ilaha illallah)

Laa ilaaha illallah ni maneno yanayopaswa kupewa uzito unaostahili kutokana na umuhimu wake katika maisha ya Muislamu. Asili na maana halisi ya maneno Laa ilaaha illallah ni:

“Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah.”

Laa ilaaha illallah ni maneno yenye fadhila kubwa kutokana na nafasi yake ya kuelezea upweke wa Allah katika Ibada. Ni maneno yenye fadhila kwa yule mwenye kumtaraji Allah Ta’ ala na Siku ya mwisho. Kwa bahati mbaya sana watu wengi wamekuwa wakishindwa kutamka maneno haya wakati wa kufa.

Roho ya mtu inapofika kwenye koo lake, hakuna tena nafasi ya kutubia, kwani wakati huo huwa mgumu zaidi kwa mwenye kutolewa roho. Katika mazingira haya ni dhahiri kwamba mtu atamuamini Allah kwa sababu anaona uhalisia wa kile alichokuwa akielezwa wakati wa uhai wake.

Firauni alikiri kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allah, lakini kuamini huko hakukumfaa chochote. Alipokaribia kufa maji, Allah alimwambia:

“Ala! unaamini sasa ilihali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa mafisadi? Leo tutakuokoa kwa mwili wako ili uwe ishara kwa ajili ya walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na ishara zetu.” [Qur’an, 10:91–92].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close