4. Darasa La Wiki

Hii Ndiyo Tofauti ya Kusali na Kusimamisha Sala

Sala ni nguzo ya pili ya Uislamu baada ya shahada, na ndiyo ibada ya kwanza kuhesabiwa Siku ya Kiyama. Sala ikiwa nzuri (ikikamilika), amali zilizobakia zitakuwa nzuri; na ikiwa mbaya amali zote zitakuwa mbaya. Kimsingi, sala ndiyo kioomatendo ya mja, na Muislamu hana budi kuisimamisha inavyotakiwa.

Ili mtu alipwe ujira wa matendo yake mema Siku ya Kiyama ni lazima awe amekamilisha na kutimiza nguzo ya sala. Kwa mantiki hii ni lazima tuiwajibikie ipasavyo ibada ya sala kwa sababu ndio msingi mkuu wa imani ya Kiislamu. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Hakika baina ya mtu na shirk na kufru, ni kuacha sala.” [Muslim].

Swali la msingi ni je, tunaposali tunatenda ndivyo? Au ndio tunaharibu huku tukijiliwaza na kujipa matumaini kwamba Allah ni Msamehevu na Mwenye huruma hivyo atakubali sala zetu hata kama zina kasoro. Kama unafikiri hivyo basi hujafikiri sawasawa.

Allah Mtukufu anatutaka tumuabudu Yeye kikamilifu kwa ufanisi na weledi.

“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha, wala msife isipokuwa mmekuwa Waislamu.” [Qur’an, 3:102].

Katika aya hii, Waumini wanakumbushwa kumtii na kumuabudu Mwenyezi Mungu kikwelikweli ili walipwe ujira mwema Siku ya Kiyama. Ni katika muktadha huu tunatakiwa kutekeleza ibada ya sala na nyinginezo kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Anachopaswa kufanya kila anayeitwa Muislamu ni kusimamisha sala na si kusali. Kusimamisha sala ni tofauti na kusali. Kusimamisha sala ni kusali kwa kufuata kisawasawa sharti na nguzo zake zote; kunyenyekea na kuihudhurisha nafsi katika sala. Ukiacha jambo moja katika haya utakuwa hujasimamisha sala bali umesali tu.

Hakika amri ya kusali imeambatanishwa na uzuri na kutenda ndivyo. “Allah ni Mzuri hakubali ila kilicho kizuri.” Kwa maana nyingine, haitozingatiwa Siku ya Kiyama kwamba mja alifanya tu matendo ya sala, bali sala zitapekuliwa ili kuthibitisha usahihi wake. Kama hakufanya kwa usahihi, itakuwa kazi bure.

Mtume amesema, siku ya Kiyama Allah atawaambia Malaika wake:

“Zipekueni sala za mja wangu. Je, amezitimiza au amezipunguza?’ Ikiwa zimetimia, itaandikwa kuwa zimetimia. Na ikiwa amekosea sehemu fulani, Allah atawaambia, ‘Muangalieni kama ana sala za sunna mkamilishe kwazo sala zake za faradhi…’” [Abu Daudi na Tirmidhi].

Jambo muhimu la kuzingatiwa katika Hadithi hii ni kwamba, Siku ya Kiyama kutakuwa na upekuzi mkali wa sala ili kuona kama kweli waswaliji walisali au walikuwa wakipiga gema tu, ukiachilia mbali wale walioiacha kabisa.

Abu Huraira (Allah amridhie) amesimulia kwamba, mtu mmoja aliingia msikitini, ambamo Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alikuwa amekaa, akasali rakaa mbili kisha akamwendea Mtume na kumsalimia. Mtume akajibu salamu yake kisha akamuambia:

“Rudi tena ukasali kwani wewe hukusali.”

Yule mtu akarudi, akasali (rakaa mbili) kama alivyofanya awali. Kisha akaja tena kwa Mtume na kurudia kutoa salamu. Mtume akajibu salamu yake na kumumbia:

“Rudi tena ukasali kwani wewe hujasali.” Yule mtu akarudi, akasali (rakaa mbili) kama alivyofanya awali, kisha akaja tena na kurudia kutoa salamu. Mtume akamuitikia kwa mara nyingine kisha akarejea kusema: “Rudi tena ukasali kwani wewe hukusali.” Mtu yule akasema: “Naapa kwa Yule ambaye amekutuma wewe kwa haki. Ewe Mtume wa Allah, sijui kusali vizuri zaidi ya nilivyosali, basi nifundishe.”

Mtume akamwambia: “Ukisimama kwa ajili ya sala, sema, ‘Allahu Akbar’. Halafu soma ambacho kitakujia kwa wepesi katika Qur’an, kisha rukuu mpaka utakapohisi kwamba umetulia katika rukuu yako. Kisha, simama mpaka uwe umesimama wima kisawa sawa. Kisha, sujudu mpaka uwe umetulia katika sijida yako. Kisha kaa mpaka uwe umetulia katika kikazi chako. Kisha sujudu mpaka uwe umetulia katika sijida yako. Na uwe unafanya hivi ndani ya sala yako yote.” [Bukhari na Muslim].

Maelezo ya Hadith

Hadith hii ni sahihi kabisa na imeandikwa takriban katika vitabu vyote mama vya wanazuoni wa Hadith kikiwamo cha Bukhari, Muslim, Abu Daudi, Ibn Majah, Tirmidhiy, Nasaiy na Ahmad. Wanazuoni wengi wanaizingatia Hadith hii kuwa ndiyo msingi wa kubainisha nguzo, sunna na vitenguzi vya sala.

Aidha, Wanazuoni wameifanya Hadith hii waliyoiita ‘Hadith ya jamaa aliyeharibu sala yake,’ kuwa rejea muhimu kila wanapoelezea sifa ya sala inayokubalika.

Hatari ya kusali kwa kudonoadonoa

Katika sunna za Kabliya, baadiya na sala ya Tarewehe katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wengi wetu tunasali kwa haraka sana kiasi cha kushindwa kuutuliza mwili wote sehemu tunapopaswa kufanya hivyo. Baadhi ya Maamuma tunawatangulia Maimamu wetu katika vitendo, ama tunakwenda sambamba nao.

Baadhi ya maimamu wanasoma sura fupi fupi kwa haraka (kama vile Surat Ikhlas) na kuwafanya maamuma (wanaowafuata) washindwe kumaliza kuisoma Suratul Fat–ha. Hata pale zinaposomwa sura ndefu kwa lengo la kumaliza juzuu, zinasomwa haraka haraka bila ya adabu.

Kifupi ni kuwa, katika sala nyingi za Tarawehe hakuna unyenyekevu isipokuwa tunadokoadokoa tu nguzo mbalimbali katika sala nzima. Kudokoadokoa sala ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo sharia na nguzo za sala, kutokuwa na khushui (unyenyekevu), kutokujituliza katika sala mahala inapopasa, kutokukamilisha visomo, kutozingatia tunachosema, na kadhalika.

Ikiwa tunataraji kupata radhi za Allah, yatupasa tutekeleze ibada ya sala kama alivyoelekeza Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) katika Hadith tuliyoitaja hapo juu.

Tathmini ya sala zetu

Tumekwishaona madhara yatokanayo na kupuuza sala, hivyo ni jukumu letu kufanya tathmini ya kina katika sala zetu zote ziwe za faradhi ama za sunna. Tukusudie/ tuazimie kuzitekeleza sala ipasavyo ili tuweze kupata mafanikio yake, vinginevyo, tutakuwa tunajiandalia maangamivu na hasara hapa duniani, kaburini na kesho Akhera.

Sanjari na hilo, tunapaswa pia kuzipima sala zetu kama zinatuepusha na mambo machafu au la. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an:

“Bila shaka sala (ikisaliwa vilivyo) humzuilia (huyo mwenye kusali na) mambo machafu na maovu, na kwa yakini ndani ya sala kuna kumkumbuka Mwenyezi Mungu kuliko kukubwa kabisa, na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.” [Qur’an, 29:45].

Pamoja na kasoro nyingine, kosa kubwa tunalolifanya wengi wetu ni kusali harakaharaka (chapuchapu) na kukosa utulivu (twumaanina) wakati wa kufanya matendo ya sala. Tulio wengi hatuzingatii nguzo, sunna na yale yanayoweza kuharibu sala.

Tukiizingatia Hadith tuliyoitaja hapo juu, tunaona jinsi Mtume alivyochukulia hatua uchafuzi wa ibada alioufanya kijana aliyekwenda kumsalimia. Hii ni dalili kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa makini katika kufuatilia na kuhakikisha usahihi wa ibada za wafuasi wake, jambo ambalo katika misikiti yetu limekosekana.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close