4. Darasa La Wiki

Hekima, mafunzo ya kutajwa wanyama ndani ya Qur’an

Allah Aliyetukuka anaisifu Qur’an katika Surat Al Aaraf kuwa ni kitabu ambacho ndani yake kumepambanuliwa elimu na pia ni uongofu na rehma kwa wenye kuamini. Elimu ya Qur’an ipo katika mfumo wa sheria na mifano mbalimbali.

Aina mbili za aya ndani ya Qur’an Katika Qur’an, Surat Imran [3:7], Allah anaeleza kuwa aya za Qur’an zipo aina mbili.

Kwanza: Muhkamat yaani zilizobeba hukumu (sheria) ikiwemo maamrisho na makatazo. Hizi ndiyo aya Mama za Kitabu au zenye kutiliwa mkazo zaidi kwa sababu sheria ndiyo msingi wa Uislamu wenyewe. Katika Qur’an zipo sheria za ndoa, mirathi, biashara na uchumi, ibada mbalimbali na kadhalika.

Kundi la pili la aya ni Mutashabihat yaani zilizobeba mifano. Katika mifano hiyo tuliyopigiwa kuna ya wanyama, wadudu, visa vya Mitume na Manabii, visa vya watu wema, visa vya watu wabaya na kadhalika.

Wanyama ndani ya Qur’an

Mwenyezi Mungu ametaja wanyama na wadudu aina mbalimbali ndani ya Qur’an. Sura tano zimepewa majina ya wanyama na wadudu zikiwemo ng’ombe (Al-Baqara), (Al-ʾanʾʾm), tembo(Al-Fil), buibui (Al-Ankboot), sisimizi (An-Naml) na nyuki (An-Nahl).

Ni vyema kuwajua wanyama hao lakini pia kuelewa na kuzingatia ujumbe ambao Mwenyezi anatufikishia kupitia kwao. Kutajwa kwa wadudu na wanyama katika Qur’an kunaonesha umuhimu wao katika dunia hii. Wadudu na wanyama hawa wanatekeleza majukumu ambayo binadamu hajaweza kuyatekeleza. Pia, matendo ya wanyama hawa ni ukumbusho na mazingatio kwetu.

Mifano ya wanyama waliotajwa

Katika Surat Al–Baqara, kuna kisa cha ng’ombe na vilevile Nabii Musa na watu wake. Tukio hilo lina mafunzo mengi. Watu wa Musa waliagizwa wachinje ng’ombe tu, lakini wao wakafanya maisha kuwa magumu kwa kuleta utatanishi. Watu wa Musa waliuliza maswali yasiyo na msingi na kukuza mambo tu.

Funzo katika kisa hiki ni kuwa, tusiulize au tusifuatilie masuala yasiyo na msingi kwani tutafanya mambo yetu kuwa magumu na yatatupotezea muda. Pia, kwa kuuliza maswali mengi tunajiwekea vizuizi na hivyo tunaweza kupata hasara na kuonekana wajinga.

Mfano mwingine wa mafunzo yatokanayo na kisa cha mnyama upo katika Surat al-Kahf [22:18] kinachomtaja mbwa, mbwa mwitu katika Surat Yusuf, ngamia katika Surat al-Ghashiya na nyengine kadhaa. Pia, kuna viumbe wa baharini waliotajwa kama samaki wa Nabii Yunus katika Surat Yunus na samaki wa Nabii Musa katika Surat al-Kahf.

Mfano wa mbu

Kwa upande wa wadudu, nao wametajwa kwa wingi katika Qur’an Tukufu. Surat al-Baqara [2:26] pale Mwenyezi Mungu anapomuelezea mbu kwa aina yake.

Katika aya hiyo, Allah Aliyetukuka anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walioamini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale waliokufuru husema, ‘Ni nini analokusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu?’ Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu.”

Katika dunia ya leo, mbu ana nafasi ipi katika uchumi wa nchi? Analeta malaria na hivyo kupelekea mwanadamu kulazimika kutengeza dawa na vyandarua? Vipi pia kuhusu balaa analosababisha na athari yake kwa uchumi?

Allah anatufunza tusipuuze vitu vidogo vidogo. Unamuona mbu mdogo lakini kumbe ana umuhimu mkubwa. Allah anajifaharisha na mdudu huyu mbu na kuthamini kiumbe chake. Hiyo ni heshima ya aina yake sana.

Leo hii tunazungumzia haki za binadamu tamko lililosainiwa mwaka 1948, lakini karne ya saba Allah alizungumza habari ya haki ya viumbe kwa kumthamini mbu tu. Ajabu ni kuwa, sisi binadamu wala hatuheshimiani na wala hatuheshimu haki za wengine.

Mfano wa nzi

Mfano mwingine ni wa nzi katika Surat al-Hajj aya ya 73. Allah anasema: “Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.”

Aya hiyo inataja kuwa, sisi binadamu hatuna hata uwezo wa kuumba nzi hata kama tutajumuika wote au kundi. Pia Allah anasema, huyo nzi akichukua kitu chetu au mfano kunusa chakula hatuwezi hata kumkamata!

Allah anatufunza kuhusu uwezo, uumbaji na ukubwa wake na kutuonesha kuwa nzi si wa kumpuuza kabisa. Pia, Mwenyezi Mungu anaonesha hatuna mbio au nguvu za kumzuia au kumkamata nzi kiumbe mdogo tu, licha ya akili zote tulizonazo binadamu.

Pia anaonyesha nzi ana heshima kubwa kwake mpaka anamtumia kutupigia mfano kwetu. Suala linabaki pale pale katika haki za viumbe. Nzi anatumika kwa udogo wake kutoa ujumbe kuwa, tusidharau mambo madogo madogo. Nzi mdogo lakini asidharaulike kabisa.

Leo hii nzi amekuwa chanzo cha magonjwa lukuki na nyenzo ya utafiti siyo tu katika sayansi ya afya na mazingira, bali hata katika uchumi kupitia biashara ya dawa za ugonjwa wa kipindupindu na homa za matumbo. Magonjwa hayo pia yanajadiliwa katika mikutano ya kimataifa.

Mfano wa farasi na punda

Mfano mwengine ni wa farasi mwenye kasi aliyetajwa katika Surah Al-’Adiyat. Farasi huyo mwenye kasi alitumika kwa kazi nyingi ikiwemo usafiri na vitani. Huyu ni mnyama anayehimili mikikimikiki ya vita, njaa na mateso mengine.

Mfano mwengine ni wa punda ambaye ametajwa katika Surat Luqman na kwengineko. Punda anajulikana kuwa ana sauti mbaya zaidi. Katika aya ile tunaambiwa tusipige kelele au kuongea kwa sauti kubwa maana sauti mbaya zaidi ni ile ya punda. Sauti ya mtu anayefanya kelele au kuongea kwa sauti inafananishwa na ile ya punda.

Lakini nini maana ya aya hii? Leo tunazungumza habari ya utunzaji wa mazingira, ikiwemo kupunguza kelele. Qur’an ilielezea habari hii katika karne ya saba. Sio uchafuzi wa aina hii tu wa mazingira, umetajwa pia aina nyingine za uchafuzi wa mazingira ikiwemo wa vyanzo vya maji, hewa na mmomonyoko wa ardhi.

Punda huyo huyo pia anatajwa ndani ya Qur’an katika usafiri na uchukuzi wa mizigo. Kwa upande mwingine, anatolewa mfano wa mtu aliyebeba kitu cha thamani (mathalan vitabu vya Allah kama Taurat au Qur’an) lakini hajui thamani yake.

Sisimizi

Ametajwa pia sisimizi, mdudu mdogo ambaye anafundisha kuhusu kuangalia usalama wa wengine, kazi ambayo aghalabu inamshinda mwanadamu. Jukumu hilo la sisimizi linatajwa katika Surat An-Naml. Mwanadamu, aghalabu, utamkuta atamuingiza mwenzake katika matatizo, lakini sisimizi anawaambia wenzake ingieni katika majumba yenu kwani Suleiman anakuja na jeshi lake. Sisimizi anatoa ujumbe akithamini usalama wake na wa wenzake.

Taarifa hiyo muhimu inafanyiwa kazi haraka sana na wenzake. Je, Leo hii sisi binadamu tunazingatia tukipewa taarifa muhimu za maisha yetu au za usalama wetu, kama ilivyokuwa kwa sisimizi?

Kunguru

Ndege kunguru naye ametajwa katika Qur’an. Ni ndege huyu ambaye alimfunza binadamu kuzika hadi yule mtoto wa Nabii Adam akajiona mjinga sana. Leo hii wengi wetu tumeshindwa kufanya anachofanya kunguru.

Leo hii, sisi binadamu tunawazika watu bila ya utaratibu au hata wakati mwingine tunawatupa kabisa. Wakati mwingine tunawasema vibaya maiti zetu na kususia kushiriki mazishi yao. Tumeshindwa hata na kunguru ? Basi, ni vema tusimdharau mwalimu wetu huyo.

Nyuki

Nyuki naye ni mdudu wa aina yake akitoa ujumbe wa umoj na, kutumia rasilimali vizuri ili kuzalisha na kujenga uchumi, kama Allah anavyotaja:

“Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki, ‘Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayo jenga watu.’” [Qur’an, 16:68].

Asali imekuwa ni bidhaa muhimu sana kama kinywaji hadi kimataifa, lakini pia nyuki anasaidia katika utunzaji wa mazingira. Asali ya nyuki pia ni dawa kubwa ya maradhi lukuki.

Buibui

Wametajwa pia buibui ambao wanatufunza kuhusu usalama binafsi, ubora wa kuunda kitu mwenyewe na kutumia ulichonacho vizuri kwa usahihi. Tizama alivyotumia uwezo wake aliojaaliwa na Allah Ta’ala kujenga nyumba yake!

Hata hivyo, pia, Allah anasema katika Surat Ankabut kuwa nyumba ya buibui ni dhaifu sana. Kwa mujibu wa Allah Ta’ala, anayetegea ulinzi usiokuwa wa Allah ni sawa na ulinzi alionao buibui. Nyumba yake ni dhalili.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close