4. Darasa La Wiki

Hawakuamrishwa ila wamuabudu Mungu Mmoja

Nianze kwa kupingana na methali ya Kiswahili inayosema ‘Hewala si utumwa.’ Mimi naona hewala ni utumwa kwa sababu chimbuko hasa la methali hii ni kuwafanya watu watii matakwa ya ‘wakubwa’ au waajiri wao kwa kutumia maneno mazuri yaliyojaa busara na hekima.


Jambo la msingi na bora ni kujiepusha na maasi, pumbao na mambo mengine ya hovyo ambayo jumla ya malengo yake ni kumtoa mwanadamu katika utu na ustaarabu wa dini

Licha ya kubeba mafunzo muhimu ya kijamii, kwa upande mwingine methali hii pia inalenga kushawishi watu kufuata miongozo na sheria zilizotungwa na wanadamu badala ya sharia tukufu za Mwenyezi Mungu. Sina tatizo na hewala, bali nachelea watu wasijeingia katika utumwa wa kuwaabudu wanadamu wenzao badala ya Mwenyezi Mungu. Nasema hivyo kwa sababu ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake havikuumbwa bure bure tu bali kwa makusudio na malengo maalum.

Ni kwa kuzingatia hilo, Mwenyezi Mungu ameyaegemeza maisha ya mwanadamu katika misingi maalum yenye uhusiano na dhana nzima ya kuabudu, na ambayo ndiyo lengo kuu la kuwapo kwetu hapa ulimwenguni.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mun-gu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike sala, na watoe zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti.” [Qur’ an, 98:5–6].

Kwa mujibu wa Uislamu, ibada ni jambo linalojumuisha kila alipendalo Allah na kuliridhia. Uislamu umekuja na sharia na kanuni madhubuti zinazohusu maisha yote ya mtu binafsi, familia na kiuchumi, kisiasa, kijamii na hata kiutamaduni. Kwa maana nyingine ni kwamba Uislamu si kutekeleza ibada maalumu kama vile sala, funga na hijja bali Uislamu ni kushikamana kikamilifu na itikadi, sharia na muongozo wa Qur’ an na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Hivyo, ni wajibu kila mmoja kuifuata dini ya haki (Uislamu), licha ya kuwepo changamoto za hapa na pale. Mojawapo ya changamoto hizo ni watu kujishughulisha kupita kiasi na mambo yenye mrengo na maslahi ya kidunia.


Na Tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); hofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. na wapashe habari njema wanaosubiri.[Qur’an, 2:155].

Jambo la msingi na bora ni kujiepusha na maasi, pumbao na mambo mengine ya hovyo ambayo jumla ya malengo yake ni kumtoa mwanadamu katika utu na ustaarabu wa dini. Muislamu kujiepusha na mambo yasiyokubaliana na dini ni jihad kubwa katika maisha yake. Kwa maana nyingine inaweza kusemwa, ujumbe wa msingi katika lengo la kutumwa kwa Manabii ni kulingania (watu) kwenye ibada ya Mungu peke yake na kupiga vita ushirikina wa aina zote. Kinachopaswa kufanywa na kila anayeitwa Muislamu ni utiifu mbele ya Allah, na kunyenyekea kuliko bora ni kutii amri za Allah Ta’ala milele sambamba na kupambanua baina ya haki na batili, ukweli na uwongo, na kufanya hivyo ndiyo kuabudu kuliko sawa.

Sababu yake ni kwamba, mwanadamu ni kiumbe aliyetukuzwa na Allah Ta’ala kwa kupewa kipaji na uwezo wa kipekee katika kufikiri jambo linalopelekea kutofautisha ukweli na uongo. Kulingana na hayo, Allah Ta’ala ameahidi siku ya kiyama kumuuliza mwanadamu huyo juu ya kila alichomneemesha.

Kwa kuwa Uislamu ndiyo njia ya haki kwa kila mwenye kutaka uongofu, ni wajibu kwetu kuutekeleza Uislamu kwa vitendo na si kujisifu kwa wema pasipo amali njema. Kwa sababu hiyo, yeyote atakayeshindwa kuufuata Uislamu baada ya kubainishiwa kuwa ni haki, basi atakuwa katika hatari kubwa kabisa siku ya Kiyama. Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema: “Yeyote miongoni mwa Wakristo na Mayahudi atayesikia kuhusu mimi, lakini bila ya kuyakinisha imani yake kwa yale niliyoyaleta na akafa katika hali hiyo, atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.” [Muslim].

Hivyo basi, Muislamu anatakiwa atambue nguzo kuu za utambulisho wa Uislamu wake ambazo ni itikadi, imani, thamani na mtindo wa maisha aliouelekeza Allah Ta’ala kupitia kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Katika hili kila mtu anatakiwa kujihadhari kwa sababu yeyote mwenye kufuata muongozo wa dini isiyokuwa Uislamu atapata hasara duniani na Akhera.

Hakuna kheri kwa yeyote atakayeishi nje ya muongozo wa Uislamu na ndiyo maana Allah aliwatuma Mitume kwa ajili ya kazi moja tu ya kuwalingania watu Tauhiid. Anasema Allah Ta’ala katika Qur’an: “Na bila shaka tulimpeleka Mjumbe kwa kila umma (akawaambie umma wake) muabuduni Mwenyezi Mungu na muepuke (utwaghuti) masanamu.” [Qur’an, 16:36].

Hata hivyo, ni vema tukajua sababu za watu wengi katika zama hizi kuishughulikia zaidi dunia kuliko akhera. Sababu ni wanadamu kukosa subira kwa Allah Ta’ala ambayo ndiyo silaha pekee inayoweza kumuokoa mja kuathiriwa na hamasa za kidunia.

Wapo wanaohalifu ada kwa kuona sharia za dini ni ngumu hivyo kuamua kutumia njia za hujuma katika kupata mafanikio ya kidunia kama vile mali na umaarufu huku wakisahau kuwa Allah anaweza kuwatahini kwa namna atakayopenda. Qur’an inabainisha hilo: “Na Tutakutieni katika msukosuko wa (baadhi ya mambo haya); hofu na njaa na upungufu wa mali na wa watu na wa matunda. na wapashe habari njema wanaosubiri.[Qur’an, 2:155].

Aya hii inathibitisha kwamba muumini yeyote madamu yungali hai duniani ni lazima ataonjwa na Mola wake kwa kumpa mitihani mbalimbali na katika hili hatokuwa na pa kukimbilia. Watu wengi hadi sasa hawajaweza kujenga uhusiano mwema na Mola wao na bado wanaendelea kutukuza miongozo na sheria walizozibuni watu badala ya sharia tukufu za Mwenyezi Mungu. Lini hali hii itakoma? Sijui, tusubiri tuone.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close