4. Darasa La Wiki

Hakika tutaulizwa kwa dhamana tulizopewa

“KiIa mmoja ataulizwa ni vipi ametekeleza majukumu yake ipasavyo. Inawezekana tukashindwa kujibu maswali haya. Kwa hivyo, fanyeni kazi kwa nguvu na maarifa kwa sababu tuna maswali hayo magumu ambayo sisi wanadamu tutashindwa kuyajibu. Mtu makini anapofanya kazi lazima ajiulize je, nimetimiza wajibu wangu ipasavyo? Tukijiuliza maswali haya, naamini tutaendelea kutimiza wajibu wetu.”

Hayo ni maneno ya Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo aliyoyasema siku chache zilizopita wakati wa hafla ya kuapishwa kwa viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais John Magufuli katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Maneno ya Waziri Jafo yananikumbusha kauli ya kiongozi wa umma huu, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) aliyesema:

“Kila mmoja wenu ni mchungaji na ataulizwa kwa alichokichunga… Kiongozi ni mchunga wa wale anaowaongoza na anawajibika kwao…”

Nirejee katika maneno ya Waziri Jafo, ambayo kwa hakika yamejaa busara, hekima, imani, uadilifu na unyenyekevu wa hali juu. Ni maneno machache lakini yaliyobeba uzito usiomithilika hasa kwa viongozi vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Ni wazi kuwa Waziri Jafo hafurahishwi na uwajibikaji wa baadhi ya viongozi katika ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri. Na bila shaka kauli yake inalenga kufuta fikra za baadhi ya watumishi wa umma wanaodhani kuwa kuwahudumia wananchi ni jambo la hisani kwao na siyo wajibu.

Ni jambo la faraja kuona Waziri analisemea hili ingawa pia ni aibu kwa baadhi ya watendaji walio chini yake kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kiasi cha mkuu wao kuyabaini mapungufu yao.

Jamii inahitaji viongozi waadilifu

Uadilifu ni jambo linalopigiwa kelele na watu wengi, wakiwemo viongozi wa Dini na hata wa Serikali. Katika sharia ya Uislamu, muadilifu ni yule ambaye anaishi kwa kufuata maadili, nidhamu na kuchunga haki za wengine.

Hata hivyo utekelezwaji wa dhana ya uadilifu katika jamii yetu umekuwa wa kusuasua kutokana na viongozi wengi kutowajibika ipasavyo katika kusimamia haki, nidhamu na maadili ya wale wanaowaongoza. Viongozi wengi wanadhani kuwa, jukumu hilo linawahusu viongozi wa dini na kwamba wao hawahusiki.

Lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuambia:

“Nyote ni wachungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga. Kiongozi ni mchunga, mume ni mchunga juu ya mkewe, na mke ni mchunga juu ya nyumba ya mumewe na watoto wake; kwa hivyo nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga.” [Bukhari na Muslim].

Hadith inamtaka kila mmoja wetu kutambua kuwa, uongozi ni dhamana, na wala siyo utukufu. Hivyo, itakuwa jambo la kushangaza kwa mtu kudhani kuwa kupatiwa uongozi wa wizara, taasisi, kampuni au shirika ndiyo kibali cha kufanya ufisadi na kutumia wadhifa kwa faida binafsi na wanaomzunguka.

Kwa sababu ya kukosekana uadilifu, leo tunashuhudia watu wengi wakiishi katika hali ya wasiwasi, mashaka na kukosa imani na viongozi wao jambo linalosababisha migogoro na vita katika mataifa mengi ulimwenguni.

Kwa minajili hii, ni wazi ulimwengu wa sasa unahitaji viongozi waadilifu watakaokuwa na hima ya kudhibiti maovu kama vile dhuluma, ubadhirifu, upendeleo, ufisadi, rushwa, ubakaji na kadhalika.

Katika namna ya kukabiliana na kadhia hizi, Allah Ta’ala anawataka viongozi wa kada zote kuhakikisha wanasimamia haki na uadilifu kwa watu wote bila kujali rangi, dini, wadhifa (cheo) au tabaka la mtu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhuluma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka.” [Qur’an, 16:90].

Ikumbukwe kuwa moja ya maswali ambayo kiongozi yeyote ataulizwa ni vipi aliwaongoza wale anaowajibika kwake? Hii inaonesha wazi namna kipengele hichi kilivyo na umuhimu kwetu. Kwa hakika tunahitaji rehema za Allah katika eneo hili ili tuweze kutekeleza jukumu la uongozi kwa uadilifu na uaminifu. Wapo wanaoweza kuuliza na kustajabu vipi Uislamu uzungumzie uongozi, huku si kuchanganya dini na siasa! Watu hawa wamesahau kauli ya Allah Mtukufu aliposema kuwaambia Malaika:

“Hakika Mimi nitaweka katika ardhi Khalifa (Kiongozi).” [Qur’an, 2:30].

Kwa hakika dini yetu hii tukufu haiishii tu kwenye ibada ya sala katika kuta nne za misikiti bali imeangaza nyanja zote za maisha mpaka kwenye uongozi.

Uongozi ni amana

Ifahamike kuwa uongozi ni amana na neema ambayo Mwenyezi Mungu amewatunuku baadhi yetu ili kwayo waweze kutumia vipawa vyao katika kujiweka tayari kukabiliana na mitihani ya Siku ya Kiyama.

Kubwa na muhimu ni kuwatumikia waja wa Mwenyezi Mungu kwa uadilifu na uaminifu. Mwenyezi Mungu anasema:

“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie ilichokitanguliza kwa ajili ya kesho (akhera). Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari ya mnayoyatenda.” [Qur’an, 59:18].

Katika hali ya kawaida, haijuzu kwa mtumishi wa shirika au asasi yoyote ile kupingana na maelekezo halali (yasiyopingana na sheria ya Mwenyezi Mungu) ya mwenye shirika au asasi hiyo, . Kwa hiyo, kiongozi wa serikali ni mwajiriwa wa wananchi, hivyo anawajibika kuwatumikia watu wote na kutatua kero zao bila kujali kabila, rangi, dini, itikadi au hadhi ya mtu.

Na Allah Mtukufu ametoa muongozo na mafundisho yake katika suala zima la uongozi, kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi taifa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close