4. Darasa La Wiki

Fadhila za siku kumi za mwanzo za Dhul-Hijja

Kwa hakika Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi na akajichagulia mbingu ya saba. Pia, akaifanya Makka kuwa mji patakatifu. Vilevile akaumba Pepo na Malaika, na kuifanya Firdaus kuwa ndiyo pepo ya juu zaidi. Muongoni mwa Malaika, Mwenyezi Mungu akamfanyaJibril ndiye Kiongozi wa Malaika.

Upande wa majira, Mwenyezi Mungu akajaalia kuwe na mwaka uliogawanyika katika miezi, siku, nyakati za siku na saa. Vilevile, akachagua Ramadhan, kuwa mwezi mtukufu na siku bora akaifanya kuwa ni Ijumaa, na Lailatul Qadri akaufanya kuwa usiku mtakatifu na akafanya saa ya kukubaliwa dua ipo Ijumaa.

Kadhalika, Mwenyezi Mungu amejaalia masiku matukufu yapo kwenye siku kumi za mwanzo wa mfungo tatu, Dhul-Hijja.

Allah akawaumba wanadamu, akawachagua aliowathamini kuwa ni Waumini; na na akawachagua katika Manabii kutoka miongoni mwa Waumini, akawapandisha cheo Manabii fulani na wakaitwa ‘Rasul.’ Na katika hao Rasul akawapandisha vyeo wengine wkaitwa Ulul–‘azm. Bado katika hao Ulul– ‘azm akatubainishia vipenzi vyake huku kiongozi wao akiwa ni Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Muislamu amebarikiwa na Mwenyezi Mungu, na akawekewa madaftari mawili – moja la kuandikiwa mazuri yake na jengine la kuandikiwa mabaya yake. Ama kafiri aliwekewa daftari moja tu analoandikiwa mabaya tu.

Hivyo, ni juu ya Muislamu aweke lengo ya kwenda peponi na ajizatiti kiibada katika kila msimu. Hii ni siri aliyotueleza Mwenyezi Mungu na Mtume.

Kwa kweli kuruzukiwa umri na kuishi hadi kushuhudia siku kumi za mwanzo wa mwezi mtukufu wa Dhul-Hijja ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa neema hiyo, inatupasa tumshukuru Allah Aliyetukuka kwani amali njema katika masiku hayo zina thawabu nyingi mno.

Tunapokaribia kuingia katika mwezi wa Dhul-Hijja, tujue kuwa siku kumi hizi za mwanzo ni bora kabisa mbele ya Allah Aliyetukuka. Amali yoyote itakayotendwa katika miezi hiyo ni yenye kupendwa mno na Allah.

Swahaba Mtukufu Ibn Abbas (Allah amridhie) amehadithia kwamba Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakuna siku ambazo ndani yake matendo mema yanapendwa mno na Allah kama yanayotendwa katika) siku kumi hizi.” (Yaani: siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijja).

Wakauliza (Maswahaba): “Ewe Mjumbe wa Allah! Je, hata kuliko Jihad katika njia ya Allah?” Akajibu: “Hata Jihad katika njia ya Allah isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo.” [Bukhari].

Ewe ndugu Muislamu! Usiache fursa hii kukupita bila kujichumia thawabu tele kutokana na uzito wa malipo katika masiku haya. Katika safu hii tunapenda kuwanasihi Waislamu kuhusu fadhila za masiku haya kumi ya Dhul-Hijja. Pia, tunapenda kuwanasihi Waislamu juu ya matendo ya kufanya katika masiku haya matukufu kabisa mbele ya Allah Aliyetukuka.

Kwa jinsi siku hizi zilivyokuwa na umuhimu mkubwa, Allah Aliyetukuka ameziapia katika Qur’an pale aliposema” Anaposema: “Naapa kwa Alfajiri. Na kwa masiku kumi.” [Qur’an, 89: 1-2]. Wanachuoni wafasiri wa Qur’an wamekubaliana kwamba zilokusudiwa hapo ni siku kumi za Dhul-Hijja.

Katika siku hizi tunapaswa kumdhukuru mno Allah Aliyetukuka kwa kukumbuka neema zake zisizohesabika kama kwetu. Mwenyezi Mungu anasema:

“Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allah katika siku zinazojulikana.” [Quran, 22:28]. Ibn Abbas (Allah amridhie amesemna: “Hizo ni siku kumi za Dhul-Hijja.” Na amesema: “Manufaa ya Dunia hii na ya Akhera.”

Manufaa ya Akhera yanajumuisha kupata radhi za Allah. Manufaa ya vitu vya Dunia yanajumuisha wanyama wa kuchinjwa na biashara. [Rejea: ‘Tafsir Ibn Kathir’].

Kutokana na ilivyotajwa katika usimulizi wa Hadith tuliyoitaja hapo awali, matendo yoyote utendayo katika siku kumi hizi ni bora kuliko kwenda kupigana Jihad vitani. Tukumbuke kuwa, isipokuwa kwa mwenye imani ya hali ya juu aliyetayari kufa Shahidi, Jihad ni jambo zito mno kwa mtu kuliitikia kwani huko kuna mashaka mbalimbali ikiwemo kupoteza mali, hofu ya kujeruhiwa na kupoteza viungo vya mwili, kufariki na kadhalika.

Kwa hiyo, mwisho wa siku tunahimiza kuwa usidharau matendo amali yoyote. Hata iwe ndogo vipi itekeleze amali hiuo kwani Allah Aliyetukuka ni Al-Jawwaad (Mwingi wa Ukarimu), Al-Kariym (Mkarimu), Al-Wahhaab (Mwingi wa kutunuku, Mpaji wa yote), AlMajiyd (Mwingi mno wa vipawa na ukarimu).

Vile vile, miongoni mwa fadhila na ubora wa siku hizo takatifu ni kwamba zinajumuisha ibada zote katika siku hizi ikiwemo sala, funga, sadaka na Hijja. Ibada hizi hazijumuiki pamoja wakati mwingine wowote.

Aidha, msimu wa ibada wa siku hizi kumi, haupatikani ila kwa mwaka mara moja. Dakika zake, saa, siku na wiki, ndizo zinazompendeza Mwenyezi Mungu, kwa hiyo lau mwanadamu atajitahidi kiibada siku hizi atakuwa amefaulu sana.

Katika siku hizi kumi, siku ya tisa ni Arafa ambayo inajulikana kwa thawabu na msamaha mwingi kutoka kwa Allah. Hii ndiyo siku Waumini wanapeleka dua zao kwa wingi.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Dua bora nzito ni ya siku ya Arafa.” Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Waumini – mahujaji na wasiokuwa mahujaji – wanaacha machafu yao kwa ajili ya Arafa. Pia, mwenye kufunga siku hii, husamehewa madhambi ya mwaka uliopita na mwaka ujao.

Pia, ipo siku ya mwisho, tarehe kumi ya mfungo tatu inayojulikana kuwa ni siku ya kuchinja. Katika siku hii zipo ibada tofauti tofauti ikiwemo kutupa vijiwe, kunyoa, kutufu, kukimbia baina ya Swafaa na Marwaa, kuchinja na kuswali Idd.

Fadhila za siku hii ni nyingi. Muislamu wanatakikana wasizipoteze bali wazitumie kushindana katika kufanya mambo ya kheri.

Ndugu Muislamu, usighafilike. Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumba hivyo ulivyo na akakuchagulia alichokuchagulia na akakupa nawe nafasi ya kujichagulia vile utakavyo. Hivyo, kuwa na moyo, uchume juani kwa muda mfupi na ukale kivulini kwa muda mrefu kwenye maisha ya milele.

Kwa kuwa Allah ametudokezea misimu tofauti yenye malipo mengi ikiwemo masiku kumi haya 10 ya mwanzo ya mfungo tatu na usiku wa Lailatul-Qadr, basi nasi tuzidishe ibada katika siku hizo kwa kusali, kufunga, kutoa sadaka, kuleta tasbihi, tahlili na mwisho kuswali Idd na kuchinja

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close