4. Darasa La Wiki

Elimu ni kinga kwa vijana dhidi ya fikra za ugaidi

Aya ya kwanza kuteremshiwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ilikuwa wito wa kutafuta elimu. Wito huo wa Allah Aliyetukuka ulitokana na kutambua mchango na nafasi ya elimu katika kuendeleza jamii na kuilinda nchi na dunia kutokana na maovu na mabaya ya aina zote.

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu alitoa amri kwa Mtume wake asome. Kusoma ndiyo msingi na hatua ya kwanza kabisa ya kutafuta elimu. Aya hii inaonesha kwa uwazi athari ya elimu na nafasi yake katika Uislamu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba. Amemuumba binaadamu kwa tone la damu. Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.” [Qur’an, 96: 1-5].

Elimu ni njia ya pekee ya kuleta amani na utulivu kwa umma. Elimu inawachochea wananchi kuendeleza na kulinda jamii na nchi yao na ndiyo maana siyo jambo la kushangaza kukuta Uislamu ukiipa elimu heshima kubwa na kuwapa wanazuoni cheo cha juu kabisa mpaka wakawa warithi wa Manabii na Mitume.

Kama hiyo haitoshi, Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amewafanya wanazuoni kuwa mashahidi wa Upweke wake kama alivyosema katika Qur’an: “Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye elimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima.” [Qur’an, 3:18].

Naye Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) aliwafaradhishia Waislamu kutafuta elimu na akabainisha ubora wa wenye elimu dhidi ya wasio na elimu. Uislamu unawataka Waumini kujifunza. Kwa kuwa vijana ndiyo nguzo muhimu zaidi katika umma wowote, basi wao wanatakiwa kuwa na elimu ya kutosha ili waweze kukabiliana na mawimbi yanayowavuta katika fikra kali na misimamo ya kigaidi.

Kuna majaribio mengi ya kushawishi vijana kuingia kwenye misimamo mikali. Wale wanaowashawishi vijana wanaelewa uwezo wa kundi hili wa kujenga au kuangusha umma wowote. Ni kwa sababu hii, tunawahimiza vijana wajikinge na majaribio ya ushawishi huu wa kuingizwa katika mambo mabaya.

Kinga kwa kijana dhidi ya majaribio hayo haitapatikana isipokuwa kupitia elimu. Ni elimu ndiyo itakayomkinga kijana dhidi ya mafisadi wanaojitahitahidi kuchafua akili zao na kuwatumia vibaya. Pia ni kazi yetu kuwakinga na kulinda vijana wetu dhidi ya shari na fitina hizo.

Inafahamika kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya umma na ni moja ya sababu zinazopelekea katika mafanikio.

Na kwa hakika, jamii isiyo na elimu ni rahisi kushawishiwa na kuharibika na ndiyo maana makundi ya kigaidi yanajaribu kuwavuta vijana wasio na elimu ya kuwasaidia kupembua haki na batili. Hata hao baadhi ya vijana wenye elimu, mara nyingi si kiwango wala aina ya elimu inayoweza kuwalinda dhidi ya hatari ya kushawishiwa na kuathirika kwa fikra mbaya za ukatili, vurugu na ugaidi.

Kama nilivyotangulia kusema, mafisadi wanatambua nafasi na uwezo wa vijana katika kubadilisha mambo katika umma; na hakika hiyo ndiyo sababu watu hao wanaotaka kueneza vurugu na ugaidi duniani wanapenda kuwatumia vijana.

Watu hao wabaya wanajua kuwa, vijana ndiyo silaha muhimu ya umma wowote, ndiyo msingi wa maendeleo ya umma na ndiyo tegemeo la jamii. Vijana ni hazina ya kiuchumi, kijeshi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Lakini hazina muhimu iliyo ndani ya vijana kwa umma wowote ni hazina ya utu.

Kama ukitaka kujua mustakabali wa taifa lolote, basi usiuliza juu ya dhahabu yake na hazina yake ya kifedha, bali angalia vijana wake na mambo gani wanayoshughulikia. Ukiwakuta vijana hao wanashikilia dini, tambua kuwa hilo ni taifa kubwa lenye hadhi nzuri.

Ama ukiwakuta vijana wamepoteza maadili na wana tabia mbaya, basi ujue kuwa ni hilo ni taifa dhaifu (nyonge) litakaoanguka kwa haraka mbele ya madui zake. Kwa hivyo basi, vijana ni msingi wa umma na sababu ya kuimarika au kuanguka kwake.

Laiti shughuli ya kupambana na ugaidi wa kifikra ingelianza mapema, ingekuwa na manufaa makubwa. Njia kubwa ya kupambana na ugaidi ni mazungumzo na kushauriana ili kuunda dhana sahihi, kubainisha haki na kudhihirisha ufisadi wa baadhi ya itikadi.

Watu, taasisi na mamlaka mbalimbali zipambane na ugaidi ili walioshawishiwa kuharibu nchi, kufanya vurugu na mauaji, kusababisha ghasia na uharibifu wa aina yoyote waelewe kuwa wanafanya hatia kubwa zilizokatazwa katika sheria ya Kiislamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close