4. Darasa La Wiki

Deni na taratibu zake

Ni kawaida kwa mwanadamu kufikwa na shida ama mkwamo wa kimaisha na akahuzunika kwa kushindwa kutatua shida hiyo.

Hapo, mtu huyo, huangalia kulia na kushoto kutafuta nduguye kifamilia au nduguye katika imani, juirani, urafiki ili amsaidie.

Kwa upande mwengine, anakuwa hayuko tayari kuomba kutatuliwa shida yake hiyo bure (kwa gharama za nduguye) wakati anatarajia hapo baadae mambo yake yatakaa sawa.

Katika mazingira kama hayo, Uislamu umeweka utaratibu wa kukopeshana kwa muda maalumu. Utaratibu huu ni wa kimaumbile katika jamii ya watu wanapoishi pamoja.

Makosa katika utaratibu wa kukopeshana

Hata hivyo, tunadhani kuwa, suala hili ni nyeti mno na Waislamu hawajalifahamu vya kutosha. Matokeo ya hali hiyo, Waislamu wamekuwa wakikopeshana kiuzoefu – zoefu, bila ya kufuata maagizo ya sharia, hali inayopelekea kudhulumiana na baadhi yao kula mali za wengine bila ya haki.

Makala yetu hii ina lengo la kufafanua hukumu na taratibu za kukopeshana kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu kwa kadri inatakavyowezekana, InshaAllah.

Maana ya deni, kukopeshana

Deni ama mkopo ni maelewano ya hiyari baina ya watu wawili au zaidi ya kuchukua kitu halali kwa mtu au watu kwa lengo la kurejesha mfano wake kwa muda watakaokubaliana.

Uislamu umeruhusu mtu kukopa kitu chochote halali chenye maslahi na manufaa iwe pesa taslim au kifaa.

Umuhimu wa kutoa mkopo

Katika sharia ya Kiislamu, kukopesha ni moja ya vikurubisho vikubwa kwa Allah kwa sababu kunapelekea watu kuamiliana kwa huruma, upendo na upole. Yule aliyekopesha anamrahisishia anayekopeshwa mambo yake ya maisha na kumuwezesha kutatua shida zake.

Uislamu umewataka matajiri wawakopeshe masikini na mafukara, na Uislamu ukawaahidi malipo makubwa wenye nacho watakaokopesha wenzao wasiionacho, licha ya kwamba watarejeshewa kile walichokopesha. Katika hadith maarufu sana, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Mwenyezi Mungu yu katika kumsaidia mja madamu mja huyo humsaidia nduguye”

Na katika hadith ya iliyopokewa na Imam Tirmidhi na kuhadithiwa kutoka kwa Barraa bin Aazib (Allah amridhie) Mtume amesema :

“Mtu ambaye anapenda Allah amuokoe na matatizo ya Siku ya Kiyama, basi na amtatulie au amuondolee shida nduguye aliyefikwa na uzito.”

Katika kuonesha nafasi na umuhimu wa muamala huu, Qur’an imehimiza watu kukopeshana na kufafanua hukumu na sheria za deni kwa ufasaha kabisa. Katika aya hii ndefu zaidi kuliko zote a msahafuni, maarufu kwa jina la aya ya deni, Mwenyezi Mungu anaweka maelekezo makini yakiwemo, ikiwemo kuweka kumbukumbu ya maandishi na kuweka Mashahidi.

Kuandika deni na kuweka mashahidi

Utaratibu wa kuandika madeni na kuyawekea Mashahidi ameshauelekeza Allah katika kitabu chake kitukufu kama ifuatavyo, pale aliposema: “Enyi mlioamini, mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi iandikeni. Na muandishi aandike baina yenu kwa uadilifu. Wala mwandishi asikatae kuandika kama alivyomfunza Mwenyezi Mungu, basi naandike. Na ayatamke (maneno ya kuandikwa mkopaji) ambaye juu yake iko haki, naye amuogope Mwenyezi Mungu Mola wake, wala asipunguze chochote ndani yake. Kama Yule ambaye juu yake iko haki (mkopaji) amepumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe walii (msimamizi) wake kwa uadilifu.

“Na mshuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume (Waislamu); lakini iwapo hakuna wanaume wawili, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowakubali kuwa mashahidi, ili mmoja wao akipotea mwengine amkumbushe. Na mashahidi wasikatae waitwapo (kushuhudia).

“Wala msipuuze kuiandika (deni) iwe ndogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo bora mbele ya Mwenyezi Mungu, na imara zaidi kwa ushahidi, na pia ya kupelekea kuwa msiwe na shaka. Ila ikiwa ni biashara iliyohudhuria mnayouziana baina yenu, hapo si vibaya msipoiandika.

Na shuhudisheni mnapouziana. Na wala asitiwe taabu muandishi wala shahidi. Na kama mkifanya hivyo, basi hilo ni kosa kwenu, na muogopeni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anakufundisheni, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.” [Qur’an, 2:282].

Mazingatio

Huu ndiyo msingi wa nidhamu ama muamala wa kukopeshana, ambapo suala hilo limeruhusiwa pamoja na kuwekewa mkakati makini.

Katika aya tuliyoirejea hapo juu, tumeona msisitizo wa kuandika deni kwa ajili ya kutunza haki ya mkopeshaji na hata mkopaji pia.

Imetakiwa uwekwe muda maalumu wa kurejesha deni. Deni iwe kubwa ama ndogo ni vyema iandikwe na kopi za hati yake zihifadhiwe vyema mbele ya mkopaji na mkopeshaji.

Hekima ya hili ni kuwa mmoja ama wote (mdai na mdaiwa) wanaweza kufikwa na: (a) kifo hivyo deni kutofahamika kwa walio hai. (b) kusahau kama kweli waliwahi kufanya muamala kama ule, (c) kutafautiana kuhusu kiwango cha deni. Mathalan, mkopeshaji anasema alimkabidhi laki mbili, wakati mkopaji anadai kwamba alipokea laki moja. Hapo itakuwa ndiyo mwanzo wa mgogoro.

Uislamu hautaki watu wahitalifiane hususan katika masuala ya mali ambayo ndiyo nguzo (msingi) ya maisha.

Kadhalika, pamesisitizwa kuwepo mashahidi, hata kama wanawake iwapo kutakuwa na upungufu wa mashahidi wa kiume kwa lengo la huhifadhi haki na kuzirejesha kwa wenyewe.

Aidha, kumependekezwa kuwekwe ushahidi tunapouziana vitu ana kwa ana, hata kama siyo kwa kuandikishana. Aya imeishia kuwataka Waumini wamche Mola wao wanapofanya miamala yao wasije kudhulumiana.

Na katika Sunna, kuna hadith nyingi zinazoelezea kanuni za deni, kama tutakaziona hapo baadae inshaAllah.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close