4. Darasa La Wiki

Bila hekima na maarifa, elimu haina tija

Naam ! Ndugu yangu msomaji wa safu hii ya ‘Nasaha za wiki’, ujumbe wangu wa leo unatoka katika Qur’ an [3:164] inayosema: “Hakika Allah amewafanyia wema mkubwa Waumini pale alipowaletea Mtume kutokana na wao wenyewe, anayewasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na Hekima, japokuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu wa wazi.”

Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu anawakumbusha Waumini neema kubwa ya kuwaletea Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), ambaye ujio wake si tu rehema kwa wanadamu bali viumbe wote wakiwamo wanyama, ndege, wadudu na kadhalika.

Kwa upande wao, Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie wote) walifanya juhudi kubwa katika kuiandika Qur’ an na kuitafasiri, jambo ambalo lilileta mabadiliko ya mtazamo wa kiimani na kiitikadi kwa Waislamu wa zama zao na hata sasa.

Hii inadhihirisha wazi namna Maswahaba walivyotumia elimu na maarifa yao kuhakikisha wanaikusanya Qur’ an na kuiandika katika msahafu mmoja kwa maslahi ya Uislamu na watu wake.

Tunapoisoma historia ya uandishi wa kitabu kitukufu cha Qur’ an na kuenezwa kwake ulimwenguni, tunajifunza kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya hekima na maarifa ya mtu katika shughuli anazozifanya.

Kwa kutumia hekima, mtu hupanga mikakati yake ya muda mrefu na mfupi na kwa busara alizojaliwa huomba ushauri na kutafuta taarifa zote muhimu kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake. Kwa utaratibu huu, uwezekano wa mtu kuitumia vema elimu yake huwa mkubwa.

Hii ni kwa mambo yote ambayo mtu anakusudia kuyatekeleza iwe kazini, katika dini, biashara au kwenye masuala yanayohusu jamii inayomzunguka. Hekima, mipango sahihi na kumtegemea Mungu hufanya mambo yawe mepesi .

Katika makala yangu hii nitataja mambo matano ambayo Muislamu akiyazingatia na kuyafanyia kazi yanaweza kumfanya awe na hekima.

Mosi, kuelewa maana halisi ya hekima Zipo Aya nyingi na Hadithi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) zinazozungumzia maana na umuhimu wa kuwa na hekima, lakini kwa ufupi tunaweza kusema kwamba hekima ni kukiweka kitu katika mahali stahiki au kufanya maamuzi yasiyo na majuto. Kama hivyo ndivyo, basi kuanzia sasa jitahidi uwe mtu mwenye hekima.

Pili, kusoma visa vya waja wema Kudurusu (kurejelea) historia za Mitume na Manabii wa Allah (amani ya Allah iwashukie) na waja wema waliopita ni jambo muhimu liwezalo kukupeleka mahala ilipo hekima.

Nasema hivyo kwa sababu, visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya Mitume na waja wema wa Allah vina mchango mkubwa katika kukuondolea hofu, kudhibiti hasira, kuachana na ‘uteja’ wa jambo fulani na mambo mengine mengi kama hayo.

Ni muhimu kufuata mwenendo wa waja wema kwa sababu ndiyo wanaotupa mifano halisi ya tabia za hekima na zisizo za hekima. Pia ifahamike wazi kuwa kushikamana na mwenendo wa waja wema waliotangulia si jambo geni lililozuliwa kama wanavyodai baadhi ya watu, hivyo ni wajibu kwetu kujipamba na sifa na mwenendo wao kwani kufanya hivyo ndiyo uongofu wa sawa sawa.

Allah Ta’ala anasema: “Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.” [Qur’an, 12:108].

Nikinukuu kauli ya Mwanachuoni Sheikh Swalih bin Fawzaan al Fawzaan aliyobainisha katika kitabu ‘Salafiyyah Uhakika wake na sifa zake’. Katika ukurasa wa nne wa kitabu hicho Sheikh anasema: “Kushikamana na mfumo wa Salaf ndiyo suluhu.

Ni lazima mgawanyiko utokee na umeshatokea, kama alivyotujuza Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Njia ya uokovu ni kushikamana na yale aliyokuwa akifuata Mtume na Maswahaba zake (Allah awe radhi nao).

Kama tunataka kuwa katika kundi la watu wenye hekima, hatuna budi kufuata mienendo ya waja wema ili kufikia mabadiliko tuyatakayo.

Tatu, suhubiana na rafiki mwema Katika kukuza uzoefu wako kwenye masuala tofauti ya maisha, ni vizuri ukasuhubiana na rafiki mzuri, mchaMungu na mwenye hekima kwani kupitia urafiki mwema ndipo Allah humuokoa aliyepotea na kumuongo za aliyekosea.

Mwenyezi Mungu anasema: “Siku hiyo (ya Kiyama) marafiki watakuwa maadui wao kwa wao, isipokuwa wacha Mungu.” [Qur’an, 43:67].

Nne, tafuta elimu kwa watu wenye hekima Kusoma kwa maana ya kutafuta elimu huongeza upeo katika maisha yetu na kutuongoza kwenye njia ya kuielekea hekima. Hivyo, ni muhimu kuchukua elimu kutoka kwa watu wachamungu na wenye hekima.

Qur’ an Tukufu inamtaja Luqman kama mtu mcha Mungu, mwenye hekima
nyingi na tabia nzuri. Ni utukufu ulioje aliokuwa nao Luqman ambaye jina lake limetajwa katika Sura nzima ya Qur’an. Qur’an Tukufu imeyanukuu maneno ya Luqman mwenye hekima ili yawe muongozo wa watu wote ulimwenguni.

Tano, chunguza tabia zako na za wengine Kujichunguza tabia ni mtaji mkubwa katika kubadili mwenendo na tabia mbaya. Tunaweza kutambua tabia nzuri na mbaya kwa kujifunza na kujijua tulipo kimaadili.

Kwa kufanya hivyo, tunaweza pia kujua ikiwa sisi ni miongoni mwa wale wenye hekima au la. Ni muhimu kujichunguza kwa sababu bila hekima na busara elimu au maarifa tuliyonayo haviwezi kuwa na maana yoyote.

Hii ni kwa sababu hekima ndiyo jambo pekee linaloweza kukamilisha imani ya mtu na kuepukana na sababu zinazopelekea mtu kufanya mambo ya hovyo na yanayomchukiza Allah.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close